SMZ yabainisha kuvunja mikataba ya sekta binafsi iwapo…

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema haijasita kuvunja mikataba na sekta binafsi endapo watoa huduma watashindwa kutimiza viwango vilivyokubaliwa, kufuatia kutoridhishwa na ubora wa huduma katika baadhi ya maeneo yanayotekelezwa kwa ubia.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, Januari 15, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa tathmini ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Zanzibar. Amesema Serikali imeingia mikataba mbalimbali ya kushirikiana na sekta binafsi, lakini katika baadhi ya maeneo kiwango cha huduma hakijaridhisha.

Hemed amesema Serikali tayari imewaita wahusika wa miradi hiyo, kusikiliza changamoto zao na kuwapa muda wa kurekebisha kasoro zilizobainika, akisisitiza kuwa endapo hawatatimiza matakwa ya Serikali, mikataba hiyo itasitishwa kwa mujibu wa makubaliano.

Amesema pamoja na changamoto hizo, uwekezaji wa kushirikisha sekta binafsi umeleta mafanikio makubwa, hususan katika sekta ya afya, akitolea mfano huduma za X-ray ambazo awali zilikuwa chache na kuchelewa kutoa majibu, lakini sasa zimeongezeka na wagonjwa hupata majibu siku hiyohiyo.

Wakati huohuo, Serikali imesema jumla ya miradi 110 yenye thamani ya Sh1.8 trilioni imezinduliwa na mingine kuwekewa mawe ya msingi wakati wa maadhimisho ya Mapinduzi, ikiwa ni ishara ya utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi kwa vitendo. Miradi hiyo inahusisha sekta za afya, elimu, maji, barabara, biashara na miundombinu ya usafirishaji, huku Unguja ikiwa na miradi 68 na Pemba 42.

Hemed amesema miradi hiyo inalenga kuimarisha uchumi, kurahisisha biashara na kuboresha maisha ya wananchi, akiongeza kuwa Zanzibar ina mtandao wa barabara wa kilomita 1,344, ambapo kati ya hizo 1,084 zipo kwenye mchakato wa kujengwa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, amesema Serikali itaendelea kuwasimamia watendaji wake kuhakikisha wanashirikiana na vyombo vya habari ili umma upate taarifa sahihi kwa wakati.