ULIAMUANGALIA kiungo wa Yanga Moussa Balla Conte katika mechi za michuano ya Kombe la Mapiduzi 2026? Basi jamaa kuna upepo ameubadili ndani ya klabu hiyo akizalisha kambi mbili zinazobishana akatwe ama apewe muda.
Katika mechi hizo za Mapinduzi, zilizoisha kwa Yanga kubeba ubingwa kwa penalti 5-4 dhidi ya Azam FC, kocha Pedro Goncalves kuna matumizi ya aina mbili ambayo aliyafanya kwa Conte kwanza alimchezesha kama beki wa kati na jamaa akazima vizuri.
Jaribio la pili likawa kuchezeshwa katika nafasi yake kama kiungo mkabaji tena mechi ya Fainali dhidi ya Azam na jamaa akafanya vizuri, Yanga ikachukua ubingwa wa tatu wa michuano hiyo tangu mwaka 2007 ikibeba awali mwaka huo wa 2007 na 2021.
Baada ya kiwango hicho, kumeibuka mvutano ndani ya Yanga juu ya hatua za kumtoa kwa mkopo kiungo huyo ambapo baadhi ya mabosi wa timu hiyo wameingia mtego wa mashabiki wakitaka Conte apewe muda.
“Baada ya mechi ya fainali kuna wenzetu wanaona kama maamuzi ya kumtoa kwa mkopo tumeyachukua kwa haraka na kutaka tumpe muda labda ndio ameanza kujipata,” amesema bosi mmoja wa juu wa Yanga.
Hata hivyo, mtazamo huo unaopingana na kundi la pili ambalo limesimamia msimamo wa kwamba kuanzia kiwango hicho cha Conte kupitia mechi hizo akakiendeleze kwenye timu ambayo wanataka kumpeleka kwa mkopo.
“Hili kundi lingine sasa lenyewe halitaki kupoteza muda wao wanataka hatua za kumtoa kwa mkopo ziendelee hasa kutokana na kiwango cha Damaro (Mohammed) na hawa wengine kina Duke (Abuya) na Mudathir (Yahya) amepona, wanaona ni bora akaendeleze kiwango hicho huku kisha tathimini yake ya kina ifanyikwe mwisho wa msimu.
“Unajua Conte bado ana mkataba mrefu ndio kwanza amemaliza miezi sita ya kwanza akimaliza msimu huu atabakiza miaka miwili, katika mkataba wake wanaona muda wa kumpima kiwango chake bado upo.
“Bado hatujajua kipi kitaamuliwa kuna kikao kitafanyika kwa kocha na uongozi na hapo ndio tutajua maamuzi ya kocha kwamba ameona nini kiufundi.”
Yanga imeshamsajili Damaro kutoka Singida Black Stars ambapo kiwango chake kimeonyesha kuwakosha mabosi wa Yanga na makocha wa timu hiyo na ilipangwa Conte sambamba na Mohammed Doumbia watolewe kwa mkopo wakati Andy Boyeli akirudishwa Sekhukhune United ya ASfrika Kusini iliyowapa Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja na kutumika kwa miezi sita.
Hesabu za Yanga ni kupunguza idadi ya nyota wa kigeni kwani kanuni zinahitaji wachezaji 12 wakati tayari imeshazidisha ikiwa na 13 baada ya ingizo la Allan Okello, Depu na kurejea kwa Yao Kouassi aliyekuwa majeruhi anayeungana na kina Diarra Djigui, Chadrack Boka na Frank Assinki.
Pia kuna Prince Dube, Pacome Zouazoua, Maxi Nzengeli, Dube Abuya, Celestine Ecua, Lassine Kouma na yeye Conte aliyewagawa mabosi kuamua nani wa kumchomoa, japo inadaiwa kama vita yake ya kubakishwa itatiki basi mtu wa kuondolewa itakuwa ni Assinki atakayerudi Singida BS.
