Chunya yajipanga kuzalisha tani 250,635 za mazao ya chakula, biashara

Mbeya. Zaidi ya hekta 83,450 zimetengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, kwa lengo la kuzalisha jumla ya tani 250,635 za mazao ya chakula na biashara kwa msimu wa kilimo wa 2026/27, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza tija na mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa halmashauri na wakulima kwa ujumla.

Hatua hiyo inaenda sambamba na maandalizi ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo, ikiwemo tani 19,264 za mbolea, lita 34,838 za viuatilifu, kilo 12,250 za viuatilifu vya baisi pamoja na tani 351.71 za mbegu bora za mazao mbalimbali ya kimkakati.

Mkuu wa Sehemu ya Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Paul Lugodisha, ameliambia Mwananchi Digital leo Alhamisi Januari 15, 2026, kuwa mipango hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ikiwemo zao la tumbaku, ambalo ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara wilayani humo.

“Kwa mwaka huu wa kilimo tumejiwekea mikakati kabambe ya kuhakikisha tunafikia malengo tuliyokusudia, hasa ikizingatiwa kuwa sekta ya kilimo inachangia wastani wa asilimia 60 ya mapato ya ndani ya halmashauri,” amesema Lugodisha.

Amesema katika utekelezaji wa sera ya kilimo, halmashauri imewawezesha maofisa ugani kwa kuwapatia vitendea kazi vikiwemo vishkwambi na pikipiki, ili kuwawezesha kuwafikia wakulima kwa urahisi na kuwapatia elimu sahihi ya matumizi bora ya pembejeo za kilimo katika msimu huu.

Lugodisha amesema licha ya wakulima wengi kupanda mazao yao kwa wakati, changamoto ya upungufu wa mvua imejitokeza katika baadhi ya maeneo, hali iliyosababisha mbolea iliyowekwa mashambani kutofanya kazi ipasavyo na kuathiri matarajio ya uzalishaji.

Amefafanua kuwa lengo la kuzalisha tani 250,635 litafikiwa baada ya kufanya makisio kulingana na mwenendo wa kilimo, matumizi ya pembejeo, upatikanaji wa mbegu bora na uzoefu wa misimu iliyopita kwa mazao ya chakula na biashara.

Akizungumza kuhusu upatikanaji wa pembejeo, Lugodisha amesema halmashauri imeweka mikakati maalumu ya kuhakikisha wakulima wanazipata kwa wakati, licha ya changamoto ya baadhi ya mawakala kushindwa kufika maeneo ya pembezoni kutokana na jiografia ya Wilaya ya Chunya.

“Kuna maeneo ambako wakulima hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata pembejeo, jambo linalopelekea wengine kushindwa kuzipata kutokana na ukosefu wa fedha za usafiri, hasa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali,” amesema.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, amesema wameendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya umuhimu wa kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kuzingatia kalenda halisi ya kilimo, pamoja na ratiba za kupanda, kupalilia na kuvuna.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona, amesema kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya kilimo, halmashauri itaendelea kuelekeza nguvu na rasilimali kupitia mapato ya ndani ili kuboresha mazingira ya uzalishaji.

“Asilimia 60 ya mapato ya ndani ya halmashauri yanatokana na sekta ya kilimo, hususan zao la tumbaku. Kutokana na hilo, tumenunua mtambo wa kisasa wa kuchonga barabara ili kuboresha miundombinu ya maeneo ya pembezoni na kurahisisha usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa masoko,” amesema Kambona.

Ameongeza kuwa halmashauri pia imetoa pikipiki kwa maofisa ugani na watendaji wa kata na vijiji, ili wawe karibu zaidi na wakulima, kusikiliza changamoto zao na kutoa elimu ya kilimo bora kwa vitendo.

Kwa upande wa wakulima, Sophia Ndomba, mkulima wa Kijiji cha Mbugani, amesema kwa msimu huu Serikali imejipanga vizuri katika kusaidia wakulima, hususan kwenye upatikanaji wa pembejeo.

“Kwa upande wa Serikali mambo yako sawa kabisa, changamoto kubwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaweza kuathiri uzalishaji. Tunaomba wataalamu wa kilimo wafike mara kwa mara ili kutupa elimu zaidi,” amesema Ndomba.