Stars, Afrika Kusini wakutana tena WAFCON

TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars imepangwa Kundi B katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026, droo iliyofanyika leo mjini Rabat, Morocco.

Mashindano hayo yanatarajiwa kupigwa Machi 17 hadi April 3 mwaka huu nchini Morocco, huku Stars ikipangwa kundi B pamoja na mabingwa wa mwaka 2022, Afrika Kusini.

Katika kundi hilo gumu, Tanzania pia itakabiliana na Ivory Coast pamoja na Burkina Faso huku mechi zote za Kundi B zikipangwa kuchezwa katika Uwanja wa Al Medina, Rabat.

Hii ni mara ya tatu Stars kucheza WAFCON na mara ya kwanza ni mwaka 2010 ilipoishia hatua ya makundi na 2024 pia katika hatua hiyo ilipomaliza mkiani kwenye kundi C na pointi moja.

Kupangwa kundi hilo Stars kunaiweka kwenye changamoto kubwa, hasa dhidi ya Afrika Kusini ambao ni miongoni mwa timu bora Afrika na yenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa.

TWIG 01

Hii ni mara ya tatu Tanzania kupangwa kundi moja na Banyana Banyana na Oktoba 31, 2010 zilipokutana kwa mara ya kwanza Stars ilitandikwa mabao 2-1 na 2024 zilitoshana kwa sare ya 1-1.

Hata hivyo, ubora wa wachezaji wa Stars hasa wale wanaokipiga ligi mbalimbali duniani, kunalifanya kundi hilo kuwa gumu kutokana na nafasi za kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake 2027.

Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano, timu nne zitakazofuzu hatua ya nusu fainali zitapata tiketi za moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia 2027, huku timu zitakazoishia hatua ya robo fainali zikipewa nafasi ya kuwania tiketi mbili za mchujo.

MAKUNDI
KUNDI A
Morocco
Kenya
Senegal
Algeria

KUNDI B
Afrika Kusini
Burkina Faso
Ivory Coast
Tanzania

KUNDI C
Nigeria
Malawi
Misri
Zambia

KUNDI D
Cape Verde
Mali
Cameroon
Ghana