Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Temeke imepanga Januari 23, 2026 kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya wizi wa Sh62.8 milioni, inayomkabili Laila Khatibu (42).
Khatibu ambaye alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya African Energy Ltd, anakabiliwa na kesi ya jinai namba 4085 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la wizi.
Kesi hiyo ilipangwa leo Ijumaa Januari 16, 2026 kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, lakini shahidi wa jamhuri ambaye alitakiwa kutoa ushahidi wake amepata msiba.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda, anayesikiliza kesi hiyo ameahirisha hadi Januari 23, 2026 itakapoendelea.
Awali, Wakili wa Serikali Shabani Shabani alidai, kesi hiyo imeletwa kwa ajili ya uamuzi mdogo na kuendelea kusikilizwa.
“Shahidi wa upande wa mashtaka ambaye alitakiwa kuendelea kutoa ushahidi Said Seif, amepatwa na msiba hivyo ameshindwa kufika mahakamani,” alidai na kuongeza.
“Kwa hali hii, tuomba mahakama ipange tarehe nyingine ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa Jamhuri,” alidai.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana
Katika kesi msingi, Laila anadaiwa kati ya Januari 2022 hadi Agosti 2023, katika kituo cha kujaza mafuta cha Kurasini Flour kilichopo Wilaya ya Temeke, aliiba fedha za mwajiri wake.
Mshtakiwa huyo, anadaiwa kuiibia kampuni hiyo Sh62.8 milioni, fedha ambazo zilifika kwake kutokana na nafasi yake ya ajira.