Wenyeviti Chadema waja na maazimio saba yaliyokea Oktoba 29

Dar es Salaam. Umoja wa Wenyeviti wa Mikoa 31 ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umekuja na maazimio ya kuunga mkono kile kilichofanywa na Kamati Kuu juu ya matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Siku hiyo ya uchaguzi kuliibuka maandamano yaliyozua vurugu, uharibifu wa mali na vifo vya watu.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Tume ya Uchunguzi wa kilichotokea Oktoba 29, 2025, ambayo inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande.

Kamati Kuu ya Chadema chini ya Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, Desemba mwaka jana ilikutana kwa njia ya mtandao na kutoka na msimamo kuhusu kadhia hiyo.

Kwenye msimamo wake, ilipendekeza ulipaji wa fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, uwajibikaji kwa wote waliohusika na kuzuia ukandamizaji wa kisiasa na uhalifu wa dola kabla, wakati na baada ya Oktoba 29, miongoni mwa mambo mengi.

Mambo hayo na mengine yamejadiliwa na kuungwa mkono na mkutano wa wenyeviti wa mikoa, uliofanyika kwa njia ya mtandao jana, kisha tamko likatolewa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai.

Mungai katika taarifa hiyo, amedai Oktoba 29, 2025 hakukuwa na uchaguzi bali uhalifu wa kisiasa na kilichotokea kinahitaji uwajibikaji wa kitaifa na kimataifa.

“Tunaunga mkono azimio la Kamati Kuu la kuwepo uwajibikaji wa vyombo vya usalama na mageuzi ya vyombo vya usalama… Fidia kwa wapendwa waliopoteza familia zao, mchakato wa Katiba mpya, haja ya jumuiya ya kimataifa kutumia mikataba yao kutuweka sawa,” amesema.

Mungai amesema imani ya Watanzania kwa Chadema kwa sasa ipo juu kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

“Wananchi wameitambua Chadema kama chama kilichosimama imara kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa 2025 bila kuyumba na kusaliti dhamira ya Watanzania,” amesema.

Amesema wananchi wameielewa Chadema na kuisimamia kikamilifu agenda ya No Reforms No Election (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi), akisema kaulimbiu hiyo ni msimamo wa msingi unaotokana na uzoefu wa wananchi kuibiwa kura mara kwa mara.

Amesema wananchi wanafahamu fika kuwa bila mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi na mazingira sawa ya kisiasa, hakuna uchaguzi wa haki unaoweza kufanyika nchini.

Katika kukuza zaidi chama hicho, amesema wenyeviti hao wamekubaliana kuongeza ushawishi kwa wananchi, kuimarisha chama katika ngazi zote na kuongeza mapambano ya kudai haki nchini.

Kuhusu zuio la mahakama, mazingira ya kisiasa na polisi, Mungai amesema pamoja na wananchi kuwaunga mkono Chadema, mazingira ya kisiasa nchini bado ni magumu, yasiyo huru na yenye kukiuka Katiba.

“Polisi wameendelea kutumia kile wanachokiita zuio la mahakama kama kisingizio cha kuzuia vikao halali vya kisiasa, kuvuruga mikutano ya chama, kukamata viongozi wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayoendelea hadi sasa,” amesema.

Amesema hakuna zuio lolote la mahakama linaloweza kuminya haki ya kikatiba ya watu kukutana na kuzungumza.

Mungai amesisitiza matukio yaliyotokea Oktoba 29 yanahitaji uwajibikaji na uchunguzi huru wa kimataifa.

Akizungumzia kamatakamata ya viongozi wa Chadema kabla na wakati wa uchaguzi, amesema mamia ya wananchi na wanachama wa chama hicho walikamatwa na kufunguliwa kesi za kisiasa zilizolenga kuwanyamazisha.

“Tunasisitiza mahabusu wote wa kisiasa waachiwe huru na ukamataji wa wananchi kwa sababu za kisiasa usitishwe mara moja,” amesema.

Amezungumzia vizuizi vilivyowekwa barabarani baada ya uchaguzi, akisema vimegeuka kuwa rushwa na vyanzo vya mapato pamoja na ukiukwaji wa haki za wananchi kunyimwa uhuru wa kutembea, ambapo amesema kanda ya Serengeti na ya Ziwa zimeathirika zaidi.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche, akizungumza baada ya kusomwa kwa tamko hilo, ameitaka Serikali kumwachia Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kwa kuwa imeruhusu demokrasia ya kisiasa.

“Kama wanaamini wao wana waumini wengi na Lissu ana waumini wachache, wamuachie wapambane kwenye uwanja wa siasa. Siasa inapokuwa na nguvu nchini itaondoa wananchi kulalamikia Serikali,” amesema.

Lissu yupo gerezani kwa zaidi ya siku 250 sasa akikabiliwa na kesi ya uhaini ambayo itaendelea Februari 9.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Manyanya Malambaya amesema tamko la wenyeviti hao linazungumzia haki ya wananchi.

“Nawapa pole Watanzania kwa mazingira waliyopitishwa na watawala wa nchi hii wametupeleka kwenye uchaguzi ambao ni mgumu sana kuufikiria na kwenda kuutazama,” amesema.