Rais Yoweri Museveni amepiga kura katika Kituo cha Shule ya Sekondari iliyoko katika kijiji chake cha asili cha Rwakitura ya Karo nchini Uganda, huku akisema anaunga mkono maelezo ya Tume ya Uchaguzi (EC) kurudi kwenye mfumo wa upigajikura kawaida ili kuepuka usumbufu kwa wananchi.
Museveni amewasili katika Shule ya Sekondari ya Karo, iliyoko katika Kijiji cha Rwakitura, saa 5:25 asubuhi leo Alhamisi Januari 15, 2026 na kusimama kwenye foleni fupi nyuma ya wapigakura watano kisha kukamilisha upigaji kura ndani ya dakika 12.
“Walikuwa na tatizo la mashine za kuthibitisha wapiga kura. Mashine zinafanya kazi. Lakini mwanzoni hazikukubali alama zangu za vidole, kwa sababu nadhani wakati zilipochukuliwa, pembe ilikuwa tofauti lakini uso wangu ulipopigwa picha, mashine ilinithibitisha,” amesema Museveni.
“Baadhi ya watu ndani ya EC hawakutuma taarifa za waendeshaji kwenda kwenye mashine. Wengine, hata hadi asubuhi ya leo, hawakuwa wametuma taarifa zao za kibayometria. Je, hili lilifanyika kwa makusudi? Tutalichunguza,” ameongeza.
Alipoulizwa kama atakubali matokeo ya uchaguzi, Museveni alisema: “Huu ni mojawapo ya udanganyifu tunaopaswa kuchunguza ili kujua tatizo lilikuwa nini? Kwa hiyo, hatujui kama ilikuwa ni uzembe au sehemu ya udanganyifu, lakini tutachambua mambo yote kwa kina.”
Kiongozi huyo mkongwe wa Uganda amesema amekubali pendekezo la dakika za mwisho la EC la kurejea upigaji kura wa kawaida ili kuepusha kuwarudisha wapigakura nyumbani.
“Nilipouliza asubuhi ya leo, niliambiwa kuwa kufikia saa 4 asubuhi mashine zilikuwa zinafanya kazi katika baadhi ya maeneo na maeneo mengine hazifanyi kazi. EC ilipendekeza tupige kura kwa njia ya kawaida, nami nikakubali kwa sababu isingekuwa rahisi wananchi kurudi nyumbani,” amesema.
Amependekeza huenda baadhi ya maofisa walikuwa na hofu kuhusu matumizi ya mashine za kibayometriki, hali iliyosababisha ucheleweshaji na akaonya kuhusu dosari zilizokuwepo katika chaguzi zilizopita ambazo ziliruhusu kura za upinzani kuongezwa kwa njia isiyo halali.
Awali, Mwenyekiti wa EC, Simon Byabakama amevielekeza vituo vya kupigia kura kurejea upigaji kura katika mfumo wa kawaida baada ya kushindikana kufanya kazi mashine za kwa njia ya kibayometriki, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa zaidi ya saa nne, hasa katika Jiji la Kampala, ambayo ni ngome ya upinzani.
