Mwili wa mtoto mchanga watupwa shambani Arusha

Arusha. Simanzi imetawala leo Januari 15, 2026 katika Mtaa wa Korongoni jijini Arusha baada ya mwili wa mtoto mchanga mwenye jinsia ya kike kukutwa umetupwa pembezoni mwa shamba la migomba.

Mwili wa mtoto huyo umekutwa shambani ikiwa zimepita siku tano tangu mwili mwingine wa mtoto wa kike kukutwa kwenye mfuko wa salfeti kwenye takataka jijini Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo amesema upelelezi wa matukio hayo unaendelea.

“Bado tunapeleleza wahusika waliotekeleza ukatili huo kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika, hivyo tutakavyobaini chochote tutawajulisha” amesema.

Akizungumza katika eneo la tukio Mwenyekiti wa Mtaa wa Korongoni, Goodluck Lekaju amesema alipigiwa simu na wananchi saa tano asubuhi kuwa kuna tukio la mwili wa mtoto kukutwa shambani na alipofika alishuhudia tukio hilo.

“Nilipofika nikashuhudia mwili wa mtoto huyu akiwa uchi wa mnyama, na katika uchunguzi wa awali tukakuta na kondo la uzazi limefukiwa pembeni ya mwili huo.

“Niliamua kuwapigia simu polisi na wakafika eneo la tukio kuchukua mwili huo huku sisi tukikubaliana kuanza msako wa kubaini nani anahusika na kitendo hiki,” amesema.

Mkazi wa eneo hilo Neema Swali amesema asubuhi saa tano hiyo alituma watoto wake dukani kununua mahitaji na ndipo wakarudi wakidai wameona mtoto shambani.

“Nilitoka kufuata njia wanayonionyesha ndio nikashuhudia mwili huo wa mtoto ukiwa mtupu na umetapakaa damu kuashiria amezaliwa hapo hapo na kutelekezwa asubuhi hii ,ndio nikaanza kupiga kelele watu wengine wakaja,” amesema.

Naye mmiliki wa shamba hilo, Rispa Simon amesema alisikia kelele pembeni ya shamba lake na alipokuja alikuta watu wengi na aliposogea zaidi alishuhudia mwili huo kabla ya kuamua kuufunika na kusubiri gari la polisi.

“Kiukweli ni tukio la kinyama sana, maana huyu mtoto anaonekana alitimia miezi tisa na mtu akaja kujifungua hapa na kwa mwonekano mtoto alikuwa na zaidi ya kilo nne kwa unene na afya nzuri”

Ametumia nafasi hiyo kulaani kitendo hicho na kuiomba jamii ya wananchi wa Korongoni kushirikiana kufanya msako wa kumpata mtuhumiwa aliyetekeleza tukio hilo.

“Huu ni ukatili wa hali ya juu jamani, hata kama mwanamke unapitia hali ngumu kiasi gani haifai kufanya hivi kwa kiumbe cha Mungu, mimi naomba Serikali iongeze nguvu ya upelelezi kumpata mtu huyo maana hii ni laana anatuletea” amesema.

Hili ni tukio la pili ndani mwezi huu baada ya Januari 11, 2026 katika mtaa wa Long’dong iliyoko kata ya Sokon One, mwili wa mtoto wa mchanga anayekadiriwa kuwa na miezi saba, ulikutwa umetupwa juu ya taka zinazosubiri kuzolewa.

Mwili huo wa jinsi ya kike uliokuwa kwenye mfuko wa salfeti na haijafahamika nani alihusika na tukio hilo.