Omary Chibada anukia KMC FC

KMC inaendelea na maboresho katika dirisha hili dogo la usajili ambapo kikosi hicho cha Kinondoni jijini Dar es Salaam kiko kwenye hatua za mwisho za kumsajili kiungo Omary Chibada.

Kiungo huyo mkabaji anayeichezea Mbeya City aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu akitokea Kagera Sugar, yupo katika mazungumzo na KMC ambayo imeonyesha nia ya kumhitaji ili kuongeza nguvu katika kikosi.

Chanzo kimeliambia Mwanaspoti kwamba, Chibada ataruhusiwa kuondoka Mbeya City baada ya ujio wa Abdallah Kulandana aliyetokea Fountain Gate, Said Naushad (MFK Karvina B) ya Jamhuri ya Czech na Hijjah Shamte aliyeachana na Kagera Sugar.

“Mazungumzo ya awali ni ya kumtoa kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu, lakini uamuzi wa mwisho bado haujafikiwa. Lengo ni kumpa nafasi ya kucheza na kuonekana. Kwa sasa viungo tuliowasajili inaweza ikawa ngumu kwake,” kilisema chanzo hicho.

KMC inayonolewa na Abdallah Mohamed ‘Baresi’ aliyejiunga nayo Desemba 30, 2025 akichukua nafasi ya Mbrazili Marcio Maximo inapambana ili kupata saini ya kiungo huyo kabla usajili haujafungwa Januari 30, 2026.

Mwanaspoti linatambua mabosi wa KMC wanaitaka huduma ya kiungo huyo aliyeanzia kituo cha JMK Youth Park ambako alikuzwa kiufundi huku akizichezea Yanga ya vijana na wakubwa pamoja na Biashara United.

KMC inapambana kupata saini ya kiungo huyo ambapo mabosi wanaamini atakuwa mbadala sahihi wa Ahmed Bakari Pipino aliyevunja mkataba na kujiunga na Singida Black Stars.

KMC ndio inayoburuza mkia katika Ligi Kuu ikiwa na pointi nne kupitia mechi tisa, ikishinda mara moja na kutoka sare moja, ikipoteza mechi saba na kufungwa mabao 14, huku ikifunga mawili yote kupitia kwa Daruwesh Saliboko.