Moshi/Dar. Mtuhumiwa kujinyonga akiwa mahabusu anakoshikiliwa na jeshi la polisi ni uzembe au bahati mbaya? Hili ni swali linalohitaji majibu ya kina kutokana na matukio ya namna hiyo kutokea kwa nyakati tofauti.
Swali hilo linaibuka baada ya kifo cha Michael Lambau (18), mkazi wa Mtaa wa Karikacha, Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambaye anadaiwa kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Kikuu cha Moshi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, kifo hicho kilitokea Januari 13, 2026, siku hiyohiyo ambayo mtuhumiwa alikamatwa kwa tuhuma za kumshambulia na kumpiga kwa bapa la panga, baba yake mdogo Brian Felix.
Kamanda huyo wa Polisi mbali na kusema Jeshi la Polisi linachunguza tukio hilo, amesema awali Lambau alikuwa akituhumiwa kufanya tukio la mauaji ya baba yake mzazi Novemba 22, 2025 kwa kumchoma kitu chenye ncha kali shingoni, na alitoroka hadi alipokamatwa kwa tukio hilo la shambulio la kudhuru mwili.
Ingawa tukio hilo limezua sintofahamu lakini si la kwanza kutokea nchini. Kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwa na mfululizo wa visa vya vifo vya mahabusu katika vituo vya polisi, vingi vikidaiwa kusababishwa na kujinyonga.
Miongoni mwa matukio hayo ni la Mussa Martine (17), mkazi wa Kijiji cha Kerende, Kata ya Kemambo wilayani Tarime mkoani Mara, aliyekutwa amekufa katika Kituo cha Polisi Nyangoto usiku wa kuamkia Agosti 22, 2017, akidaiwa kujinyonga kwa kutumia shati lake.
Jingine la Nicholas Mushi (27), ambaye alidaiwa kujinyonga kwa kutumia tambara la dekio akiwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi usiku wa kuamkia Septemba 13, 2022.
Aidha, Daud Matola (41), mkazi wa Namtumbo mkoani Ruvuma, alikutwa amefariki dunia Machi 2017 akiwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea, ikidaiwa alijinyonga.
Matukio mengine ni la Victoria Edward (51), mkazi wa Arusha, aliyekutwa amekufa baada ya kudaiwa kujinyonga ndani ya chumba cha mahabusu katika Kituo cha Polisi Arusha Agosti 24, 2016.
Pia, tukio la Mwita Makwabe (52) aliyekutwa amejinyonga chooni akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Sirari mkoani Mara mwaka 2016.
Vilevile, Bosco Ndunguru (40) alikutwa amefariki dunia akidaiwa kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma mwaka 2015.
Katika jiji la Dar es Salaam, Stella Moses (30) aliripotiwa kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Mburahati mwaka 2020.
Lingine lililozua maswali zaidi ni la Ofisa wa Polisi Grayson Mahembe (26), aliyedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara Mjini Januari 22, 2022.
Mfululizo huu wa matukio ya watuhumiwa kujinyonga wakiwa mahabusu katika vituo vya polisi wanakoshilikiwa kwa makosa mbalimbali umekuwa ikiibua swali au maswali kwa jamii.
Miongoni mwa maswali ambayo baadhi ya Watanzania wanajiuliza ni pamoja na ni vipi mtuhumiwa anaweza kujinyonga akiwa chini ya ulinzi wa polisi? Wanatumia vifaa gani? Je hawakaguliwa ipasavyo?
Ni maswali yasiyokuwa na majibu, hata baadhi ya wadau wa haki za binadamu na wanasheria waliozungumza na Mwananchi wamesema ni ngumu kujua moja kwa moja kama wamejinyonga au wamekufa kwa sababu nyingine.
Hata hivyo, wadau hao wameshauri ndugu au marafiki wanaofikwa na kadhia kwenda mahakama ya Corona (inayochunguza vifo vya kutatanisha) ili kushinikiza kufanyika kwa uchunguzi wa vifo vyenye utata.
“Katika hali ya kawaida ni ngumu kusema kama kweli wamejinyonga au hawa, ndio maana tunahitaji ile mahakama ya Corona katika hatua kama hii ya vifo vya aina hiyo vinatakiwa vichunguzwe,” amesema Fulgence Masawe ambaye ni Mkurugenzi wa Utetezi na Ufikiuaji wa Haki wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Amesema: “Tunavyojua mtu akiwa mahabusu atakiwi kuingia na kitu chochote, kutokana na ukaguzi, je anajinyongaje, je mahabusu alikuwa na nani? Wakati mwingine kuna walakini kujua kama wamejinyonga na kuna mengine wanakutana nayo.”
Kwa mujibu Masawe, ili kuondokana na changamoto hiyo watu watakaokumbwa na kadhi hiyo, wanapaswa kwenda mahakama ya Corona ili kufungua kesi ya kuomba uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu kifo cha utata cha mpendwa wao.
Wakili John Mallya aliungana na Masawe, akisema kama ndugu wana wasiwasi kuhusu kifo cha mpendwa wanapaswa kutumia sheria ya upelelezi wa vifo kwa kwenda mahakama ya Corona itakayochunguza.
