Singida Black Stars kutumia mbili Bara kujiweka sawa Afrika

KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesema mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na JKT Tanzania watazitumia kama njia ya kujiweka tayari kwa ajili pambano la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Otoho ya Jamhuri ya Congo Brazzaville.

Mechi hiyo ya CAF inatarajiwa kupigwa Januari 25 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo Singida itakuwa ikisaka ushindi wa kwanza ikiwa Kundi C katika mechi mbili za awali za kundi hilo ilipoteza mbele ya CR Belouizdad ya Algeria kisha kutoka sare ya 1-1 na Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwa sasa imeweka kambi jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mechi za Ligi Kuu inayorejea baada ya kusimama kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea kule Morocco.

SING 01

Kwa mujibu wa ratiba mpya, Singida inatarajiwa kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kesho Ijumaa dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kurudia tena uwanjani Januari 20 dhidi ya maafande wa JKT Tanzania inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 17.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Ouma amesema baada ya kushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026, timu imeendelea kujifua kwa ajili ya michuano iliyo mbele yao na lengo likiwa ni kuona wanakuwa bora zaidi.

“Timu inaendelea vizuri na kwa mujibu wa ratiba tutakuwa na mechi mbili za ligi kabla ya michuano ya kimataifa, hivyo tutazitumia hizo kuhakikisha tunakuwa bora kabla ya kuivaa AS Otoho d’Oyo,”  amesema Ouma na kuongeza;

SING 02

“Ninachofurahia ni kwamba timu ipo kwenye hali nzuri ya utimamu baada ya kutoka kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kukosa baadhi ya wachezaji sasa timu imekamilika na inaendelea na maandalizi.”

Kocha huyo raia wa Kenya, aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyepandishwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo huku akiendelea kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars, amesema anatarajia kupata ushindani wa kutosha kutoka kwa Dodoma Jiji na JKT Tanzania timu hizo ndio zitakazotoa picha ya timu yake itaikabiri vipi AS Otoho ikiwa uwanja wa nyumbani.

“Ligi yetu ni bora na yenye ushindani, ilianza vyema msimu huu nafikiri kutakuwa na muendelezo bora baada ya kurejea tena, sitarajii mechi rahisi hata wachezaji wanatambua hilo hivyo tunafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunakuwa bora na imara tayari kwa ushindani.”

SING 03

Singida iliyotolewa nusu fainali ya Mapinduzi 2026 na Yanga iliyobeba ubingwa juzi usiku kwa kuifunga Azam FC kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu, kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ikiwa na pointi nane kupitia mechi tano.

Katika michuano ya Shirikisho Afrika inashika mkia katika Kundi C ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili ikiambulia sare moja na kupoteza mbele ya CR Belouizdad yenye alama tatu ikiwa ya tatu nyuma ya As Otoho na Stellenbosch zenye pointi nne kila moja kwa sasa.

Singida itacheza na As Otoho mechi mbili mfululizo, kwani baada ya kuwa wenyeji Januari 25 itasafiri kuifuata jijini Brazzaville kuruidiana kabla ya kujiandaa kumalizia mechi mbili za mwisho za kundi dhidi ya Stellenbosch na Belouizdad ili kusaka tiketi ya robo fainali.