Mwili wa mwanafunzi wakutwa ndani Mbeya

Mbeya. Taharuki na sintofahamu imetanda katika Mtaa wa Igodima jijini Mbeya baada ya mkazi wa eneo hilo anayedaiwa kuwa mwalimu na mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Zainabu Mwalyepelo, kukutwa amefariki dunia nyumbani kwake.

Taharuki hiyo imetokea leo Alhamisi Januari 15, 2026 katika eneo hilo baada ya baba mzazi wa marehemu, Jacob Mwalyepelo kufika nyumbani hapo na uongozi wa serikali ya mtaa huo kubomoa mlango na kukuta mwili kwenye sofa.

Akizungumza huku akitokwa machozi, Mwalyepelo amesema ni maumivu makali kumpoteza mtoto wake ambaye amehangaika naye kwa muda mrefu na gharama kubwa kwa matibabu.

Amesema mwanaye alikuwa mwalimu kitaaluma na alikuwa akijiendeleza kielimu katika Chuo Kikuu cha Catholic Mbeya (CUoM).

“Naumia jamani, bora ningekufa mimi niliyezeeka, nimehangaika sana na mwanangu kuanzia India, Hospitali ya Rufaa Kanda, leo mtoto wangu anakufa, nifanyeje,” amesema.

Akimzungumzia mdogo wake, kaka wa marehemu, Christopher Mwalyepelo amesema mdogo wake hakuwa na mume wala mtoto na alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na wakati mwingine kubanwa na kifua.

Amesema kwa muda ambao alitoka hospitali hakupenda kukaa sehemu ya kelele, hali iliyomfanya kuwa mwenyewe nyumbani kwake katika mtaa huo.

“Alipotoka Hospitali tulimwambia aende kwa dada yake Ivumwe akagoma kwamba anaenda kwake, alikuwa hapendi kelele, baada ya muda tukawa tunapiga simu hapokei, tukawasiliana na Dar es Salaam ambapo huwa anafikia kwa ajili ya kufanya uchunguzi wakadai hajafika.”

Wananchi wakiwa nyumbani kwa marehemu Zainabu Jacob aliyekutwa amekufa nyumbani kwake mtaa wa Igodima jijini Mbeya.

“Baadaye Baba akasema nyumbani kwake milango imefungwa ila taa zinawaka usiku na mchana zinazima, tukashauriana kwenda Polisi wakatuelekeza twende kwa Mwenyekiti wa mtaa tubomoe, tukafanikiwa kuingia ndani tukakuta amefariki,” amesema.

Kwa upande wake, Herman Kanjanja aliyekuwa akiishi karibu na marehemu, amesema Zainab  alikuwa akishinda anaimba na kupiga ngoma, lakini kwa takribani wiki tatu kimya kilitanda nyumbani kwake, hadi kuamua kupiga simu kwa baba yake mzazi kumjuza hilo.

“Nilimwambia baba yake kwamba kwa sasa ni kimya, ameseti taa ikifika saa 1 usiku zinajiwasha na asubuhi zinajizima, ukipiga simu yake inaita tu, ndio leo asubuhi tukafika kufungua ndani tukakuta amefariki,” amesema Kanjanja.

Akithibitisha tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Ayoub Mwazyele amesema tukio hilo ni la kwanza mtaani humo, akieleza kuwa ni masikitiko makubwa kumpoteza mtu huyo na kushauri wananchi kutoishi wapweke.

“Taarifa nimeipokea leo, tulipofungua mlango akakutwa kafariki ndani, nitoe rai kwa wananchi mtu anapoishi nyumbani asiwe peke yake, kiujumla ni masikitiko na hili ni tukio la kwanza mtaani kwangu,” amesema Mwazyele.