Dodoma. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemfikisha mbele ya Baraza la Maadili Mkuu wa Idara ya Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Alex Manyama kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.
Manyama anayekabiliwa na mashtaka manne tofauti alifikishwa mbele ya baraza hilo jana Jumanne Januari 14, 2026 katika ukumbi wa Ofisi za Sekretarieti ya Maadili jijini Dodoma kujibu tuhuma zinazomkabili ambazo kwa pamoja alizikubali.
Wakili Mkuu wa Serikali, Hassan Mayunga ameliambia Baraza kuwa, Manyama bila sababu za msingi alishindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na 6(1)(c) vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hivyo, kukiuka maadili ya uongozi kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Wakati akikaimu nafasi ya mkurugenzi wa halmashauri ya Mbogwe na akitekeleza majukumu yake alimuhamisha kituo cha kazi mtumishi wa halmashauri hiyo Asifiwe Chipata na kumshusha cheo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu jambo ambalo ni kosa,” amesema Wakili Mayunga.
Wakili Mayunga ameongeza kuwa, “Kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 6(1) (c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinachosomeka pamoja na kanuni ya 3(2)(a) ya kanuni za udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.”
Ameliambia Baraza la Maadili kuwa, mlalamikiwa pia alimuhamisha kituo cha kazi mtumishi mwingine wa halmashauri hiyo, Mercy Kabaka na kumshusha cheo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kinyume na kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinachosomeka pamoja na Kanuni ya 3(2)(a) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.
Kwa mujibu wa Wakili huyo, shtaka lingine ni kumpandisha cheo Mohamed Manawa mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mercy Kabaka aliyemuhamisha na kumshusha cheo.
Amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakati kosa la nne kwa mtumishi huyo ni kumpandisha cheo Edmund Kowi ambaye ni mtumishi wa halmashauri hiyo ili kuziba nafasi ilioachwa wazi na Asifiwe Chipata ambaye naye alihamishwa na kushushwa cheo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji mstaafu Rose Teemba, alimuuliza mlalamikiwa kama amesikia mashtaka dhidi yake na kama anakiri kutenda kosa.
Manyama ameliambia Baraza hilo makosa yaliyosomwa mbele yake ni kweli lakini akaomba Baraza limsamehe kwa kukosa kwake umakini katika utendaji kwenye nafasi aliyopewa.
“Nimesikia mashtaka dhidi yangu na ninakiri kutenda hayo makosa katika kipindi ambacho nilikuwa kiongozi nikikaimu nafasi ya mkurugenzi, kwa kuwa maelezo yote yaliyosemwa na vifungu vya sheria vilivyotamkwa vilifanyika, hivyo sina neno zaidi ya kuomba kusamehewa kwani nilifanya hivyo kwa kukosa umakini,” amesema Manyama.
Jaji Teemba amesema kwa kuwa maelezo yametolewa na mtuhumiwa amekiri kwa kinywa chake, Baraza litafanyia kazi shauri hilo kwani namna lilivyosikilizwa na kufikia mwisho kinachosubiriwa ni uamuzi na mapendekezo.
Baraza la Maadili linaongozwa na Jaji mstaafu Rose Teemba, akisaidiana na wajumbe ambao ni Suzan Mlawi, na Jaji mstaafu John Mgetta, wakati upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Emma Gelani, Hassan Mayunga, Lydia Mwakibete na Catherine Tibasana.
