Dodoma. Serikali ya Malawi imetangaza kuanza kutumia Hospitali ya Rufaa ya Benjamini Mkapa kama kituo maalumu cha tiba kwa wagonjwa wanaotoka nchini humo, ikitaja sababu kuu nne za uamuzi huo.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Januari 16, 2026 na Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Serikali ya Malawi, Modalitso Baloyi, alipotembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea huduma zinazotolewa, ikiwemo ubora wa miundombinu kwa wagonjwa.
Waziri Baloyi ametaja sababu za uamuzi wa Malawi kuwa ni ukaribu wa kijiografia ikilinganishwa na umbali wa kwenda mataifa ya Ulaya ambako awali walikuwa wakipeleka wagonjwa wao, gharama ndogo za matibabu, uhakika wa kupata huduma, pamoja na utayari wa hospitali hiyo kutoa mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu wao.
Amesema mwanzoni mwa Desemba 2025, Malawi ilituma timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya kutembelea Hospitali ya Benjamini Mkapa kwa ziara ya mafunzo, na kwamba taarifa yao ndiyo iliyomchochea kuja Tanzania, akisisitiza kuwa ripoti hiyo iliipa Serikali yao matumaini makubwa.
“Hapa ni jirani na sisi ukilinganisha na mataifa ya Ulaya. Leo Serikali tumekuja kuona kile ambacho tuliambiwa na wataalamu wetu. Hakika nimeridhishwa na huduma za hapa, nimeridhishwa na mazingira na sasa uamuzi ni kuwaleta watu wetu hapa, labda kwa tiba ambazo hazipatikani ndipo tutakwenda Ulaya,” amesema Baloyi.
Mwanasiasa huyo amesema mahusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili yamekuwa ya kudumu, ndiyo maana wameamua kuchagua Tanzania kama kituo cha kupata huduma za kibingwa, huku akisisitiza kuwa wataendelea kujenga uwezo kwa kupata ujuzi wa kina kutoka kwa wataalamu wa Hospitali ya Benjamini Mkapa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, tayari wananchi wa Malawi wameshaanza kupata huduma katika hospitali hiyo na wameonyesha kuridhishwa, hususan katika eneo la tiba za kibingwa, jambo linalotoa matumaini makubwa kwa wagonjwa na ndugu zao.
Waziri wa Afya na Usafiri wa Mazingira wa Serikali ya Malawi Modalitso Baloyi (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa Profesa Abel Makubi
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema mkakati wa hospitali hiyo kutoa mafunzo ya kibobezi na matibabu ya kibingwa ndiyo chanzo cha Malawi kuvutiwa na huduma zinazotolewa.
Amebainisha kuwa timu ya madaktari na wataalamu wa Malawi walipofika mwishoni mwa mwaka jana walikuta huduma zilizozidi matarajio yao, hali iliyowafanya kuishauri Serikali yao.
Profesa Makubi amesema miongoni mwa huduma zilizowavutia ni matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo, upandikizaji wa figo na upandikizaji wa uroto, huduma ambazo kwa Malawi zilikuwa zikipatikana kutoka mataifa makubwa ya ng’ambo.
Ameongeza kuwa tangu mwaka 2016 hospitali hiyo imetoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 400 kutoka mataifa mbalimbali, na kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 pekee jumla ya wagonjwa 46 kutoka nchi tofauti wamepata huduma za matibabu ya kibingwa.
Kwa mujibu wa Profesa Makubi, kwa sasa Hospitali ya Benjamini Mkapa inashirikiana na mataifa ya Malawi, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Comoro na Zambia.
Amesema katika ushirikiano huo, mbali na madaktari na wagonjwa kutoka mataifa hayo kuja Tanzania kupata huduma, pia kumekuwepo na kliniki tembezi ambapo madaktari wa hospitali hiyo huenda kutoa huduma katika nchi hizo, hali inayochochea wengi kufanya utalii wa afya kwa kuja Tanzania kuona na kujifunza kinachofanyika.