Dar es Salaam. Hatua ya kuzima au kuzuia mawasiliano ya intaneti wakati wa uchaguzi, ambayo inaendelea kushamiri katika mataifa mbalimbali barani Afrika na kwingineko, imeibua upinzani mkali kutoka kwa wadau wa siasa, utawala bora na wanaharakati wa haki za binadamu, wakionya kuwa inaathiri kwa kiasi kikubwa misingi ya demokrasia.
Katika karne ya sasa, intaneti imepita matumizi ya anasa au burudani za mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook, Instagram, X na TikTok, na sasa imekuwa miundombinu muhimu inayogusa kila nyanja ya maisha ya binadamu na uendeshaji wa mifumo ya kidemokrasia.
Wadau wanasema mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali ndiyo njia kuu kwa wananchi kupata taarifa kwa wakati, vyama vya siasa kuwasiliana na wafuasi wao, waandishi wa habari kuripoti matukio, na waangalizi wa uchaguzi kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upigaji na uhesabuji wa kura.
Tayari suala hilo limetokea katika nchi za Tanzania, Niger, Zambia, DRC, Gabon, Zimbabwe, Ethiopia, Guinea, Chad, Mali, Sudan na sasa Uganda zimewahi kuripotiwa kuzima intaneti wakati wa uchaguzi au migogoro ya kisiasa, na kusababisha athari mbaya kwa demokrasia.
Wakati Uganda ikifanya uchaguzi mkuu, imeingia siku ya tatu bila mawasiliano ya intaneti tangu ilipozimwa Januari 13, 2026, saa 48 kabla ya upigaji kura.
Serikali imeeleza kuwa hatua hiyo ni kinga dhidi ya vurugu, taarifa potofu na uchochezi kipindi cha uchaguzi.
Hatua hiyo inayoendelea kukithiri na kuonekana ya kawaida kwa kisingizio cha kulinda usalama wakati na baada ya uchaguzi, inatafsiriwa na wadau wa siasa kama njia ya kuzima demokrasia kwa kuwa inakata mnyororo wa uwazi na kuweka mchakato wa uchaguzi katika utata.
Hali kama hiyo ndiyo iliikuta Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 na siku zilizofuata ambapo intaneti ilizimwa na shughuli karibu zote zinazotegemea huduma hiyo zilisimama, lakini Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilifanikiwa kukusanya matokeo ya kuyatangaza kwa wakati.
Kutokana na hilo, leo Alhamisi, Januari 15, 2026, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akifungua mwaka na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, pamoja na mambo mengine, ametoa pole kwa wanadiplomasia hao kwa changamoto ya upatikanaji huduma na kuzimwa kwa intaneti waliyokumbana nayo, wakati na baada ya uchaguzi.
“Kwa washirika wetu jumuiya ya kimataifa na wageni wanaoishi hapa Tanzania, ninatoa pole kwa sintofahamu iliyotokea, kukosekana kwa huduma na kuzimwa kwa mtandao mlikopitia. Ninawahakikishia tumejizatiti kulinda usalama wenu na kuhakikisha hili halitajirudia tena,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema wanatambua kwa moyo mgumu yaliyotokea siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Amesema ilikuwa ni muhimu kuingilia kati ili kulinda amani na usalama kwa mujibu wa Katiba.
Rais Samia amesema demokrasia ni safari ya ukuaji na kila safari ya aina hiyo ina maumivu yake, hivyo ni wazi kwamba hakuna kanuni moja ulimwenguni kwa changamoto hii ya kipekee.
Watetezi wa haki za binadamu, mashirika ya kimataifa na waangalizi wa uchaguzi wamekuwa wakikosoa kitendo hicho, wakisema kinawanyima wananchi haki ya kupata taarifa na kinaathiri mchakato wa uchaguzi.
Akizungumzia kitendo hicho, Mwanahabari mkongwe na mtetezi wa haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema uzimaji wa intaneti wakati na baada ya uchaguzi ni kuzima demokrasia.
“Kwa maoni yangu kuzimwa mtandao ni ishara tosha kuwa uchaguzi unaofanyika si huru wala haki, yeyote atakayeshinda hawezi kuwa ameshinda kihalali, maana mchakato mzima unakuwa umekosa uhalali wa umma,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Nkya, ili uchaguzi uwe huru na haki, lazima ufanyike kwa uhuru, uwazi na matokeo yatangazwe kwa uwazi kama wananchi walivyochagua,
Amesema haki hiyo inapotoweka uchaguzi mzima unakosa uhalali na hivyo mshindi wake anakuwa hajashinda kihalali.
Kuhusu kuzima mitandao kwa kigezo cha kulinda amani, Dk Ananilea anasema hakuna uhusiano kati ya kuzuia mawasiliano ya watu na amani, akihoji ni amani gani inayoharibika watu wakiwasiliana.
