Mandawa anaposahau kumbakishia Mstaafu | Mwananchi

Siku chache zilizopita Mstaafu wetu ambaye hupenda kujinasibu kuwa macho yake yameshaona kila kitu hata yale yasichopaswa kuona. Amesoma habari kwenye mitandao yetu ya kijamii ambayo imemfanya akiri kuwa mimacho yake ya kizee hakika bado haijaona kitu kabisa!

Labda inawezekana kuwa macho yake yameishazeeka au pensheni yake ya laki moja elfu hamsini kwa mwezi haijamwezesha kufanya kile wanachofanya wenye pesa zao au wale wanaofika daraja fulani la juu kimaisha, ambao ghafla macho yao yanakuwa mabovu yanayohitaji miwani.

Pamoja na macho yake kuwa na miaka 67, kama alivyo mwenyewe, ana hakika kuwa bado yataendelea kuona kila kitu, hata kile asichopaswa kuona, na hayatakuwa mabovu kamwe hata akalazimika kuvaa mawani, ambayo sasa imekuwa fasheni tu, tofauti na miaka ile ya 47.

Ndiyo. Miaka ile ambapo mawani ya macho ilikuwa inavaliwa na wasomi wachache tu na wabovu wa macho wa kweli waliokuwa wachache zaidi. Watu walikuwa kweli wanakula karoti bwana!

Haya, Mstaafu akasoma kwenye mitandao na kumsoma mheshimiwa mmoja akimsifu mheshimiwa mwingine anayeongoza waheshimiwa na wasio waheshimiwa lakini waajiri wake, kuwa mheshimiwa mkubwa huyo anawapenda sana Watanzania na ana huruma sana na Watanzania na anawasaidia sana kwenye maisha yao!

Mstaafu wetu anakiri kwamba pamoja na kuwa kweli, habari hii ilinishitua sana kiasi cha kunikumbusha hadithi moja mashuhuri niliyopata kuisoma enzi zile shule zilipokuwa shule kweli na sio hizi za sasa ambazo kama fedha hazijajenga kibanda cha kudumu mifukoni, basi ‘kayumba’ itawahusu vijana wako. Pole!

Hadithi ile nadhani iliitwa ‘Manenge na Mandawa’ ambapo mume alikuwa ameoa mke anayependa sana ‘kufukia’ kiasi cha kumsahau hata mumewe Manenge aliyekuwa mtafutaji wa chakula, huku Mandawa akibaki kuliambia tumbo lake limkumbushe kumwekea chakula mumewe!

Mstaafu amejikuta akitafakari sana aliposikia mheshimiwa yule akimjazia maujiko mheshimiwa mwenzake wa waheshimiwa wengine wote kwa huruma zake na kuwajali kwake Watanzania, japo tumemwajiri kwa kazi hiyo. 

Mstaafu wetu hapingi sifa anazorundikiwa mheshimiwa mkuu. Tatizo lake anajikuta akikumbuka mno ya Manenge na Mandawa’!

Anajiona mstaafu akiwa Manenge tu huku mwezake Mandawa akifanya vitu vyake vya ‘kufukia’ msosi na kuliachia tumbo limkumbuke Manenge ili awekewe msosi. Hii ni pamoja na kuwapeleka wasanii wetu ndege nzima hadi Korea ili kupata uzoefu, japo baada ya mwaka mmoja kuwapeleka huko hatujaona wasanii wetu walichojifunza. Bonge la msosi lakini Mstaafu hajui umetusaidiaje wastaafu.

Tumeshuhudia pia mheshimiwa akiwapenda zaidi vijana wetu wacheza mpira kiasi cha kukubali wapewe Shilingi milioni…mama wee! mia mbili kwa kila goli watakalofunga ndani ya dakika 90 za mchezo.  Hii ina maana siku timu yetu ya taifa ikiweza kufunga magoli matano kwenye michuano fulani Shilingi…mama wee! bilioni moja itakuwa imeyeyuka kutoka tozo za Watanzania. Dakika 90 bilioni moja?

Ni bahati mbaya sana kwamba huruma na kujali kwa mheshimiwa kwa Watanzania kunaishia kwa wasanii na wacheza kandanda na haijafika kwa Mstaafu wa kima cha chini, ambaye baada ya kuijenga, kuipigania na kuilinda nchi kwa miaka 40 aliishia kulipwa kiinua mgongo cha Sh30 milioni tu.  

Wasaidizi wako wanaotaka wachezaji wa timu ya taifa walipwe Sh200 milioni kwa goli wanakwambiaga hili linalofanana na la Manenge na Mandawa?

Mstaafu huyu sasa analipwa pensheni ya shilingi laki moja alfu hamsini kwa mwezi kwa miaka 21 sasa! Hivi hata hesabu imekaa vizuri hapo? Miaka 40 ya kujenga Taifa kwa jasho na damu’ uishie kulipwa Sh39 milioni tu na pensheni ya shilingi laki moja elfu hamsini kwa mwezi!

Huku kijana akilipwa milioni 200 kwa goli moja katika dakika 90! Wastaafu wanawataka wanaohusika waweke hesabu zao vizuri. Tusifanye wastaafu waombe vijana wetu wasifunge goli ili mamilioni yanayochezewa yabaki kwenye kibubu che Siri-kali na baadaye isiyo mbali sana yawafae wastaafu walioijenga na kuipigania nchi hii.

Tujiulize kidogo, ni kwa nini magoli yamenyauka kama Jangwa la Kalahari kwenye timu yetu ya Taifa? Tuwape wastaafu wetu pensheni inayomstahili ya shilingi laki tano kwa mwezi (linawezekana, ni utashi wa watu tu!) halafu muone magoli yatakavyomiminika kwenye nyavu za wapizani, kila goli Sh1 milioni! 

  0745 340606 / 0784 340606