Geita. Wazazi na walezi ambao hawajapeleka watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza katika muhula mpya wa masomo 2026, wametakiwa kufanya hivyo badala ya kuwaozesha katika umri mdogona kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Wito huo umetolewa na Naibu Meya wa Manispaa ya Geita, Elias Ngole akiwataka wazazi na walezi katika kata hiyo kuacha mazoea ya kuwatumia watoto wao katika shughuli za kilimo, na badala yake kuwapa elimu kwa faida yao ya baadaye.
Ngole ambaye pia ni diwani wa Kata ya Nyanguku alitoa wito huo Januari 15, 2026 katika Shule ya Sekondari Nyanguku wakati wa ugawaji wa madaftari kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, ambapo wanafunzi 90 wamesharipoti kati ya 135 waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Aidha, Ngole ameonya baadhi ya wazazi wanaothamini posa na kuwaozesha watoto wao katika umri mdogo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria, taratibu na kanuni za nchi.
“Tuwatoe watoto nyumbani waje wasome, tuko nyuma sana. Mikoa yetu hii ni kati ya mikoa iliyoonekana sisi elimu tuliweka pembeni. Kuozesha kisiwe kipaumbele kwa mtoto mdogo; wakati mwingine anayeoa na anayeolewa awe aliyefikia umri wa kujitambua,” amesema Ngole.
Kata ya Nyanguku ina shule mbili za sekondari ambazo ni Shule ya Sekondari Nyanguku, ambapo wanafunzi 90 kati ya 135 wamesharipoti, huku Nyakato Geita Sekondari wakiripoti wanafunzi 39 kati ya 69 waliopangiwa.
Viongozi wa kata hiyo Jumatatu, Januari 19, 2026, wanatarajia kuanza kufuatilia wazazi ambao hawajapeleka watoto wao shuleni.
“Kama una mtoto ulitakiwa umpeleke darasa la awali bado unaye nyumbani, kama una mtoto alitakiwa aende darasa la kwanza bado unaye nyumbani, kama una mtoto wa sekondari unaye nyumbani—Jumatatu tuna wewe. Ukishawaona sungusungu wanazunguka kule, wala usinipigie simu,” amesema Ngole.
Naye Leo Elias, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyanguku, amesema kutokana na mabadiliko ya sera katika sekta ya elimu, ambapo elimu ya msingi inaishia kidato cha nne, amewasihi wazazi kuzingatia haki ya watoto wao kupata elimu.
“Wazazi wawahimize watoto kuja shule ili wapate kile ambacho Serikali inahitaji wapate, na suala la kuozesha siyo wakati wake kwa sasa, kwani huu ni wakati wa mtoto wa kike na wa kiume kupata elimu ili ajikwamue katika maisha yake binafsi,” amesema Leo Elias.
Ofisa Elimu Kata ya Nyanguku, Inocent Asese, amesema baadhi ya wanafunzi hufanya vibaya darasani kutokana na kuchelewa kujiunga na masomo maalumu ya msingi yanayofundishwa pindi wanapojiunga na shule walizopangiwa.
“Wazazi niwaombe kuleta watoto shuleni. Wakiripoti mapema, inawarahisishia walimu namna ya kuwafundisha. Hivyo wanapowachelewesha, wanasababisha walimu wasifundishe katika utaratibu waliojiwekea,” amesema Asese.
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu huyo, licha ya juhudi za Serikali na wadau kuendelea kuboresha mazingira wezeshi ya kujifunzia, suala la utoro limeendelea kuwa kikwazo cha mafanikio ya kielimu katika kata hiyo.
“Huku kuna shughuli za kilimo zinazofanyika kipindi kama hiki; kuna kilimo cha mpunga lakini pia kuna kilimo cha bustani. Ni wazalishaji wazuri wa nyanya, vitunguu na mbogamboga. Shughuli hizi zinafanya wanafunzi kuwa na utoro wa rejareja,” amesema Leo Elias.