Wanandoa waweka rekodi ya dunia kwa kuzama kwenye maji ya baridi kali

Wanandoa Chloé Frammery na Steven Kittirath wameingia katika historia baada ya kuweka rekodi ya dunia ya kufanya mahojiano marefu zaidi wakiwa kwenye bafu la maji ya baridi kali, tukio lililovutia hisia za watu wengi duniani na kuonyesha uwezo wa binadamu wa kuvuka mipaka ya hofu na maumivu.

Rekodi hiyo iliwekwa Oktoba 12 mwaka jana katika mji wa Commugny, Uswisi, ambapo Steven, raia wa Ufaransa, alimhoji mke wake Chloé, raia wa Uswisi, kwa muda wa dakika 21 na sekunde 33 wakiwa wamezama kwenye maji ya barafu. Mahojiano hayo yametambuliwa rasmi kama mahojiano marefu zaidi kuwahi kufanyika ndani ya bafu la maji ya baridi kali.

Zaidi ya kuwa rekodi ya Guinness World Records, tukio hilo limeelezwa kuwa safari ya kihisia na kisaikolojia kwa wanandoa hao.

Steven (39) ni mpiga picha wa video, mhadhiri, mwanamichezo na mtafiti wa safari za kipekee, ambaye anaendesha kituo cha YouTube kinachowahoji watu waliovunja rekodi na wenye mafanikio ya kipekee. Safari hii, aliamua kumhoji mtu wa karibu zaidi ambaye ni mke wake.

Chloé (51) ni mtaalamu na mwalimu wa hisabati, mhadhiri na mwandishi, ambaye alitumia fursa hiyo kuzungumzia kitabu chake cha kwanza kiitwacho La Suisse au Coeur (Uswisi Moyoni).

Licha ya kukiri kuwa hapendi baridi na hupata hisia za kuganda haraka, Chloé alisema alikubali changamoto hiyo kama njia ya kujitambua na kujiamini zaidi.

Steven alisema lengo la mahojiano hayo halikuwa tu kuvunja rekodi, bali pia kujaribu nguvu za akili na mwili, huku wakijifunza zaidi kuhusu wao wenyewe na uhusiano wao. Alisema uzoefu huo uliwasaidia kuvuka hofu na mtazamo waliokuwa nao kuhusu baridi kali.

Ili kujiandaa kwa jaribio hilo, wanandoa hao walitumia miezi 10 wakijiandaa kwa kuoga maji ya baridi mara kwa mara, zoezi lililolenga kuzoesha miili yao na kuimarisha uimara wa akili. Kupitia maandalizi hayo, waligundua pia kuwa kukabiliana na baridi kali kunaweza kuwa na manufaa kwa afya ya mwili na akili.

Kwa wanandoa hao, rekodi hiyo ni zaidi ya namba na dakika. Ni ushuhuda wa nguvu ya ushirikiano, mawasiliano na ujasiri wa kukabiliana na changamoto kwa pamoja.

Kupitia tukio hilo, Chloé na Steven wameonyesha kuwa kwa mshikamano na maandalizi, hata mazingira magumu zaidi yanaweza kubadilishwa kuwa fursa ya mafanikio na ukuaji binafsi.