MSHAMBULIAJI nyota wa Singida Black Stars, Mzambia Andrew Phiri amekamilisha uhamisho wa kujiunga na Hard Rock FC inayoshiriki Ligi Kuu Zimbabwe, baada ya dili lake kwenda Ureno kufanya majaribio kukwama.
Nyota huyo alikwenda Ureno katika timu ya Clube Desportivo Nacional, baada ya uongozi wa kikosi hicho kuridhia kwa lengo la kwenda kujaribu bahati yake Ulaya, ingawa baada ya kutofanikiwa amepelekwa Hard Rock ya Zimbabwe kwa mkopo.
Phiri aliyejiunga na Singida, Agosti 26, mwaka jana akitokea Maestro United ya Zambia na mkataba alionao na timu hiyo utafikia tamati rasmi Juni 30, 2028, ingawa baada ya ushindani wa nafasi katika kikosi hicho mabosi wameona ni vyema wamtafutie timu nyingine.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti Phiri bado ni mchezaji mzuri anayeweza kukisaidia kikosi hicho, ingawa baada ya majadiliano kati yao na kambi ya nyota huyo wameona ni vyema wamtafutie klabu itakayompa zaidi nafasi.
Phiri aliyezaliwa Mei 21, 2001, alifanya pia majaribio Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini Machi 2025, ambapo nyota huyo alimaliza mfungaji bora wa Maestro United kwa misimu minne mfululizo, huku akiifungia mabao 69, kwenye mashindano yote.
Mwanzoni mwa msimu, nyota huyo alikuwa anahusishwa na timu za Zesco United na Power Dynamos zote za kwao Zambia, baada ya kuonyesha kiwango kizuri kilichoivutia miamba hiyo, huku kwa msimu wa 2023-2024, akichaguliwa mchezaji bora wa msimu.
Pia, mshambuliaji huyo kabla ya kujiunga na Singida msimu huu, alikua akihusishwa na miamba wa soka hapa nchini Yanga, Simba na Azam, kisha Pamba Jiji kuingilia kati dili hilo na kushindwa kumudu fedha zilizohitajiwa na Maestro United na kuibukia kwa Wauza Alizeti hao.
