Dar es Salaam. Wakati Kampuni ya Mofat inayotoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika Barabara ya Kilwa ikiomba daladala ziondolewe katika njia hiyo, wadau na wananchi wamelipinga ombi hilo, wakisema mahitaji ya usafiri ni makubwa kuliko idadi ya mabasi hayo ya mwendokasi.
Ombi la Mofat kuhusu kuondolewa kwa daladala linatokana na kile ilichoeleza, tangu inaanza kutoa huduma Oktoba 2025, kuwa inapata hasara kutokana na abiria wachache inaowapata kutokana na wangi wao kupanda daladala, bajaji na bodaboda.
Tayari kampuni hiyo, imeshawasilisha ombi kwa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra), kuomba daladala, bodaboda na bajaji ziondolewe katika njia hiyo, ili ibaki pekee kutoa huduma za usafiri kwa njia hiyo.
Katikati ya malalamiko hayo ya Mofat, wananchi na wadau wa usafiri wamesema hautakuwa uamuzi sahihi kuiruhusu kampuni hiyo pekee itoe huduma katika njia hiyo, wakirejea yaliyotokea kwa Barabara ya Morogoro na kuzua adha ya usafiri kwa wananchi.
Wananchi hao wamekwenda mbali, wakisema baadhi yao usafiri wa mabasi yaendayo haraka unawagharimu zaidi kwani, unawatoza Sh1, 000 kwa safari tofauti na daladala na bajaji zinazotoza Sh500 hadi Sh700.
Akizungumzia ombi hilo la Mofat, Mkazi wa Toangoma, Anord Kelvin amehoji kampuni hiyo inapataje hasara na kutaka kushindana na daladala na bodaboda, ilhali ina barabara yake isiyokuwa na foleni, mabasi yake yanatumia gesi na nauli yake ni kubwa.
“Ifike mahali mwendokasi wasitake kujiona wao ni bora kuliko wasafirishaji wengine, maana kila upendeleo wamepewa kuanzia miundombinu,” amesema.
Jenifer John, mkazi wa Chamazi, amesema daladala bado zinahitajika hasa kwa abiria anayekwenda Ubungo, Kawe au Mwenge ambako usafiri wa mwendokasi haujafika.
Kwa abiria huyo, amesema akipanda daladala moja kutoka Mbagala amefika, lakini akipanda mwendokasi itamlazimu kupanda magari mawili na nauli pia kuongezeka.
Oscar Shimbo, Mkazi wa Mbagala, amesema usafiri katika Jiji la Dar es Salaam bado unahitajika kwa kiasi kikubwa, kama Mofat ina mabasi mengi kuliko abiria, yapelekwe maeneo mengine ambapo miundombinu yake imeshakamilika zaidi ya asilimia 90.
“Mfano Gongo la Mboto, ile barabara ya mwendokasi tumeambiwa imekamilika kwa asilimia 90 hadi sasa, kwa nini mabasi hayo yasipelekwe huko, halafu yakija ya njia hiyo yaondolewe kwa kuwa kama ni mikataba imeandikwa na binadamu, shida iko wapi wakiibadili ili kuwanusuru wananchi na adha ya usafiri,” amesema.
Katibu wa Chama cha Madereva Tanzania (Tadwu), Ramadhan Seleman, amesema Latra kabla ya kuchukua uamuzi wa kuondoa daladala ikumbuke adha iliyotokea barabara ya Moropgoro pindi daladala zilipoondolewa.
“Kibiashara kuondolewa kwa daladala ni sawa lakini kihuduma sio sawa, kwani ukisema leo daladala ziondolewe kwa haraka yatatokea kama yale ya Kimara ambapo wananchi walipaza sauti hadi kuleta vurugu walipoona changamoto wanazozipata kwenye usafiri huo wa mwendokasi hazisikilizwi.
“Baadaye ndio tukaona Serikali ikaingilia kati kupeleka mabasi ya Mofat ili kuokoa jahazi lakini ukweli hali ilikuwa mbaya,” amesema Seleman.
Katibu huyo, amesema imekuwa mapema kusema wanapata hasara wakati hata mwaka hawajafikisha, hivyo wajipe muda kidogo.
Mwenyekiti wa madereva na makonda wa daladala Stendi ya Mbagala, Mwinshehe Chambuso amesema anachokiona ni kutofautiana kwa vipato vya wananchi, hivyo kila mtu anaamua kupanda usafiri anaoumudu.
