Dar es Salaam. Macho na masikio ya wanachama wa ACT Wazalendo yataelekezwa Jumapili Januari 18, 2026 wakati chama hicho, kitakapofanya uamuzi wa kuingia au kutoingia kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar.
Uamuzi wa ACT – Wazalendo kuingia au kutoingia ili kuunda SUK Zanzibar, utafanyika siku hiyo katika kikao cha kamati kuu, ambacho pamoja na mambo mengine suala hilo, litachukua nafasi kubwa miongoni mwa wajumbe.
Kikao hicho ni cha kwanza tangu kumalizika wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambao ACT Wazalendo, kilipata wabunge wanane katika majimbo ya Tanzania bara na Zanzibar kati ya 272.
Pia, katika uchaguzi huo, ACT Wazalendo, kilipata viti 10 vya wawakilishi wa majimbo na viti maalumu vinne. Mgombea urais wa chama hicho Zanzibar, Othman Masoud alishika nafasi ya pili, baada ya mgombea wa CCM, Dk Hussein Mwinyi kuibuka kidedea.
Dk Mwinyi alipata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 na Othman Masoud alipata 139,399 sawa na asilimia 23.22.
Ni kamati kuu iliyobaki na uamuzi baada ya chama hicho kutanguliza mguu mmoja kuelekea SUK, kutokana na majadiliano ya makubaliano yanayoendelea yakikaribia hatua za mwisho.
Taarifa zinaeleza ajenda zingine zitakazojadiliwa ni tathimini ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, ulivyokwenda, hali ya kisiasa katika nchi na mipango ya chama hicho kwa siku za usoni.
“Katika ajenda ya kisiasa nchi, itajadili suala SUK na kupokea taarifa ya maendeleo kuhusu mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kisha tutatoa uamuzi wa kuingia au kutoingia.
“Taarifa kuhusu mwenendo wa SUK, itatolewa na kamati ya mashauriano upande wa Zanzibar, ambayo inaratibu mchakato huo,” amesema mmoja wa vigogo wa chama hicho alipozungumza na Mwananchi.
Kwa mujibu wa kigogo huyo, kuna mambo ya msingi yanayotakiwa kufanyika au kuwekewa utaratibu wa kupata ufumbuzi ili chama kiamue kuhusu mwenendo wa SUK.
“Sasa hiyo taarifa kamati ya mashauri itakayotupa mwongozo,” amesisitiza Kigogo huyo.
Wakati kigogo akieleza hayo, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Bara, Ester Thomas ameliambia Mwananchi leo Jumatano Januari 14, 2025 maandalizi ya kikao hicho kitakachofanyika makao makuu ya chama hicho Magomeni , jijini Dar es Salaam yanaendelea vizuri.
Ester amesema katika kikao hicho watajadili tathmini ya uchaguzi na namna chama hicho kitakavyoweka mikakati ya namna ya kusonga mbele kutoka hapo kilipo.
“Lazima tuwe na uamuzi kuhusu msimamo wa chama baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, jinsi gani tutasonga mbele au tunaelekea wapi. Hiki kikao ndicho kitakachotoka na msimamo,” amesema Ester.
Alipoulizwa kuhusu SUK, Ester amejibu akisema, “hili pia litajadiliwa katika kamati kuu na itakuwa sehemu ya msimamo wa chama, kwa pande zote Tanzania bara na Zanzibar,” ameeleza Ester.
Kati ya Januari 5 hadi 9, mwaka huu viongozi wakuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu na Isihaka Mchinjita walifanya ziara kwenye baadhi ya majimbo ya mikoa ya kusini na kaskazini.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa kusikiliza maoni ya viongozi wa maeneo hayo na waliokuwa wagombea kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 na kufafanua misimamo mbalimbali iliyochukuliwa na chama hicho, baada ya mchakato huo.
Kwa sasa kinachosubiriwa ni ACT Wazalendo kuwasilisha barua kwa Dk Mwinyi yenye jina la mwanachama atakayeteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Novemba 2025, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Ahmed Said aliiandikia barua ACT Wazalendo ikiitaka ipeleke jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman aliwaambia wanachama wa chama hicho, akiwa ziarani Pemba, kuwa hawakupeleka jina wakati huo, kwa sababu ya kutoridhishwa na mazingira ya kisiasa.
Kutokana na yanayoendelea na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Zanzibar, kushawishi na kuanza kutekeleza baadhi ya masharti yaliyowekwa na chama hicho, huenda kikao cha kamati kuu kitatoa mwanga.
Kwa mujibu wa baadhi ya wanachama na viongozi waandamizi wa ACT Wazalendo, huenda chama hicho, kikaingia SUK ambapo ni takwa la kikatiba, lakini pia kwa mustakabali wa Zanzibar wa kuimarisha umoja na mshikamano.
Kauli ya kwamba ‘yupo tayari kutekeleza maridhiano na kuunda SUK’ iliyotolewa na Rais Mwinyi Novemba 10, 2025, wakati akizindua Baraza la Wawakilishi ni miongoni mwa mambo yanayochochea ACT Wazalendo kushiriki kuunda Serikali.
“Nitaheshimu maridhiano na nipo tayari kuunda SUK kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar,” alisema Dk Mwinyi. Hata hivyo, alipotangaza Baraza la Mawaziri, aliacha nafasi nne zitakazozibwa na wajumbe kutoka ACT Wazalendo.
Hadi leo Alhamisi Januari 15, zitakuwa zimebaki siku 26 kati ya 90 zilizotolewa na Dk Mwinyi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kuhusu ACT Wazalendo kuingia SUK.
Endapo muda huo utapita bila uteuzi kufanyika, Rais anakuwa na mamlaka ya kuunda Serikali ya chama kimoja, hali inayomaanisha kuwa upande wa upinzani unapoteza sifa za kushiriki serikalini.
Wizara hizo ambazo zimeachwa ni ya Utalii na Mambo ya Kale, Wizara ya Afya, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
