Dar es Salaam. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kama kisingekuwa na uimara wa kiitikadi na mshikamano wa wanachama wake, kingekuwa kimesambaratika kutokana na misukosuko mikubwa iliyokikumba katika kipindi cha miaka 33 tangu kuanzishwa kwake.
Miongoni mwa majaribu hayo ni vifungo vya chama, viongozi na wanachama, kutekwa, kubambikiwa kesi, kuwekwa vizuizini kwa muda mrefu, pamoja na kuwapoteza mashujaa wengi waliofariki dunia wakiwa katikati ya mapambano ya kudai haki, demokrasia ya kweli na utawala wa sheria.
Akizungumza leo Januari 15, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitangaza ratiba kamili ya maadhimisho ya miaka 33 ya chama hicho yaliyoanza leo na kilele chake kitakuwa Januari 21, 2026, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, Aman Golugwa, amedai chama hicho kimepitia majaribu mazito ambayo chama kingine chochote kingeshindwa kuyavumilia.
“Katika safari ya miaka 33, tumelipa gharama kubwa ya mapambano ya kidemokrasia. Pamoja na risasi, vifungo, vitisho na mikikimikiki yote, Chadema haijafa bali imezidi kuimarika kwa sababu chama hiki ni watu, watu waliobeba ujasiri wa kusema tutashinda,” amedai Golugwa.
Amedai chama hicho kinaamini hakuna hali ya kudumu, na siku ya ushindi itafika licha ya machungu ya kupoteza mashujaa wake wengi, baadhi yao wakifariki dunia wakiwa katika harakati za kudai haki na demokrasia ya kweli nchini.
Katika hotuba yake, Golugwa pia amemtaja Mwenyekiti wa sasa wa Chadema, Tundu Lissu, akisema aliwahi kumiminiwa risasi katika viunga vya nyumba za viongozi wakuu wa nchi, huku akirejea pia matukio ya mauaji ya kutisha yaliyoripotiwa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akielezea ratiba ya maadhimisho hayo, Golugwa amesema Chadema itaendesha shughuli mbalimbali nchi nzima ikiwemo kuwatembelea wananchi walioathirika na matukio ya Oktoba 29, 2025.
“Kuwatembelea wafungwa wa kisiasa magerezani, pamoja na kuwatembelea waasisi wa chama hicho kama ishara ya heshima, shukurani na kujifunza busara za waanzilishi wa harakati za mageuzi nchini.
“Tutatembelea makaburi ya mashujaa na makamanda wetu kuthibitisha kuwa damu iliyomwagika haikumwagika bure, bali ilikuwa wino wa kuandika historia ya mapambano ya kurejesha utawala wa haki,” amesema.
Amesema katika wiki hiyo, chama hicho kitaendesha mabaraza ya kidijitali na mijadala mitandaoni kuhusu mustakabali wa Taifa, hususan masuala ya chaguzi huru na za haki, pamoja na kuandaa michezo, mabonanza, masoko na mashindano mbalimbali ya vijana na wazee.
Kwa upande wa Dar es Salaam, Golugwa amesema Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Jacob Boniface, maarufu Boni Yai atakuwa na jukumu la kuratibu shughuli za michezo zitakazolenga kuimarisha mshikamano na umoja wa jamii.
Golugwa amesema maadhimisho ya miaka 33 ya Chadema si ya kukata keki bali ni tamko la kisiasa na kihistoria linalosisitiza kuwa demokrasia nchini Tanzania haitauzwa, kuzikwa wala kunyamazishwa.
“Wiki hii ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya kudai katiba ya wananchi, tume huru ya uchaguzi, kukomesha vitendo vya utekaji, mauaji ya kisiasa na ukandamizaji wa haki za binadamu,” amedai.
Amesema kupitia maadhimisho hayo, chama kitaweka rekodi wazi za mchango wa viongozi waliowahi kukiongoza, akiwemo Mwenyekiti wa muda mrefu Freeman Mbowe, pamoja na tathimini ya mwaka mmoja wa uongozi wa Mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu.
Golugwa ametoa maagizo kwa viongozi wote wa Chadema kuanzia ngazi ya matawi kuzingatia ratiba ya maadhimisho kama ilivyopangwa, akisisitiza kuwa ni wiki muhimu kwa chama na inapaswa kuheshimiwa.
Pia amevitaka vyombo vya dola kutoingilia au kuchokoza shughuli hizo, akisisitiza kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kwa amani na kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi.
“Tunaviomba vyombo vya usalama viheshimu haki na uhuru wa wanachama wetu wa kufurahi na kujumuika. Shughuli zote zitafanyika kwa amani,” amesema.