“Mwendokasi nauli ni Sh1,000 kituo hadi kituo, lakini daladala hadi Sh500 mtu anapanda na hasa wale wanaoishia vituo vya katikati, hivi kuziondoa kabisa watakaoumia ni wananchi ukizingatia kuna wengine wakiamka asubuhi hata hiyo 1,000 hawana,” amesema Chambuso.
Hata hivyo, amesema wao wakiwa mashuhuda wanayaona magari ya Mofat yakijaza watu nyakati za asubuhi na jioni na kwamba mchana ni jambo la kawaida abiria kupungua.
Ameshauri daladala zisiondolewe kwa sasa na hata kama italazimika kufanya hivyo, ufanyike utafiti kwanza, zikiondolewa zinapelekwa wapi kwa kuwa kuna familia zinaishi kutokana na magari hayo.
“Daladala moja imeajiri watu hadi watano bado wale wa gereji, leo utakapowaondolea mkate wao huu unataka waishije, Serikali itafakari na hili pia,” amesema.
Wakati Chambuzo akisema hayo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Madereva wa Bajaji na bBodaboda, Daud Kagomba amesema wakati Mofat ikiwalalamikia, ikae ikijua wao ndio wanawaletea abiria kutoka pembezoni na hivyo wajue kuwa wanategemeana.
Kagomba amesema anashangaa inakuwaje waonekane ni washindani wao wakati wao wanabeba abiria wawili kwenye boda, bajaji hawazidi wanne, lakini wao gari moja wanapanda zaidi ya abiria 160.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliitahadharisha Serikali endapo itaamua kuziondoa, watarajie wakabaji na vibaka watarudi tena mtaani ukizingatia hadi sasa sekta hiyo imeajiri zaidi ya watu 200,000 huku Wilaya ya Temeke pekee bajaji na bodaboda zilizosajiliwa hadi sasa ni zaidi ya 38,000.
Amesema Mofat wanachotakiwa ni kuangalia nini waboreshe badala ya kuwalalamikia bodaboda na bajaji ambao hawafanani nao.
Amesema usafiri huo wa mwendokasi umeanzishwa na Serikali ili kuondoa adha ya usafiri kwa maeneo ambayo abiria walikuwa wakipata tabu ikiwemo wa Mbagala ambapo imeshuhudiwa watu wakipandia madirishani.
Mmoja wa wamiliki wa daladala ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema walishakaa vikao vingi na Latra kuwapa ushauri wa namna ya kuziondoa daladala bila kuleta athari, ikiwemo kupewa zabuni ya kutoa abiria pembezoni na kuwapeleka kwenye vituo vha mabasi hayo.
Hata hivyo, amesema wameshangaa zabuni hiyo kupewa kampuni ya kigeni wakati maamuzi hayo huko baadaye yanaweza kuleta shida kwa watu wenye daladala.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusiana na tathimini yao tangu wameanza kutoa huduma hiyo, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Mabrouk Masasi amesema tangu wameanza kutoa huduma wanapata hasara.
Akifafanua zaidi hilo, Masasi amesema ilitakiwa mabasi hayo yanapoingia barabarani daladala, bajaji pamoja na bodaboda nazo ziwe zimeshaondolewa katika njia, lakini cha kusikitisha ni kwamba mpaka leo zipo.
“Kutokana na kufanya kazi sambamba na vyombo hivyo vya, tumejikuta tukigawana abiria waliopo na hivyo hakuna faida tunayoipata na pia ndio maana tumeshindwa kuongeza magari mengine barabarani kwani mpaka sasa ni 40 tu ndio yaliyo barabarani huku 160 yakiwa yameekeshwa.
“Hii kibiashara haijakaa sawa, ukiacha magari kutofanya kazi, tuna mikopo tuliyoingia katika kuyanunua inatakiwa marejesho, tuna madereva zaidi 187 tumewaajiri leo hawatumiki wote wakati mwisho wa mwezi wanatakiwa wapewe mishara na marupurupu yao yote,” amesema Ofisa huyo.
Ni kutokana na hali hiyo, amesema wameshaiandikia Latra kuomba kuondolewa kwa daladala na bajaji hizo ili waweze kupata walau faida kidogo ya kujiendesha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Latra, Salum Pazzy alikiri wamepokea nakala ya barua hiyo na kueleza wapo wanaifanyia kazi kwa kuwa ni jambo linalotakiwa kuwashirikisha na wadau wengine katika sekta hiyo ya usafirishaji.