Anayedaiwa kusafirisha bangi, apewa siku tano kupitia nyaraka za ushahidi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Januari 20, 2026 kwa ajili ya Jamhuri kumsomea hoja za awali (PH) mshtakiwa Salma Said (60) anayekabiliwa na shtaka la kusafirisha gramu tatu za dawa za kulevya aina ya bangi.

Hatua hiyo imekuja baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na mshtakiwa kupewa siku tano asome na kupitia nyaraka hizo za Jamhuri, kabla ya kusomewa PH.

Salma anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha gramu 3.8 za bangi, tukio analodaiwa kulitenda Juni 28, 2025 eneo la Mbezi Msigani.

Uamuzi huo umetolewa leo, Januari 15, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi umekamilika na wanaomba wapangiwe tarehe kwa ajili ya kumsomea hoja za awali.

“Mshtakiwa utapewa documents ( nyaraka) zinazohusiana na kesi yako ikiwemo maelezo ya mashahidi wa upande wa Jamhuri, ukazisome vizuri ili ujue ushahidi wa upande wa mashtaka ukoje na wewe utajipanga vipi katika utetezi wako,” amesema Hakimu Mwankuga na kuongeza:

“Hivyo, mshtakiwa kesi yako itaitwa tena hapa mahakamani Januari 20, 2026 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali na utaendelea kuwa nje kwa dhamana,” amesema Mwankuga na kuahirisha kesi hiyo.

Awali, Wakili wa Serikali, Pancrasia Protas aliomba Mahakama impe nafasi ili ampatie mshtakiwa huyo nyaraka hizo ili akazisome na kuzipitia kabla ya kumsomea hoja za awali.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mwankuga na kumpa siku tano mshtakiwa huyo kupitia nyaraka hizo kabla ya kusomewa maelezo yake Januari 20, 2026.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Salma anadaiwa Juni 28, 2025, eneo la Mbezi Msigani, Wilaya ya Ubungo, alikutwa akisafirisha gramu 3.8 za dawa za kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria. Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo alikana kuhusika.

Kwa mara ya kwanza, alifikishwa mahakamani hapo Desemba 15, 2025.