Kwa zaidi ya nusu karne, ramani ya uzalishaji wa mafuta barani Afrika imekuwa ikitawaliwa na mataifa ya Afrika Kaskazini na Afrika Magharibi, hususan Nigeria, Angola, Algeria na Libya.
Mataifa haya yamekuwa yakichangia sehemu kubwa ya uzalishaji, mauzo ya nje na mapato ya mafuta ya bara hili. Hata hivyo, taswira hiyo inaanza kubadilika taratibu huku Afrika Mashariki ikijipambanua kama eneo jipya lenye uzito mkubwa katika sekta ya mafuta, kufuatia uendelezaji wa miradi mikubwa nchini Uganda na Kenya.
Ugunduzi wa mafuta katika Bonde la Albert nchini Uganda na Bonde la South Lokichar nchini Kenya umefungua ukurasa mpya wa kiuchumi kwa ukanda huu, ambao kwa muda mrefu umeonekana kama mtumiaji zaidi wa mafuta kuliko mzalishaji.
Hivi sasa, matarajio ni kwamba ndani ya miaka michache ijayo, Afrika Mashariki inaweza kubadilika na kuwa kitovu kipya cha uzalishaji, usafirishaji na huduma za mafuta barani Afrika.
Uganda ndiyo nchi iliyoenda mbali zaidi katika safari ya kugeuza ugunduzi wa mafuta kuwa uzalishaji wa kibiashara. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Serikali ya Uganda, nchi hiyo ina akiba ya mafuta ghafi inayokadiriwa kufikia mapipa bilioni 6.5 ardhini, huku takribani mapipa bilioni 1.4 yakitajwa kuwa yanaweza kuzalishwa kibiashara kwa teknolojia ya sasa.
Mafuta hayo yaligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2006 katika Bonde la Albert, eneo linalopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tangu wakati huo, Serikali ya Uganda imekuwa ikiwekeza kwa tahadhari katika maandalizi ya muda mrefu, ikisisitiza kujenga mifumo ya kisheria, sera na taasisi kabla ya kuanza uzalishaji.
Mradi wa mafuta wa Uganda unahusisha ujenzi wa zaidi ya visima 400 vya uzalishaji katika vitalu vya Tilenga na Kingfisher, vinavyoendeshwa na kampuni za TotalEnergies na China National Offshore Oil Company (CNOOC).
Kwa mujibu wa Serikali, uzalishaji wa awali unatarajiwa kufikia wastani wa mapipa 200,000 ya mafuta kwa siku, huku uzalishaji huo ukitarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 25 hadi 30 kuanzia nusu ya pili ya mwaka huu (2026).
Serikali ya Uganda imekuwa ikisisitiza kuwa mafuta haya yanapaswa kuwa kichocheo cha maendeleo ya viwanda, miundombinu na ajira, badala ya kuwa chanzo cha utegemezi au migogoro ya rasilimali.
Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Ruth Nankabirwa, hivi karibuni amesema kuwa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umevutia takriban Dola za Marekani bilioni 4 za uwekezaji, jambo linaloonyesha imani kubwa ya kimataifa.
Alibainisha kuwa makubaliano yaliyopo yanatoa uwezekano wa kuchakata mapipa 60,000 ya mafuta kwa siku, huku ujenzi wa kiwanda cha kuchakata ukitarajiwa kuanza baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya utekelezaji.
“Mafuta ghafi yatakayobakia ambayo yanayokadiria kuwa karibu mapipa190,000 kwa siku, yatapelekwa na kuuzwa kupitia vituo vya kuhifadhi na usafirishaji wa nje vilivyo Tanga,” alisema.
Hata hivyo Mhimili mkuu wa uzalishaji wa mafuta wa Uganda ni EACOP. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, bomba hilo lina urefu wa takribani kilomita 1,443, likianzia Hoima magharibi mwa Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
EACOP linatajwa kuwa bomba refu zaidi la mafuta ghafi linalopashwa joto duniani, kutokana na tabia ya mafuta ya Uganda kuwa mazito (waxy crude). Bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha hadi mapipa 216,000 ya mafuta kwa siku, kiwango kinachotosha kuhudumia uzalishaji wa sasa na wa baadaye, ujenzi wake umefikia asilimia 79.
Akizungumza wakati wa ziara ya Tanga Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembe ambaye alikuwa na Mwenzake wa Uganda alisema asilimia 21 zilizosalia zitakamilishwa hadi kufikia Julai mwaka huu. “Mradi unaendelea vizuri utakamilika Julai mwaka huu”
Gharama za mradi huo zinakadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 5. Mradi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya TotalEnergies (asilimia 62), CNOOC (asilimia 8), Serikali ya Uganda (asilimia 15) na Serikali ya Tanzania (asilimia 15). Kwa Tanzania, mradi huu unaifanya nchi kuwa mshirika muhimu katika mnyororo wa thamani wa mafuta ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Kenya, safari ya mafuta imekuwa ndefu na yenye changamoto, lakini sasa inaonekana kuingia katika hatua muhimu. Mafuta yaligunduliwa mwaka 2012 katika Kaunti ya Turkana, katika vitalu vya T6 na T7 vinavyounda Bonde la South Lokichar.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Serikali ya Kenya, akiba ya mafuta yanayoweza kuzalishwa kibiashara katika Turkana inakadiriwa kufikia mapipa milioni 560. Ugunduzi huo uliweka Kenya katika ramani ya nchi zenye rasilimali za mafuta Afrika Mashariki, lakini pia ulifungua mjadala mpana kuhusu haki za jamii, mazingira na mgawanyo wa mapato.