“Wanakwenda mahakamani na kuomba kufanyika kwa uchunguzi wa kifo fulani, hivyo hakimu wa kawaida, anageuka kuwa Corona na kuchagua watu watalaamu wa afya watakaouchunguza mwili wa marehemu mochwari,” amesema.
“Baada kuuchunguza wanapeleka ripoti mahakamani ambapo hakimu ataitumia sehemu ya uamuzi wake,” amesema Mallya.
Mbali na wadau, Mwananchi limezungumza limefika nyumbani kwa Lambau na kuzungumza na msemaji wa familia, baba mdogo wa kijana huyo, Today Rambau, amesema wameshangaa kupata taarifa za kijana wao kujiua kwa kujinyonga kituo cha polisi hali ambayo amesema imewapa mshituko.
“Hili tukio ni tukio la mshituko sana kwa sababu mtu amechukuliwa leo (Januari 13) halafu unapewa taarifa eti kajiua ndani ya mahabusu, hili sio jambo la kufurahisha hata kidogo,” amesema baba mdogo wa marehemu.
Kuhusu tukio la kumshambulia baba mdogo wake, amesema Januari 12 kijana huyo (marehemu) alitofautina na baba mdogo wake wakati alipochukua spana za gari kwenye gari la marehemu baba yake ambaye alifariki Novemba 22, 2025.
“Michael (marehemu) alikamatwa juzi Jumatatu kwa tukio la kumshambulia baba yake mdogo kwa kumpiga na bapa, hivyo alikamatwa jana mchana, Januari 13 na kupelekwa kituo cha polisi,” amesema Rambau.
“Nilivyoelezwa sababu ya kumshambulia baba yake mdogo ni kwamba walikuwa wanagombania spana za gari la baba yake, ambaye kwa sasa ni marehemu.”
Aidha, amesema akiwa kwenye shughuli zake alipigiwa simu na mmoja wa mwanafamilia na kumeeleza kijana huyo amefariki dunia jambo ambalo lilimshtua.
“Nilipigiwa simu kwamba ndugu yetu amejinyonga akiwa mahabusu na kwamba alijinyonga kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu,” amesema.
“Upelelezi wa kifo cha baba yake ndio umeanza maana baba yake amekufa muda sio mrefu, baada ya kuchukuliwa maelezo hapa nyumbani, tulikuwa hatujui chochote kuhusu upelelezi wa kifo cha baba yake, kwa hiyo mpaka sasa hatujui ni nani mhusika wa kifo cha baba yake.
Tumeona kwenye vyombo vya habari kwamba huenda polisi walivyokuwa wanafanya upelelezi wao walifikia huko na sisi ndio tumeshangaa na hata hapa nyumbani ndio tunaulizana imefikaje kwenye hali hii,” amesema baba mdogo huyo wa marehemu.
Kwa upande wake, mama mzazi wa marehemu, Ludovika Mushi amesema taarifa alizopewa ni kwamba mwanaye alikorofishana na baba yake mdogo, ambapo katika ugomvi huo baba huyo alipigwa kwa bapa la panga.
Amesema baada ya tukio hilo, kijana huyo aliwasiliana naye kama mama yake kwa simu, na kumwelezea, ndipo akamshauri amfuate Uru alikokuwa ili wakazungumze.
“Nilihisi bado ni mtoto, hakupaswa kushughulikiwa kwa hasira,” amesema mama huyo.
Mama wa merehemu, Ludovika Mushi, akilia kwa uchungu kufuatilia kifo cha mwanaye anayedaiwa kujiua kwa kujinyonga kituo cha polisi Moshi kati, Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Amesema baada ya hapo alimpigia baba mdogo wa marehemu kumuuliza kilichotokea, lakini hakupata majibu ya kuridhisha ndipo alipompigia mwanaye mkubwa ili kupata uhalisia wa tukio.
Mama huyo amesema wakati wakitafuta mwafaka wa ugomvi huo, Jumatatu alipigiwa simu aende nyumbani Rau ili waweze kuzungumza na kuyamaliza, alipofika, ndipo alikamatwa.
Niliambiwa alikamatwa na polisi, akaachiliwa kwa dhamana akarudi nyumbani, lakini baadaye akapigiwa simu akaambiwa arudi polisi. Jioni ndipo nikaambiwa amefariki kwa kujinyonga,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu mwanae kutoroka amesema marehemu hakuwahi kuondoka nyumbani hapo tangu kifo cha baba, bali aliondoka Alhamisi iliyopita baada ya kukorofishana na baba yake mdogo.
“Baada ya kutokea mvutano na baba yake mdogo ndipo akaja Uru hadi aliporejeshwa nyumbani Rau kusuluhisha mgogoro huo, lakini akakamatwa,” amesema mama huyo.
Marafiki zake katika kazi ya bodaboda wameelezea kushangazwa na tukio hilo wakidai marehemu alikuwa mtu mwenye tabia njema na asiye na historia ya vurugu.
Nuhu Mruma, mpangaji nyumbani kwa marehemu amesema alimfahamu kama kijana mpambanaji na siku zote waliishi naye kwa upendo na furaha.
Imeandikwa na Janeth Joseph, Florah Temba (Moshi) na Bakari Kiango (Dar)