Uchaguzi mkuu waahirisha kufungua shule Uganda

Wizara ya Elimu na Michezo nchini Uganda imetangaza kuahirishwa kufunguliwa kwa shule na taasisi zote za elimu nchini humo hadi Jumanne, Februari 10, 2026, ikitaja sababu za Uchaguzi Mkuu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Kadrace Turyagyenda leo Ijumaa Januari 16, 2026 imeeleza kuwa shule zitafunguliwa Februari 10, 2026 badala ya Februari 2, kama taarifa ya Januari 6, 2026 ilivyoeleza.

“Taarifa hii inawahusu wadau wote wa elimu kwamba, kutokana na Uchaguzi Mkuu na kwa lengo la kulinda usalama wa wanafunzi wote, shule na taasisi zote za elimu nchini Uganda zitafunguliwa rasmi Jumanne, Februari 10, 2026,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Uamuzi huo unahusu shule zote za serikali na binafsi, shule za kimataifa, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu.

“Ili kuepusha sintofahamu, maelekezo haya yanajumuisha pia shule za kimataifa, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara, mabadiliko hayo yamelenga kutoa fursa ya kufanyika kwa mchakato wa uchaguzi kwa usalama na utulivu, huku yakipunguza athari zinazoweza kujitokeza katika shughuli za masomo na kulinda ustawi wa wanafunzi.

Wakuu wa shule wameelekezwa kuzingatia kikamilifu tarehe mpya za kufunguliwa na kufuata kalenda rasmi ya shule iliyochapishwa kwenye tovuti ya Wizara.

Aidha, wazazi, walezi, wanafunzi na umma kwa ujumla wametakiwa kuzingatia mabadiliko hayo ili kuepusha mkanganyiko.

Wizara imesisitiza kuwa endapo kutakuwa na mabadiliko au taarifa zaidi, zitatolewa kupitia njia rasmi za mawasiliano.

Katika tangazo lake la awali la kalenda ya shule lililotolewa Januari 6, Dk Turyagyenda alisisitiza kuwa saa rasmi za masomo kwa shule za msingi na sekondari ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:30 jioni, huku shule za awali zikifanya masomo kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana.

Ili kukabiliana na msongamano wa magari, hususan katika maeneo ya mijini, wakuu wa shule za bweni katika eneo la Jiji la Kampala wameelekezwa kupanga ratiba tofauti za kufungua na kufunga shule kwa madarasa mbalimbali.

Ameongeza kuwa siku za kufungua shule, ratiba za ziara za wazazi na shughuli nyingine kubwa za mwaka zinapaswa kupangwa kwa kushirikiana na shule jirani ili kuepusha msongamano na vurugu.

“Usimamizi wa shughuli hizi unapaswa kufuata miongozo ya usalama katika burudani, michezo ya ziada na uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi katika shule za awali, msingi na sekondari,” imeeleza sehemu ya maelekezo ya awali ya Wizara.