Baada ya miaka ya kuchelewa, Serikali ya Kenya sasa iko katika hatua ya mwisho ya kuidhinisha Mpango wa Maendeleo wa eneo la Mafuta (Field Development Plan – FDP) uliowasilishwa na kampuni ya Gulf Energy.
Mpango huo tayari umeidhinishwa na Wizara ya Nishati na Petroli, na sasa unasubiri uamuzi wa Bunge.
Kwa mujibu wa maelezo ya Serikali, FDP ni nyaraka muhimu inayoeleza kwa kina namna mafuta yatakavyochimbwa, kuchakatwa, kusafirishwa na kuuzwa. Pia inaainisha gharama za mradi, idadi ya visima, kiwango cha uzalishaji, athari za mazingira na namna mapato yatakavyogawanywa.
Mpango wa sasa ni wa tatu kuwasilishwa kwa Serikali ya Kenya. Mpango wa kwanza uliwasilishwa mwaka 2021 lakini ulitupiliwa mbali kutokana na mapungufu ya kiufundi na kifedha. Marekebisho yaliyofuata mwaka 2023 nayo hayakuridhisha kikamilifu, kabla ya Gulf Energy kuwasilisha mpango mpya Septemba 2025, sambamba na ununuzi wa mradi huo kutoka Tullow kwa dola milioni 120.
Mpango huo unapendekeza utekelezaji wa mradi kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inalenga uzalishaji wa mapipa 20,000 kwa siku kupitia visima 48 katika maeneo ya Ngamia na Amosing. Awamu ya pili itaongeza uzalishaji hadi mapipa 50,000 kwa siku kupitia zaidi ya visima 800 katika vitalu sita.
Mwezi uliopita Rais wa Kenya William Ruto alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo wa mafuta Serikali itahakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hiyo kikamilifu hususani wakazi wa Turkana.
“Kaunti ya Turkana haitabaki nyuma tunapopita katika safari ya ajenda yetu ya mabadiliko ya kitaifa. Ili kufungua uwezo kamili wa rasilimali za mafuta katika Turkana na kuhakikisha faida halisi kwa wananchi wake,” alisema Ruto.
Usafirishaji na mapato
Kwa mujibu wa FDP, mafuta ya Turkana yatasafirishwa kwa malori hadi Bandari ya Mombasa katika awamu ya kwanza, kabla ya kuanza kusafirishwa kwa reli katika awamu ya pili.
Awali, Serikali ya Kenya ilikuwa imepanga kujenga bomba la mafuta kutoka Turkana hadi Lamu chini ya mradi wa LAPSSET, lakini mpango huo uliachwa kutokana na gharama kubwa na changamoto za kibiashara.
Uamuzi wa kutumia barabara na reli unatajwa kupunguza gharama za awali za mradi na kuruhusu uzalishaji kuanza mapema, jambo linaloendana na malengo ya Kenya ya kuanza kuuza mafuta nje ya nchi kabla ya mwisho wa 2026.
Kwa mujibu wa takwimu zilizomo katika FDP, Serikali ya Kenya inatarajiwa kupata mapato ya takribani dola milioni 864 katika kipindi cha miaka 25 hadi mwaka 2050. Kati ya kiasi hicho, dola milioni 648 zitaelekezwa kwa Serikali Kuu, dola milioni 173 kwa serikali za kaunti na dola milioni 43 kwa jamii za wenyeji.
Makadirio hayo yanategemea bei ya mafuta ya dola 60 kwa pipa, gharama za mradi zinazokadiriwa kufikia dola bilioni 4.65 na viwango vya uzalishaji vilivyopangwa. Serikali imeeleza wazi kuwa mapato hayo yanaweza kubadilika kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta duniani.
Licha ya fursa kubwa, changamoto ni nyingi. Masuala ya mazingira, haki za jamii, mabadiliko ya tabianchi na mpito wa nishati safi yanaendelea kuweka shinikizo kwa miradi ya mafuta. Serikali za Uganda na Kenya zimekuwa zikisisitiza kuwa miradi yao itaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya mazingira na uwajibikaji wa kijamii.
Kadri Uganda inavyojiandaa kuanza uzalishaji wa mafuta na Kenya ikisubiri uamuzi wa mwisho wa Bunge, jambo moja ni wazi: Afrika Mashariki ipo katika hatua ya kihistoria. Ikiwa fursa hii itatumika ipasavyo, ukanda huu unaweza kuibuka kama kitovu kipya cha uzalishaji wa mafuta barani Afrika, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
