Maswa. Wanafunzi wasio na sare mkoani Simiyu hawapaswi kuzuiwa kuhudhuria masomo hasa wale wa darasa la kwanza kwa shule za msingi na kidato cha kwanza kwa shule za sekondari, kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha wakati wa ziara yake wilayani Maswa kukagua mahudhurio ya wanafunzi katika shule ya msingi Shanwa na shule za sekondari za Zanzui,Binza na Nyalikungu zilizopo wilayani humo.
Katika ziara hiyo Macha amebaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza hawajaripoti shuleni tangu kufunguliwa kwa muhula wa masomo Januari 13,2025 huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kukosa sare za shule.
Amesema kuwa kukosa sare hakupaswi kuwa kikwazo cha mtoto kupata elimu, akiwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule mara moja hata kama bado hawajakamilisha mahitaji hayo.
“Wanafunzi wote wanaopaswa kuanza darasa la kwanza na wale wa kidato cha kwanza ambao hawana sare na hata mahitaji mengine ya shule wanapaswa kuwepo madarasani na kuanza masomo huku wazazi na walezi wakiendelea kukamilisha mahitaji yao,”amesema.
Macha ametangaza kuwa kuanzia januari 19,2025, mkoa huo utaanza msako wa nyumba kwa nyumba kuwasaka wanafunzi wote ambao hawajaripoti shuleni, hatua hiyo inalenga kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyumbani bila sababu za msingi.
Katika Shule ya sekondari Zanzui Macha aliguswa na hali ya mwanafunzi Mary Charles, anayesoma kidato cha kwanza ambaye aliendelea kuhudhuria masomo bila sare ya shule kutokana na moyo huo wa bidii aliahidi kumnunulia mwanafunzi huyo sare za shule pamoja na madaftari kama motisha ya kuendelea na masomo.
Akizungumzia hali hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney amesema kuwa serikali haitamvumilia mzazi au mlezi anayemzuia mtoto kwenda shule kwa makusudi.
“Hakuna mzazi atakayekuwa na sababu ya kumzuia mtoto kwenda shule kwa kisingizio cha sare. Mtoto anatakiwa awe darasani kwanza, sare zitafuata. Elimu ni haki ya msingi ya mtoto,” amesema.
Juma Shija ni mkazi wa kijiji cha Zanzui amesema kuwa hatua hiyo itasaidia watoto wengi waliokuwa wakibaki nyumbani.
“Wazazi wengi walikuwa wanaona aibu kuwapeleka watoto shule bila sare, sasa kauli hii imetupa mwanga. Mtoto bora asome kuliko akae nyumbani,” amesema.
Kwa upande wake, Esther John ni mzazi wa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Nyalikungu iliyopo wilayani humo amesema kuwa uamuzi huo ni mzuri na utatoa nafasi kwa watoto kupata elimu.
“Huu ni uamuzi mzuri sana. Hali ya maisha ni ngumu, lakini mtoto hapaswi kuathirika. Tumeanza tayari kuwapeleka watoto wetu shule,” amesema.
Naye Paulo Ng’wala ambaye ni mkazi wa Maswa mjini, aliipongeza serikali kwa kuchukua hatua za ufuatiliaji
“Msako wa nyumba kwa nyumba utawafanya wazazi wazembe wawajibike. Elimu ndiyo urithi pekee wa mtoto maskini,” amesema.