Mashujaa yaifuata Yanga kwa akili mpya

KIKOSI cha Mashujaa FC tayari kimeshatua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya watetezi ikiwa na akili nyingine kabisa na kocha wa timu hiyo Salum Mayanga akiweka wazi wamekuja mjini kutibua rekodi ya wababe hao waliotwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026 bila kupoteza visiwani Zanzibar.

Mashujaa itakuwa wageni wa Yanga katika mechi hiyo itakayopigwa Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam na tayari imeshawasili jijini humo tangu jana baada ya kutumia siku moja kutoka Kigoma na kocha Mayanga alitamba wamekuja kupiga kazi.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Mayanga amesema anatambua wanakutana na timu bora iliyotoka kutwaa taji la Mapinduzi bila kupoteza, lakini wakiwa ni watetezi wa Ligi Kuu, ila hilo haliwapi shida kwani na wao wapo timamu na bora kwa ushindani.

MASHU 01

“Mara zote tunapokutana na Yanga mechi inakuwa ngumu na yenye ushindani rekodi yao itavunjwa Bara tena kwenye uwanja wao wa nyumbani, wachezaji wangu wapo tayari kwa ushindani kutokana na maandalizi tuliyafanya,” amesema Mayanga nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar aliyeongeza;

“Tumepata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki baada ya maandalizi ya muda mrefu yaliyokuwa yanaendelea kutokana na mapumziko ya kupisha michuano ya AFCON 2025 na ile ya Mapinduzi 2026. Sasa tumerudi katika mechi za ushindani tulianza na kiporo hicho na Yanga.”

Mayanga amesema wanaiheshimu Yanga kutokana na ubora iliyonayo ikiundwa na nyota wengi bora wazoefu, lakini hata wao (Mashujaa) wamefanya maandalizi ya kutosha kukabiliana na ushindani huo.

“Tutaingia kwa kumheshimu mpinzani, huku tulicheza kwa tahadhari ili kuweza kufikia malengo ya kupata pointi tatu ugenini haya ndio malengo yetu bila mipango na mbinu sahihi hatuwezi kutoboa,” amesema Mayanga aliyewahi kuzinoa timu mbalimbali ikiwamo Taifa Stars.

MASHU 02

“Naamini wachezaji wangu wanatambua umuhimu wa mchezo huo Ligi bora na ngumu imerudi sasa ni kuwekeza nguvu na juhudi mchezo hadi mchezo ili tuweze kufikia malengo tuliyojipangia kuanzia mwanzo wa msimu,” aliongeza Mayanga.

Hadi Ligi imesimama Desemba 7 mwaka jana, Mashujaa ilikuwa imecheza mechi tisa ikishika nafasi ya nne kwa kukusanya pointi 13 nyuma ya Pamba Jiji yenye pointi 16 kama Yanga ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa nyuma ya kinara, JKT Tanzania yenye pointi 17.