Undeshaji wa taasizi za Wakfu na mchango wake katika huduma za kijamii

Katika maeneo mbalimbali duniani, nchi zinaendelea kubuni na kutumia mbinu mpya za kufadhili maendeleo ya kijamii ili kupanua upatikanaji wa huduma bora. Mojawapo ya mbinu hizo, inayotumika kwa ufanisi nchini Uturuki ni mashirika ya wakfu (vakıf).

Mashirika haya yamewekeza kwa kiwango kikubwa katika kwenye huduma jamii, mfano kwenye sekta ya elimu nchini humo, kupitia ufadhili wa wanafunzi, ujenzi na uendeshaji wa shule, vyuo vikuu, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, na miundombinu mingine.

Wakfu ni neno la Kiarabu linalomaanisha mali iliyotolewa kwa ajili ya manufaa ya umma. Kwa mujibu wa Dk Monzer Kahf, kwenye chapisho lake Financing the Development of Awqaf Property (1998), waqf ni mali inayowekwa katika umiliki wa mwingine, mara nyingi chini ya taasisi maalumu kwa sharti la kuendelezwa, na kwamba manufaa au mapato yake yatumiwe kwa malengo mema ya kijamii.

Kwa kutambua hilo, nchini Uturuki mashirika hayo yanafanya kazi ndani ya mfumo rasmi wa kisheria chini ya Sheria ya Wakfu ya nchi hiyo, chini ya kurugenzi ya usimamizi mifuko ya Wakfu katika Wizara ya Utamaduni (Vakıflar Genel Müdürlüğü). Kisheria, ni taasisi binafsi, lakini zimewekewa majukumu ya wazi ya kuhudumia umma na zinakaguliwa kifedha kwa ukaribu.

Tofauti na asasi za kiraia au mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotegemea michango ya wafadhili, msingi wa wakfu ambao ni mali (asset), iliyotolewa kama amana ya kudumu, kama vile ardhi, majengo, ni lazima iwe endelevu, kuzalisha mapato. Mapato hayo ndio hutumika kufadhili shughuli za kijamii, bila kuathiri mali ya msingi.

Uendeshaji wa mashirika ya wakfu hufanywa kupitia bodi ya wadhamini au menejimenti, kulingana na hati ya kuanzishwa kwake. Si kampuni za kibiashara, lakini huajiri wataalamu katika maeneo kama usimamizi wa majengo, biashara na uchambuzi, na hutumia mbinu za kisasa za kitaasisi katika kuendesha shughuli zao, yote ikiwa ndani ya lengo la kuhudumia maslahi ya umma.

Jambo hili linatupa msisitizo kwamba mifuko hii binafsi, ingawa asili yake ni ya kidini kupitia dhana ya Kiislamu ya kujitolea mali (Waqf), lakini kwao imebeba mtazamo mpya, na kuwa haipaswi kuonekana kama hisani au sadaka tu, ni mashirika makubwa.

Badala yake, yanatumika kimkakati kama nyenzo ya fedha ya kijamii (social finance instrument), serikali pia, inaweza kuyapa mashirika haya jukumu rasmi la kuchangia maendeleo kulingana na dira ya taifa katika sekta muhimu za kijamii, kupitia mipango na makubaliano maalum.

kwa sababu ya usimamizi mzuri na ufuatiliaji, mashirika ya wakfu yamechangia kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika sekta ya elimu nchini Uturuki, mfano elimu ya juu. mashirika haya yanaendesha na kumiliki zaidi ya vyuo vikuu 75 sambamba na vile vya serikali. Vyuo vikuu mashuhuri kama Istanbul medipol, Istanbul aydin, Abdullah gül üniversitesi, vinamilikiwa na kuendeshwa na mashirika ya wakfu.

Vilevile, mashirika ya wakfu yamewekeza sana katika ujenzi na uendeshaji wa mabweni na makazi ya wanafunzi. Taasisi kama TUGVA Mimar Sinan, ÖNDER İmam Hatip, zinaendesha mtandao wa mamia ya mabweni ya wanafunzi yanayotoa makazi kwa gharama nafuu kwenye mikoa mbalimbali, hali inayosaidia serikali hasa ikizingatiwa pia kuna idadi kubwa ya wanafunzi wa kimataifa.

Katika ufadhili wa masomo, mashirika kama TÜRGEV yamechangia kwa kiwango kikubwa kusaidia watoto na vijana walio katika mazingira magumu kwenye jamii ya Kituruki. Inakadiriwa kuwa taasisi hii imefadhili takribani wanafunzi 320,000 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969.

Kwa ujumla, uzoefu huu unaonesha kwamba ubunifu na usimamizi mzuri wa mifumo mbadala ya fedha kijamii unaweza kuchangia vizuri katika maendeleo, huku jamii nzima ikinufaika.