Kocha Yanga amvuta Ahoua | Mwanaspoti

Muda mfupi umebakia kwa kiungo Jean Charles Ahoua kukamilisha uhamisho wa kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria akitokea Simba.

Ahoua anaachana na Simba huku mkataba wake ukiwa umebakiza muda wa miezi sita baada ya kuitumikia timu hiyo kwa mwaka mmoja na nusu.

Baada ya mazungumzo ya kuongeza mkataba baina ya kiungo huyo mshambuliaji na Simba kushindwa kufikia muafaka, klabu hiyo imeona ni afadhali imuuze Ahoua ili ipate fedha zinazoripotiwa kuwa zaidi ya Dola 150,000 (Sh378 milioni) badala ya kubaki naye hadi mwishoni mwa msimu ambapo ataondoka bure.

Wakati nyota huyo kutoka Ivory Coast akiwa mbioni kukamilisha usajili wake wa kutua Belouizdad, tayari ameruka kiunzi kimoja, kitendo ambacho kinaweza kumuweka katika uwezekano mkubwa wa kujihakikishia namba kikosini licha ya ugeni wake.

Kiunzi hicho ni cha kitakwimu katika nafasi anayocheza ambapo anaonekana kuwa na takwimu bora kulinganisha na mchezaji mwingine wa nafasi yake ambaye atawania naye namba ndani ya kikosi cha Belouizdad.

Kuanzia msimu uliopita hadi sasa, Ahoua ameonekana kumtesa Abdelmalek Kelaleche ambaye ndio kiungo pekee mshambuliaji aliyepo kwenye kikosi cha CR Belouizdad inayonolewa na Kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic.

Katika msimu uliopita, Kelaleche alifunga bao moja tu katika mechi 23 alizoichezea Club Africain ya Tunisia ambayo aliitumikia kabla ya kutua Algeria.

Wakati kiungo huyo Mualgelia alihusika na bao moja tu katika msimu uliopita, Ahoua alimaliza akiwa amehusika na mabao 25 ambapo alifunga mabao 19 na kupiga pasi tisa za mwisho.

Katika msimu huu, licha ya Ahoua kutopata sana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba, bado ana takwimu bora kumzidi Kelaleche.

Wakati Kelaleche akiwa hajahusika na bao lolote katika mechi 12 alizochezea Belouizdad katika mashindano tofauti, Ahoua ameshahusika na mabao mawili ambayo yote amefunga, moja likiwa ni la Ligi Kuu Tanzania Bara na lingine la Ligi ya Mabingwa Afrika.