Museveni aongoza kura asilimia 76.25, Bobi Wine 19.85 akilia kuhujumiwa

Uganda. Tume ya Uchaguzi ya Uganda (EC) katika matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu, imesema mgombea wa Chama cha National Resistance Movement (NRM), Yoweri Museveni anaongoza kwa asilimia 76.25 ya kura zilizohesabiwa hadi sasa kutoka vituo 22,758 vya kupigia kura.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Simion Byabakama, matokeo ya awali yanatokana na kura halali 5,194,338 zilizohesabiwa hadi sasa.

“Kura batili hadi sasa ni 129,441. Jumla ya kura zilizopigwa ni 5,323,779, sawa na asilimia 24.59 ya wapigakura wote waliosajiliwa kwenye daftari la taifa. Jumla ya kura zilizoharibika ni 17,271,” amesema Byabakama.

Rais Museveni akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Karo huko Rwakitura Januari 15, 2026. PICHA/SCREEN-GRAB/UBC



Tovuti ya Daily Monitor wa nchini Uganda, imeeleza kuwa matokeo ya awali yaliyotolewa na tume hiyo leo Ijumaa asubuhi Januari 16, 2026 yanaonyesha kuwa mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi  maarufu Bobi Wine wa Chama cha National Unity Platform (NUP), anafuata kwa kupata kura 1,312,047, sawa na asilimia 19.85 ya kura zote zilizohesabiwa hadi sasa.

Jumla ya Waganda 21,649,067 walijiandikisha kupiga kura katika vituo 50,739 nchini huko katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Januari 15, 2026.

Jana, iliripotiwa upigaji kura ulichelewa katika maeneo mbalimbali kutokana na hitilafu za mashine bayometriki (BVVK), hali inayotajwa kuwa ilitokana na kutokana na kukatika kwa mtandao wa intaneti.

Mgombea Chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine akipiga kura.



Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Byabakama, mgombea urais wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC), James Nandala Mafabi, amepata kura 108,301 sawa na asilimia 2.08 ya kura zilizohesabiwa hadi sasa, huku Frank Bulira Kabinga wa Chama cha Revolutionary People’s Party (RPP) amepata kura 23,267 sawa na asilimia 0.45 ya kura halali zilizohesabiwa.

Wagombea wengine ni Robert Kasibante wa National Peasants Party (NPP) aliyepata kura 15,929 (asilimia 0.31), Joseph Mabirizi wa Conservative Party (CP) mwenye kura 10,910 (asilimia 0.21), Meja Jenerali mstaafu Gregory Muntu wa Alliance for National Transformation (ANT) aliyepata kura 29,504 (asilimia 0.57), na Mubarak Munyagwa wa Common Man’s Party (CMP) aliyepata kura 14,742 (asilimia 0.28).

 Matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Alhamisi yanatarajiwa kutangazwa Jumamosi, Januari 17, 2026.

Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81, anatafuta kuendeleza utawala wake zaidi ya miongo minne, huku upinzani ukiripoti kuwepo kwa “ujazaji wa masanduku ya kura kwa wingi” na kukamatwa kwa viongozi wao wakuu.

“Dunia inapaswa kujua kinachoendelea Uganda siku ya uchaguzi. Intaneti imezimwa. Ripoti za ujazaji wa kura zipo kila mahali. Viongozi wetu, wakiwemo Naibu Rais wa Kanda ya Magharibi, wamekamatwa. Mawakala na wasimamizi wetu wengi wametekwa nyara, na wengine kufukuzwa vituoni. Mashine za BVVK zimeshindwa kufanya kazi kila mahali,” amesema Bobi Wine katika ujumbe wake katika mitandao ya kijamii.