Uwekezaji katika soko la mitaji ya fedha na hisa inatajwa kama moja ya njia inayowavutia watanzania wengi sasa kujiingizia fedha bila ya msongo wa mawazo.
Eneo hili linatajwa kuchangamkiwa zaidi hivi sasa kutokana na kuendelea kuenea kwa elimu ya fedha na utambuzi mzuri wa fursa zilizopo katika masoko ya hisa.
Jambo hilo linawafanya wananchi kuchangamkia zaidi uwekezaji huo ikiwa ni baada ya baadhi yao kuwa tayari na kumbukumbu ya kupoteza fedha kupitia masoko mbalimbali yasiyokuwa rasmi yaliyowahi kuibuka kama Kalynda.
Ongezeko hili la utambuzi na kujua fursa zinazopatikana zimefanya sasa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kushuhudia ukuaji mkubwa wa mtaji ambao ulifikia Sh23.995 trilioni mwishoni mwa mwaka 2025.
Miongoni mwa maeneo yaliyoshuhudia uwekezaji mkubwa katika mwaka 2025 ni hisa za ambazo mauzo yake yalikuwa Sh5.848 trilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 86.04 ikilinganishwa na Sh3.1 trilioni mwaka uliotangulia.
Hatifungani za kampuni, mashirika ya umma na Serikali za mitaa katika mwaka 2025 zilifikia Sh12.12 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 174 ile iliyokuwapo mwaka uliotangulia.
Hatifungani ya mashirika iliyoongoza ilikuwa ni Samia Infrastructure kwa Sh4.19 bilioni, Hati fungani ya CRDB Kijani Sh3.65 bilioni, Bondi yangu ya Azania Sh2.2 bilioni na hatifungani ya jamii ya NMB Sh1.47 bilioni.
Kulikuwa na kupungua kwa Skuk kwa asilimia 86.73 hadi Sh214.19 milioni kutokatana na kutamatika kwa hatifungani ya Skuk ya benki ya KCB.
Hata hivyo zikijumlishwa hatifungani zote kwa mwaka huo zilishuhudia ongezeko kubwa la asilimia 86.08 kutoka Sh3.1 trilioni hadi Sh5.86 trilioni mwaka 2025.
Mtaalamu wa uchumi, Dk Goodhope Mkaro anasema hali hii imechangiwa na kazi kubwa inayofanyika sasa katika maeneo mbalimbali ambayo inalenga kuongeza uelewa juu ya uwekezaji wa masuala ya hisa.
Amesema hilo limekuwa likifanywa na wataalamu mbalimbali wa fedha hususani katika mitandao ya kijamii ambao wamekuwa wakiwafundisha watu na kuwahamasisha kutumia fursa ambazo zinapatikana katika eneo hilo.
“Ndiyo maana hamasa imeongezeka kutokana na kukua kwa uelewa wa mtu mmoja mmoja,” anasema Dk Mkaro.
Anasema ukuaji huo hauonekani kwa mtu binafsi pekee bali hata kwa kampuni nazo zimeanza kuwekeza katika hisa au hatifungani ili waongeze kipato pia kwa sababu uwekezaji huu ni ule ambao hatari zake ni chache.
“Hususani zile hatifungani za serikali, ndiyo maana unaona kampuni nyingi zinanunua hatifungani. Inaonesha kuwa kampuni zinafanya hivyo kwa ajili ya kupunguza hatari kibiashara.
Naye mtaalamu wa huduma za fedha za kiislama (Islamic Finance Rashid Aziz anasema Sukuk ni bonds, zina misingi fulani kuzifanya ziwe tofauti na aina nyengine za bonds za kawaida, zinavutia wawekezaji ambao ni ‘faith conscious’ kuwekeza hivyo kuna haja soko ya kubuni huduma mbadala ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
“kwa mtazamo wa kanuni fedha za Kiislam, kwa wale wanaojali sana wanaona hii mfumo wa kawaida una changamoto na zaidi ni riba, sasa, mbadala unatoa mwanya wa kubadili mbinu ili, kile kinachoitwa riba kinabadilika , hiyo inawapa imani ya kuwekeza,” amesema Aziz.
Mtaalamu na mshauri elimu ya fedha na uwekezaji, Charles Ligonja anasema ukuaji huu unashuhudiwa kwa sababu serikali imewezesha kundi kubwa la watoa elimu ya fedha ambalo sasa linatumia muda mwingi kutoa elimu kuhusu masoko ya fedha na uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo mitandaoni.
Kundi hilo sasa linasaidia kuongeza Imani ya wananchi kuhusu uwekezaji katika masoko hayo wakati ambao wengi wao wameshaumizwa na majukwaa mbalimbali yaliyowahi kutokea yaliyowataka watu kuweka fedha ili wapate fedha kama Kalynda.
“Sasa uwepo wetu umekuwa msaada sana, inapotokea fursa zilizokuwa zinakuja wanatafuta kama hatifungani za Sukuk watu wanatupigia simu kutafuta taarifa za uhakika ukimuambia ni salama na mimi nimewekeza ukampa na Ushahidi anawekeza,” anasema.
Amesema kukosekana kwa uelewa wa kutosha ni moja ya jambo ambalo awali lilikuwa kikwazo lakini sasa wanapata elimu hiyo kwa urahisi. “Na mara nyingi sisi kama watoa elimu tumekuwa tukiwashauri kama hauna uelewa wa kutosha kuhusu uwekezaji fulani ingia kidogokidogo,” anasema.
Wanafanya hivyo kwa sababu wanaamini kuwa si kila mtu ni mfanyabiashara lakini pindi anapoeleweshwa vizuri anaona bora awekeze avune kidogokidogo.
Hata hivyo, licha ya mafanikio yanayoonekana Lugonja anasema elimu hii inapaswa kuelekezwa pia katika maeneo ya vijijini ili fursa hii itumike kwa watu wote kwani sasa watu wa mijini ndiyo wanaoonekana kunufaika zaidi.
Anasema ili kufikisha elimu hiyo, vyombo vya Habari vinaweza kuwa na nafasi kubwa ikilinganishwa na mitandao ya kijamii kwani watu wengi wanaamini kinachosemwa katika vyombo mbalimbali.
“Baadhi wakiona vitu mtandaoni hawaamini lakini wakiona katika luninga au magazeti akiona na mtandaoni kitu kilekile imani inaongezeka na mwisho wa siku na yeye anaingia. Uwekezaji huu usiwe tu kwa ajili ya watu wa mjini,” anasema.
Maneno hayo yaliungwa mkono na Zakia Hamduni ambaye pia hutoa elimu ya fedha na uwekaji akisema vyombo vya habari vinaweza kuwa msaada kwa jamii ili iweze kutambua majukwaa sahihi ya kuwekeza.
“Kukosekana kwa taarifa sahihi ndiyo maana watu wakisikia sehemu ukiwekeza unapata hela nyingi wanakimbilia, wanasahau kuwa hakuna hela ya haraka, hela yoyote ya halali lazima uwe mvumilivu,” amesema.
Amesema uwekezaji kwa sasa ndani ya soko la hisa na hatifungani unaongezeka kwa sababu watu wanakuwa na uhakika wa kupata fedha zao huku hatari ya kuzipoteza ikiwa ni ndogo tofauti na biashara.
“Kwenye biashara si kila mmoja anaweza kufanya vizuri na kuisimamia, pia hasara zipo zinazoweza kuzuilika na zisizoweza kuzuilika lakini huku ni kwa kiasi kidogo hivyo uwekezaji katika hisa unabaki kuwa njia bora ya uhifadhi wa fedha zako kwa faida,” amesema Zakia.
