Katika makala iliyopita iliangazia namna Uislamu ulivyoipa ndoa uangalizi mkubwa na umakini wa hali ya juu, kwa kutambua kwamba uadilifu wa ndoa humaanisha uadilifu wa jamii ya Kiislamu.
Makala hii, ni mwendelelzo wa makala iliyopita..sasa endelea..
Uamuzi wa kuchagua mke ni miongoni mwa uamuzi muhimu zaidi katika maisha ya mwanadamu.
Kwa hiyo, mtu anatakiwa kuswali swala ya kumtaka ushauri Allah (istikhara) na ajiepushe na kuendeshwa na matamanio au mapenzi ya ghafla, azingatie vigezo vya msingi na vilivyo wazi, na vigrzo hivyo:
Mosi. Dini, ni miongoni mwa vigezo muhimu zaidi vinavyopaswa kuzingatiwa katika uchaguzi wa mke. Mwanamke mwenye dini na uchamungu hujitahidi kuishi na mume wake kwa wema, hutekeleza haki zake, hufanya wajibu wake ipasavyo, na hutii katika mambo mema yasiyopingana na amri za Allah Mtukufu.
Vilevile, mwanamke wa aina hii huweka juhudi kubwa katika malezi sahihi ya watoto, akijenga tabia na misingi yao kwa maelekezo mema na kwa kuwa mfano bora kupitia mwenendo na sifa zake njema.
Mtume wa Allah amesema: “Mwanamke huolewa kwa sababu nne: Kwa mali yake, kwa nasaba yake, kwa uzuri wake, na kwa dini yake. Basi tafuta mwenye dini, upate kheri na Baraka,” (Bukhari).
Kadhalika Mtume wa Allah amesema: “Dunia ni starehe, na starehe iliyo bora zaidi duniani ni mwanamke mwema.” (Muslim).
Pili: Uzuri, Uislamu unautambua uzuri kuwa ni miongoni mwa mambo yanayohamasisha kuoa mwanamke. Abu Huraira (Allah Amridhie) alimuuliza Mtume wa Allah, ni wanawake gani walio bora zaidi? Akamjibu:
“Mbora wa wanawake ni yule ambaye ukimtazama hukufurahisha, ukimuamuru hukutii, na unapokuwa mbali naye hulinda mali yako na (kuhufadhi) nafsi yake (hishima).”(Addailamiy). Hadithi imegusia uzuri wa mwanamke sambamba na sifa nyingine muhimu kama dini, maadili mema na kujisitiri.
Aidha, Mtume wa Allah ametoa onyo dhidi ya kuoa kwa kuzingatia uzuri pekee au mali pekee, aliposema: “Msiwaoe wanawake kwa ajili ya uzuri wao, huenda uzuri wao ukawaangamiza; wala msiwaoe kwa ajili ya mali zao, huenda mali zao zikawapotosha. Bali waoeni kwa ajili ya dini.”(Ibn Maja).
Tatu: Nasaba na asili ya kifamilia zina nafasi kubwa katika jamii nyingi, mara nyingi kijana hutamani kumuoa mwanamke anayelingana naye katika nasaba. Huenda akamuoa mwanamke wa chini yake kinasaba, na jamii ikavumilia hali hiyo.
Lakini hali huwa ngumu zaidi pale kijana anapooa mwanamke aliye juu yake kinasaba.Kwa mujibu wa mtazamo wa Kisharia wa Kiislamu, anayekusudia kuoa achague mwanamke kutoka katika familia njema, yenye sifa ya adabu, heshima na maadili mema, pamoja na mshikamano wa kifamilia.
Nne: Mali (kazi au kipato cha mwanamke), hadi kipindi cha hivi karibuni, jamii ya Watanzania haikuwa ikiangalia mali ya mwanamke kama kigezo muhimu katika uchaguzi wa mke, kutokana na kutokuwepo kwa tofauti kubwa za kiuchumi miongoni mwa watu.
Hata hivyo, baada ya hali ya kiuchumi kuwa ngumu ikilinganishwa na ilivyokuwa awali, vijana wameanza kuzingatia zaidi suala la kazi ya mwanamke.Aidha, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wasio na ajira, imekuwa ni jambo la msingi kwa kijana na familia yake kutafuta mke mwenye kazi au kipato. Hali hiyo imeanza kuathiri uamuzi wa wasichana wanaochumbiwa na familia zao, na imekuwa kikwazo kikubwa kwa ndoa nyingi.
Tano: Uelewa na ufahamu (ukomavu wa fikra).Uelewa hapa unamaanisha kuchagua mke mwenye ufahamu mpana, atakayemsaidia mume katika safari ya maisha. Mwanamke mwenye uelewa ni yule anayefahamu misingi ya uendeshaji wa nyumba, hali ya kiuchumi ya familia, malezi ya watoto, namna ya kumtunza na kumheshimu mume.
Sita. Usafi katika Uislamu ni sehemu ya dini na umepewa uzito mkubwa kupitia msisitizo wa twahara katika aina mbalimbali za ibada.
Mtu mwenye akili timamu hupenda usafi na huchukia uchafu.
Miongoni mwa mambo yanayomkera sana mume ni kuikuta nyumba ikiwa si safi, kuandaliwa chakula kisicho na dalili za usafi, au kuhisi harufu isiyopendeza kutoka kwa mke au watoto. Mwanamke msafi humpa mume na watoto wake utulivu wa kisaikolojia na faraja ya maisha ya kifamilia.
Mwanamke kumchagua mume wa kumuoa ni moja ya haki zake za msingi, ambayo mara nyingi imefichwa na mila na desturi za kijamii. Mwanamke atachagua mume wa kumuoa kwa sifa zilizoelezwa kwa mwanamke na kuongezea sifa ya uwezo wa mume kumuhudumia mkewe na familia kwa jumla.
Uislamu unasisitiza umuhimu wa ridhaa ya mwanamke katika ndoa na kuifanya kuwa miongoni mwa sharti ya kusihi ndoa. Ushahidi wa hilo ni hadithi inayobainisha kuwa msichana mmoja alimjia Mtume na kumuuliza: “Hakika baba yangu alinifungisha ndoa na mtoto wa ndugu yake ili ainue hadhi yake.”
Mtume akampa msichana huyo haki ya kuamua. Msichana huyo akasema: “Nimeridhia alichokifanya baba yangu, lakini nilitaka wanawake wajue kuwa baba hana mamlaka ya lazima katika jambo hili.”