Uzoefu kutokana na mataifa yanayozima mitandao wakati na baada ya uchaguzi, unaonyesha hali hiyo huzidisha sintofahamu kwa wadau wa uchaguzi, kwa kuwa wananchi hawawezi kuthibitisha taarifa zinazoenea baada ya mtandao kurejea.
Katika mazingira hayo, tetesi husambaa kwa kasi kupitia njia zisizo rasmi na kuaminiwa kama matukio halisi yaliyoendelea mtandao ulipozimwa, hali ambayo huzidisha hofu na kupunguza imani kwa taasisi za uchaguzi.
Kwa uchaguzi, athari zake ni nzito zaidi. Waangalizi wa ndani hushindwa kupata taarifa sahihi, vyombo vya habari hushindwa kwa uhalisia, na vyama vya siasa hupoteza uwezo wa kusikia wala kusikia kinachoendelea na kuhakikisha kwenendo wa uchaguzi na hivyo kila kitu hutiliwa shaka.
Vilevile, upande wa jamii, madhara huendelea hata baada ya uchaguzi. Biashara za mtandaoni husimama, huduma za kifedha za kidijitali hukatika, na maisha ya kawaida ya wananchi na huduma za matibabu huvurugika.
Hali hiyo, inaelezwa na Dk Azaveli Lwaitama, mwanazuoni mkongwe, akizungumzia uzimwaji wa mitandao kuwa inairudisha Afrika ukoloni katika uendeshaji wake wa chaguzi.
Amesema watu walipinga ukoloni ili wajitawale na wakaweka utaratibu wao kuchaguana kupata wawakilishi wao, lakini kukithiri kwa vitendo vya kuzima intaneti ni tatizo linalolenga kuwadhibiti watu wasiwasiliane kwenye uchaguzi wa kuwapata viongozi wao.
“Hii kuzima mitandao mimi nashangaa kuwa Afrika tunaanza kurudi tena kwenye zama za ukoloni, serikali za kikoloni zilitawala wananchi kinyapala si kuwaongoza, baada ya mkoloni kuondoka viongozi wetu wanaongoza kwa niaba ya Afrika,” amesema, akitilia mkazo kuwa kitendo hicho kinafanya uchaguzi kukosa maana.
“Hii kuogopa uchaguzi mpaka kuzima mitandao inatokana na kuwa watawala wengi wa Afrika ambao si viongozi bali watawala, maana kiongozi yupo kwa ajili ya kuwasaidia watu na kuwaletea maendeleo, lakini mtawala anawatawala watu kwa nguvu, yaani kiongozi anakuwa juu ya wananchi. Hapa kiachotakiwa ni wananchi kujitawala wala si suala la demokrasia tu,” amesema.
Dk Lwaitama ameeleza kuwa kuzima mtandao ni kuharibu kabisa uchaguzi na kuwaambia watu kuwa kinachoendelea ni waliopo kwenye mamlaka kuamua au kupanga matokeo gizani na kuwatangazia wapiga kura.
“Uchaguzi ukichezewa hiki kinachoitwa watu kujitawala hakipo tena, kuzima mawasiliano na kuwapa ugumu mawakala kuwasiliana na vyama vyao huo si uchaguzi wa watu wanaojitawala, hii inaondoa tume kwenye ushawishi kuwa itatangaza kilicho kweli. Kuzima mtandao ni ishara kuwa uamuzi wa wananchi kuchagua wanayemtaka umetoweka,” amesema.
Katika mtazamo mwingine, Dk Conrad Masabo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), amesema kuzima mtandao si tatizo bali lengo la kufanya hivyo ndilo linaweza kuwa baya, kwa kuwa mtandao ni sehemu ya mawasiliano ya jamii ambayo wapo wanaoitumia kwa mema na wapo pia wanaoweza kuitumia vibaya.
Amesema tatizo linaweza kuwa nia ya kuzimwa kwa mtandao huo, ikiwa umeziwa ili kuficha maovu yafanyike.
“Hatupaswi kuipima demokrasia ya Afrika kwa kuangalia kuzimwa mitandao, kwani mnaweza kupewa uhuru wa mitandao yote na bado mkawa hakuna demokrasia.
“Cha msingi ni kuangazia mfumo mzima wa upatikanaji wa viongozi wa Afrika, hata hivyo katika uzoefu, kuzimwa kwa mitandao maeneo mengi kumetokana na kuzuia watu kuwasiliana ili mabaya yafanyike na ndiyo maana ni sahihi watu kusema kuzimwa mtandao kunadhaifisha demokrasia,” amesema.
Amefafanua ikiwa nchi wanazima mtandao ili kuepuka mabaya, hilo siyo tatizo.
