Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashantu Kijaji amekitaka Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kutoa mafunzo ya lugha nyingine za kimataifa ambazo Tanzania inapokea watalii wengi kutoka kwao.
Waziri Kijaji ametoa wito huo leo Ijumaa Januari 16, 2026 kwenye mahafali ya 23 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nimesikia chuo kimeanza kutoa mafunzo ya lugha ya kichina, hivyo hivi karibuni tutegemee kupata wageni wengi kutoka China. Lakini pia ni vizuri kutoa na masomo ya lugha za mataifa mengine ambayo tunapokea wageni wengi kutoka kwao,” amesema Waziri Kijaji.
Kwa mujibu wa Waziri huyo kuanzia Januari 2025 hadi Novemba 2025, idadi ya watalii imeongezeka hadi kufika watalii 2,097,823 ikilinganishwa na watalii 1,924,240 kwa mwaka 2024.
Wahitimu wa chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) leo Januari 16,2026.
Pia amesema sekta hiyo kila mwaka inazalisha ajira milioni 1.5 zilizo rasmi na zisizo rasmi za moja kwa moja na zisizo rasmi, hivyo kuwa na wanataaluma wa fani hiyo wanaojua lugha nyingi kutafanya wageni wafurahie wanapokuwepo hapa nchini.
“Matamanio yetu ni kuona wanataaluma wetu wanatoa huduma kwa watalii zenye viwango vya kimataifa ili watoke wakiwa wameridhika.
“Kwani ni kutokana na changamoto hizo utakuta katika hoteli nyingi hasa za nyota tano asilimia 75 wahudumu wake sio watanzania hivyo lazima tuanze na watoto wetu.”
Waziri huyo amesema:”Lazma tujiimarishe katika maeneo hayo kuweza kuchukua nafasi hizo ukizingatia tuna malengo kama nchi kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2028 hivyo hatuna budi kufanya maboresho makubwa katika sekta hii kuanzia kwenye kuwapika wataalam wetu.”
Pia, katika mahafali hayo Waziri Kijaji ametoa baadhi ya maagizo ikiwemo kukitaka chuo hicho kuhakikisha wanatoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya sasa na yanayokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa upande wa Wizara ameitaka kuratibu vyuo vyote vinavyotoa fani hizo za ukarimu na utalii ili viweze kufundisha na kutoa wataalam wenye ujuzi unaokidhi viwango vya kimataifa.
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Dk Flourian Mtei, amesema katika mahali hayo wamewatunuku wahitimu 674 ngazi ya Astashahada na Shahada katika fani za utalii, ukarimu na uandaaji wa matukio.
Amesema chuo hicho chenye matawi manne ikiwemo lile la Bustani na Temeke ya jijini Dar es Salaam, Mwanza na Arusha tangu kianzishwa kwake kumekuwepo na mafanikio mbalimbali.
Dk Mtei ameyataja mafanikio hayonkuwa ni pamona na kuongeza udahili wa wanafunzi na wahitimu kila mwaka na hivyo kusaidia kutoa mchango wao katika utoaji wa huduma kwenye sekta ya utali
Naye Mwenyekiti wa bodi wa chuo hicho, Sharifa Salim Omar amesema ana imani wahitimu hao kwa muda wote waliokuwepo chuoni hapo wamepikwa vema hivyo ni imani yake watakwenda kuwa mabalozi wazuri huko watakapokwenda.
Kwa upande wao wahitimu, Janet Chuwa aliyesomea fani ya kuongoza watalii amesema matarajio yake ni kwenda kufanya kile alichofundishwa ukizingatia fani hiyo haichoshi kwa kuwa unakwenda kuangalia vivutio mbalimbali.
Joseph Marwa aliyehitimu fani ya ukarimu,amesema ni matarajio yake kupata ajira kwa kuwa wamehakikishiwa na serikali kuwepo kwa soko kwa wahitimu wa sekta ya utalii aina.
Hata hivyo wito wake kwa serikali kusaidia wanafunzi wasiojiweza na wanye ndoto za kusomea fani hizo za utalii kwa kuwa kuna baadhi wanaochaguliwa na chuo kusoma lakini wanakwama kwenye ada.