Mziki mpya wa Yanga huu hapa

KATIKA usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa Januari 1, 2026 huku ukitarajiwa kufungwa Januari 30, 2026, unaweza kusema Yanga imemaliza kuboresha kikosi chake kwa kuingiza mashine tano ikigusa idara zote kasoro eneo la kipa tu, huku tukitarajia kuona sura mpya ya upangaji wa timu hiyo.

Mbali na hilo, pia kwa sasa unaweza kupanga vikosi viwili vya kazi vya Yanga na vyote kuonekana imara vikakupa matokeo mazuri. Kwa kifupi unaweza kusema ndani mziki, nje mziki, huku Allan Okello na Laurindo Aurelio ‘Depu’ wakiingia kikosi cha kwanza cha mauaji.

Yanga ilianza kumtambulisha mshambuliaji Emmanuel Mwanengo kutoka TRA United, kisha kiungo mkabaji Mohamed Damaro aliyetokea Singida Black Stars kwa mkopo, akafuatia kiungo mshambuliaji Allan Okello kutoka Vipers ya Uganda.

Pia muda wowote itamtambulisha mshambuliaji Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambaye tayari klabu aliyokuwa akiitumkia ya Radomial Radom kutoka Poland imeshamuaga na kusema amenunuliwa na Yanga.

YANG 01

Nyota wa tano ni uamuzi wa Yanga kumrudisha beki wa kulia, Yao Kouassi baada ya kupona sawasawa goti lake akiwa pia ameshaanza kucheza mechi za kujirudisha katika ubora wake.

Yanga bado inaamini kwenye ubora wa Yao licha ya kukaa nje kwa takribani msimu mzima, sasa atarudishwa kwenye mfumo wa usajili baada ya hapo awali kuondoshwa.

Kuingia kwa mastaa hao wapya, kunakifanya kikosi cha Yanga kwenda kuwa na mabadiliko tofauti na kilivyoanza msimu huu.

Ikumbukwe kuwa, mastaa hao wapya walioongezwa wakiwemo wazawa wawili Damaro aliyebadili uraia kutoka Guinea na kuwa Mtanzania na Mwanengo, pia wa kimataifa Depu, Okello na Yao, unakifanya kikosi hicho kuwa na zaidi ya wachezaji 12 wa kimataifa wanaotakiwa kikanuni, hata hivyo, kuna mpango wa kuwatoa wengine kwa mkopo.

Kabla ya kuwatoa nyota hao, wachezaji wa kimataifa waliopo Yanga sambamba na wale wapya wanafika 14 ambao ni Djigui Diarra, Yao Kouassi, Frank Assinki, Chadrack Boka, Moussa Balla Conte, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Prince Dube, Celestine Ecua, Lassine Kouma, Mohamed Doumbia, Allan Okello na Depu.

YANG 03

Doumbia inaelezwa anaondoshwa, huku Assinki pia ikitajwa anarudishwa kwa waajiri wake Singida, hivyo kufanya idadi ya nyota wa kimataifa ndani ya Yanga kubaki 12. Hapo ni baada ya Andy Boyeli naye kurudishwa Sekhukhune United ya Sauzi iliyomtoa Yanga kwa mkopo.

Sura mpya ya kikosi cha Yanga ina watu wa kazi kila idara ambapo unaweza kutengeneza vikosi viwili vya maana vikacheza na kukupa matokeo mazuri.

Mapema kocha mkuu wa Yanga Pedro Goncalves alinukuliwa kwamba anaamini kikosi kimekamilika kwa sasa kwa wachezaji aliowakuta na wapya wanaoingia na kilichobaki ni kazi tu katika mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA) na Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ipo Kundi B.

YANG 04

Yanga ya Pedro inatarajiwa kucheza mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Jumatatu ijayo dhidi ya Mashujaa kabla ya kuigeukia Ligi ya Mabingwa Afrika ikiifuata Al Ahly ya Misri jijini Cairo katika mechi itakayopigwa Januari 23 kabla ya kurudiana nao Januari 30.

Kwa sasa Yanga iliyotoka kutwaa Kombe la Mapinduzi 2026 kwa kuifunga Azam FC kwa penalti katika fainali iliyopigwa Gombani, kisiwani Pemba inashika nafasi ya pili ikilingana pointi na Al Ahly kila moja ikimiliki nne baada ya mechi mbili na zinatofauti mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga ikifunga bao moja ilipoilaza AS FAR Rabat ya Morocco kabla ya kutoka suluhu ugenini na JS Kabylie ya Algeria inayoburuza mkia wa kundi hilo.

Yanga pia ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 16 kama ilizonazo Pamba Jiji ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa nyuma ya kinara JKT Tanzania inayoongoza ikiwa na pointi 17 ikicheza mechi 10.

YANG 05

Kama kocha Pedro ataamua kuanza na mziki mnene basi ni wazi atayapanga majeshi yake namna hii; Langoni atasimama Djigui Diarra, huku mabeki wa pembeni watakuwa ni Israel Mwenda na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ilihali wake wa kati watakuwa ni; Dickson Job na Ibrahim Bacca.

Viungo atawajaza kina Mohamed Damaro, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Depu, Pacome Zouzoua na Allan Okello.

YANG 06

Aboutwalib Mshery, Yao Kouassi, Chadrack Boka, Aziz Andabwile, Bakari Mwamnyeto, Moussa Balla Conte, Edmund John, Mudathir Yahya, Prince Dube, Lassine Kouma na Celestine Ecua.

Hapo kumbuka kuna vifaa vingine vitakuwa vinasubiri nje akiwamo kipa Abubakar Khomeiny iwapo hatapishana na Yona Amosi kutoka Pamba Jiji anayetajwa kuwa kwenye rada za Yanga, yupo pia Kibwana Shomary, Abubakar Ninju, Abdul Nassir ‘Casemiro’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Farid Mussa, Shekhan Ibrahim, Offen Chikola na Emmanuel Mwanengo.