Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesogeza mbele kutoa hukumu katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi inayomkabili, Kulwa Mathias (32) na mwenzake Edina Paul.
Kwa sasa, hukumu hiyo itatolewa Januari 28, 2026.
Hatua hiyo inatokana na Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube anayesikiliza kesi kuwapo kwenye mkutano.
Mathias ambaye ni mkazi wa Shinyanga na Edina mkazi wa Urambo, mkoani Tabora, wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 512.50.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 11, 2024 eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo walikutwa wakisafirisha kiasi hicho, kinyume cha sheria.
Leo Alhamisi Januari 15, 2026 wakili wa Serikali Christopher Olembille, ameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi iliitwa kwa ajili kutolewa hukumu, lakini ya hakimu anayeisikiliza hayupo mahakamani.
Olembille ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Gwantwa Mwankuga.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hili imeitwa kwa ajili ya hukumu lakini hakimu anayesikiliza kesi hii hayupo, hivyo tunaomba mahakama itupangie tarehe fupi kwa ajili ya hukumu,” amesema Olembille.
Hakimu Mwankuga amekubaliana na ombi hilo na kuwaeleza washtakiwa hao kuwa Hakimu Makube anayesikiliza kesi hiyo, yupo kwenye mkutano.
“Washtakiwa, hakimu wenu anayesikiliza kesi hii hayupo hapa mahakamani, bali yupo kwenye mkutano, hivyo kutokana na hali naiahirisha kesi hii hadi Januari 28, 2026 ambapo atatoa hukumu,” amesema hakimu Mwankuga na kisha kuahirisha kesi hiyo.
Itakumbukwa Desemba 24, 2025 washtakiwa hao walikutwa na kesi ya kujibu na kutakiwa kuanza kujitetea Desemba 30, 2025.
Hatua hiyo ilitokana na Mahakama kupitia ushahidi wa mashahidi 12 na vielelezo 11 vilivyotolewa na upande wa mashtaka na hivyo kuwakuta na kesi ya kujibu.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 5, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 5543 ya mwaka 2025.
