BEKI wa kulia wa Pamba Jiji ya Mwanza, Yunus Lema ameshindwa kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo kumrejesha kikosini katika dirisha dogo licha ya kuwa na takwimu nzuri katika Ligi ya Championship.
Lema anacheza katika klabu ya Mbuni FC ya Arusha aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Pamba Jiji kwa mkopo ili kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Beki huyo kinda, alisajiliwa na Pamba Jiji msimu wa mwaka 2024/2025 akitokea Mbuni ya Arusha, hata hivyo ameshindwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza chini ya makocha Goran Kopunovic, Fredy Delix ‘Minziro’ na sasa Francis Baraza.
Akiwa na Mbuni FC mpaka sasa, Lema amefunga bao moja na assisti sita, huku akiwa kinara kwenye Ligi ya Championship kwa kucheza dakika nyingi (1,179) sawa na Martin Kiggi (Geita Gold) na Naku James (Polisi Tanzania).
Wanafuatiwa na Fredy Tangalo na Said Kipao wote kutoka Kagera Sugar waliocheza dakika 1,177, huku Adam Uledi na Issa Dau wa Transit Camp wakicheza dakika 1,175.
Lema aliliambia Mwanaspoti kuwa Mbuni imempa nafasi ya kucheza na kuonyesha uwezo wake, huku akiuachia kazi uongozi wa Pamba kuamua hatma yake kwani yuko tayari na ameiva kukiwasha kwenye Ligi Kuu Bara.
“Nashukuru nimeanza vizuri hapa Mbuni na nimeaminiwa na kuanza katika mechi zote. Niko hapa kwa mkopo natumaini nitarejea Pamba lakini mpaka sasa sijarudi Mwanza kuungana na wenzangu kambini,” amesema Lema.
Aliongeza; “Mpaka sasa sijaonga na Kocha (Francis Baraza) kujua kama ananihitaji, lakini niko tayari kwenda kuendeleza hiki nilichokionyesha katika daraja la kwanza 9Championship).”
Kuhusu beki huyo, Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William amesema mipango ya benchi la ufundi ni kuendelea kumpa muda mchezaji huyo aendelee kucheza Ligi ya Championship hadi mwisho wa msimu huu.
“Tunafurahishwa na namna anavyocheza huko lakini hatujamrudisha kwenye timu katika dirisha dogo kwa sababu kocha (Francis Baraza) ameridhia mkataba wa mkopo na Mbuni uendelee hadi mwisho wa msimu,” amesema William.