Watoto wenye magonjwa ya moyo wakumbukwa

Dar es Salaam. Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imejitosa kusaidia mpango wa kitaifa unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu na rufaa za mapema kwa watoto wenye magonjwa ya moyo hapa nchini.

Mpango huo unatekelezwa na GGML,  kampuni tangu ya AngloGold Ashanti Afrika, kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya, ukiwa na lengo la kuimarisha utambuzi wa mapema kwa watoto wenye magonjwa ya moyo, mifumo ya rufaa, na upatikanaji wa msaada wa kifedha.

Akizungumza wakati wa ziara ya hivi karibuni katika taasisi ya JKCI iliyolenga kuimarisha ushirikiano huo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti Afrika anayesimamia masuala ya uendelevu na uhusiano, Simon Shayo, amesema msaada wa kampuni hiyo unaakisi dhamira ya muda mrefu ya kampuni hiyo katika kuboresha matokeo ya afya ya jamii, hususan kwa watoto wenye uhitaji maalum.

Kwa mujibu wa taarifa za JKCI, taasisi hiyo hupokea wastani wa rufaa 50 za watoto kila mwezi, huku kitengo cha watoto chenye vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) na huduma za uangalizi maalumu (HDU) kikiwa na uwezo wa vitanda 26 pekee.

Kwa sasa, takribani watoto 1,500 wapo kwenye orodha ya kusubiri kupata matibabu kamili ya moyo yanayogharamiwa na Serikali, huku mamia zaidi wakiongezeka kila mwaka.

Ingawa Serikali hugharamia takribani asilimia 70 ya gharama za matibabu, asilimia 30 iliyobaki, sawa na wastani wa Sh4 milioni kwa kila mtoto, imekuwa kikwazo kikubwa kwa familia nyingi.a

Shayo amesema katika mwaka 2025 pekee, GGML ilitoa Sh56 milioni, zilizowezesha upasuaji na matibabu hayo kwa watoto 14, na mafanikio ya matibabu hayo yalifikia asilimia 95 ya kuokoa uhai wao.

“Upatikanaji wa huduma bora za afya, hususan kwa watoto wenye matatizo makubwa ya moyo, si suala la kitabibu pekee bali ni jukumu la kijamii. Ndani ya GGML, tunaamini ushirikiano wa aina hii ni muhimu katika kuokoa maisha na kuimarisha sekta ya afya nchini,” amesema Shayo.

Amesema uhitaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto nchini yanaendelea kuongezeka, hali iliyoisukuma GGML kutoa msaada wa kifedha kuunga mkono jitihada za Serikali na wadau wengine.

“Tangu Novemba 2024, GGML imejikita katika kuziba pengo hili la kifedha ili kuhakikisha watoto kutoka familia zenye uhitaji hawakosi matibabu kutokana na changamoto za kifedha,” amesema Shayo.

Kupitia ufadhili, jumla ya watoto 200 wenye uhitaji wa matibabu ya moyo wamefikiwa hadi sasa. Hata hivyo, mahitaji yanaendelea kuongezeka, ambapo watoto 400 zaidi wapo kwenye orodha ya kusubiri huduma, jambo linaloonesha umuhimu wa msaada kuendelea kutolewa.

Ili kuhakikisha uendelevu wa mpango huo, Shayo amesema GGML itaendelea kutoa msaada wa kifedha pamoja na kuwekeza katika tafiti na maeneo mengine yanayolenga kuboresha matokeo ya huduma za matibabu ya moyo kwa watoto nchini.

“Lengo letu ni kuchangia katika uokoaji wa maisha kwa haraka pamoja na maboresho ya mifumo ya muda mrefu, ili watoto wengi zaidi wapate matibabu kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi,” amesema.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dk Angela Muhozya, mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Moyo JKCI, ameishukuru GGML kwa kuendelea kutoa msaada na kutoa wito kwa wadau wengine kujiunga katika jitihada hizo. Ameeleza pia pamoja na mambo mengine, changamoto wanazokabiliana nazo walezi wa watoto wanaopatiwa matibabu.

“Baadhi ya akina mama hulazimika kulala nje ya geti la hospitali na kuingia kila siku kuwahudumia watoto wao wanapopata matibabu. Mbali na matibabu, msaada wa kijamii pia unahitajika,” amesema.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa asilimia 95 ya magonjwa ya moyo kwa watoto yanatibika kikamilifu iwapo yatagundulika mapema, hasa ndani ya siku 28 za mwanzo baada ya kuzaliwa na si zaidi ya mwaka mmoja.

Kama sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza msongamano katika JKCI, taasisi hiyo inaendelea kuimarisha ushirikiano na hospitali za rufaa za mikoa ili kuboresha huduma ikiwemo mifumo ya rufaa.

Hospitali hizo za rufaa ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Chato kama kituo cha rufaa kwa Kanda ya Ziwa pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.