Dar es Salaam. Mradi unaoongozwa na vijana wa uhifadhi wa mazingira ujulikanao kama Guardians of the Peak – SeasonII umezinduliwa rasmi kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya kimataifa ikiwemo China, pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Awamu ya pili ya mradi huo imeweka mkazo mkubwa katika kuhimiza matumizi ya nishati safi kwenye Mlima Kilimanjaro, ili kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa. Kupitia mpango huo, jamii zinazoishi pembezoni mwa mlima huo pia zinatarajiwa kunufaika kwa kuhamasishwa kutumia mbadala endelevu wa nishati.
Chini ya mpango huo, wanafunzi wanatarajiwa kushiriki safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro itakayofanyika kuanzia Januari 20 hadi 31, 2026, ambapo watashiriki shughuli mbalimbali za uhifadhi ikiwemo upandaji miti na uhamasishaji kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Tanzania China Friendship Promotion Association (TCFPA), Joseph Kahama, ametoa wito kwa vyombo vya habari na umma kwa ujumla kushirikiana katika kukuza uhifadhi wa mazingira, urithi wa utamaduni na maendeleo endelevu kupitia mradi wa Guardians of the Peak – Season II.
Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu siyo tu katika kutoa taarifa kuhusu matukio ya kitaifa na kimataifa, bali pia katika kuchochea na kudumisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kahama amesema TCFPA imekuwa mdau muhimu tangu msimu wa kwanza wa mradi huo, akieleza kuwa ni nguzo imara katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka nchi zote mbili pamoja na ubalozi wa China nchini Tanzania.
Amebainisha kuwa malengo makuu ya TCFPA ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kitamaduni kati ya Tanzania na China, kutangaza utalii wa Tanzania hususan Mlima Kilimanjaro katika soko la China na duniani.
Malengo mengine ni kukuza ubadilishanaji wa tamaduni kwa vijana; kulinda taswira ya Tanzania kama nchi yenye amani na utulivu; pamoja na kuvutia uwekezaji wenye tija kwa jamii bila kuathiri mazingira.
Kahama amepongeza pia mkazo wa mradi huo katika matumizi ya nishati safi Mlima Kilimanjaro, akibainisha kuwa utegemezi wa kuni na mkaa umeathiri vibaya misitu, mifumo ya ikolojia na maisha ya jamii zinazozunguka mlima huo.
Amesema matumizi ya nishati safi yanaendana na malengo ya kitaifa na kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku yakiboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), Emmanuel Ndumukwa amesema jukumu la bodi hiyo ni kusimamia, kuendeleza na kutangaza tasnia ya filamu nchini, huku ikihakikisha filamu za Kitanzania zinatumika kama chombo madhubuti cha mawasiliano kwa ajili ya elimu, uhifadhi wa urithi wa kitamaduni na kutangaza diplomasia ya utamaduni kimataifa.
“Mradi huu ni mfano halisi wa namna uhifadhi wa mazingira unavyoweza kuunganishwa na maendeleo ya Taifa, hususan kwa vijana,” amesema. “Unalenga kulinda Mlima Kilimanjaro ambao siyo tu urithi wa Taifa bali pia ni alama ya utambulisho wa Tanzania.”.