Waarabu waanza figisu, waipeleka Yanga ‘mafichoni’

KIKOSI cha Yanga keshokutwa kinashuka uwanjani kucheza Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa kabla ya kuondoka Jumatano ijayo kwenda Misri kuvaana na Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kuna taarifa ya kushtua kwa mabingwa hao wa Tanzania.

Yanga watakuwa wageni wa Al Ahly Ijumaa ijayo katika mechi ya raundi ya tatu ya Kundi B la Ligi ya Mabingwa, kila moja ikiwa na pointi nne baada ya awali kushuka uwanjani mara mbili, lakini ni kama wenyeji wameipania mechi hiyo kwa kuamua kuipeleka machinjioni.

Al Ahly imeipeleka mechi hiyo kwenye Uwanja wa Borg El Arab uliopo Alexandria ikiwa ni mwendo wa wastani wa saa nne kutoka Cairo kwa usafiri wa treni au basi.

Yanga si wageni wa uwanja huo kwani waliwahi kupelekwa na wapinzani wao hao 2016 na kupasuka mabao 2-1 wakatolewa katika raundi ya pili ya michuano kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kutoka sare ya bao 1-1 Dar na kushindwa kutinga makundi.

Katika mechi hiyo, Al Ahly ilitangulia kwa bao la dakika ya 53 kupitia Hossam Ghaly aliyestaafu kwa sasa kabla ya Donald Ngoma kuchomoa dakika ya 67 na zile za majeruhi nahodha Abdallah El Said alifunga bao lililoing’oa Yanga.

YANG 01


Uwanja huo umekuwa ukitumiwa na Al Ahly na wapinzani wao, Zamalek kwa ajili ya mechi zote ngumu wakiukimbia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, jambo ambalo Yanga inapaswa kuanza kujiweka sawa kabla ya kuwafuata washindani wao hao wanaolingana nao pointi kwa sasa kundini.

Lakini, ni desturi za timu za Misri kutumia uwanja huo wa pili kwa ukubwa nchini humo kwa ajili ya kuwapelekea mechi mashabiki wa soka wa Kaskazini mwa Misri, na ni wa kisasa wenye urefu wa mita 105 na upana wa mita 70 eneo la kuchezea.

Uwanja huo upo kilomita 1.5 kutoka kituo cha treni na umbali wa kilomita 15 kutoka Alexandria mjini, ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 86,000 walioketi na unalo paa moja tu lililofunikwa kwa ajili ya VIP, ukiwa eneo la jangwani katika mkondo wa Cairo-Alexandria.

Borg El Arab licha ya kuwa na kila kitu cha kisasa japo umejengwa zamani, huwa haujai mashabiki kwa sababu wale wa Alexandria siyo waendaji uwanjani tofauti na ilivyo Cairo.

Ni uwanja wa kisasa mno licha ya mwonekano wake wa kizamani, ukiwa na huduma zote za kisasa na za viwango vya juu ikiwamo migahawa, maduka, vyoo na kila kitu ni kizuri.

Kama vilivyo viwanja vingi vya Misri, uwanja huu umejengwa kwenye ubunifu na usimamizi wa jeshi la Misri, na ni wa pili kwa ukubwa nyuma ya Misr unaoingiza watu 90,000 na ni wa pili pia kwa umaarufu baada ya baada ya Cairo International ukiwa karibu mno na Bahari ya Mediterrania.

YANG 03


Licha ya kuonekana ni mkakati maalumu kwa wenyeji kulipeleka pambano hilo Borg El Arab, lakini mabosi wa Yanga ni kama wameshtukia mapema kwa kuanza maandalizi ya kucheza huko wakitanguliza watu kuweka mambo sawa, wakisubiri kikosi kuondoka Jumatano.

Yanga itakuwa na saa zisizopungua 48 kabla ya kuvaana na Al Ahly inayoongoza msimamo kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa na matano na kufungwa mawili wakati Yanga imefunga moja tu ilipoichapa AS FAR Rabat kwa bao 1-0 Zanzibar.

Ahly msimu huu mechi zake za kimataifa zimekuwa zikichezwa kwenye Uwanja wa Al Salaam uliopo jijini Cairo unaochukua mashabiki 30,000, ambapo hapo walizipeleka JS Kaylie ya Algeria na kuifunga 4-1 kisha Aigle Noir hatua ya mtoano waliposhinda 1-0.

Mechi mbili za nyuma ambazo Yanga ilicheza dhidi ya Ahly ilitumia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo unaochukua mashabiki 75,000 kwenye michezo iliyopigwa Machi Mosi, 2024  bao 1-0 kisha ule wa Machi 9,2016 mabao 2-1 ambazo zote Waarabu hao walishinda.

Yanga imepanga kuondoka nchini alfajiri Jumatano ambapo ikitua Cairo moja kwa moja itawahi Alexandria kabla ya kukutana na Ahly Ijumaa ya Januari 23, kisha usiku huohuo itarejea Cairo baada ya mechi ili kurudi nchini tayari kwa pambano la marudiano dhidi ya Waarabu hao Januari 30 Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

YANG 02


Taarifa kutoka Misri ni kwamba Ahly inataka serikali ya Misri isaidia kuiongezea mashabiki kutokana na ukubwa wa uwanja ili iweze kukabiliana na Yanga ambayo wanajua haina presha na mashabiki kwenye viwanja vya Cairo na Al Saalam.

Bosi mmoja wa juu wa Yanga ameliambia Mwanaspoti kwamba walishazipata taarifa hizo za hesabu za Ahly ambapo hawana wasiwasi watapambana na Waarabu hao kwenye uwanja wowote nchini humo.

“Hayo mambo tulishayasikia muda mrefu walishakuwa wanatuma maombi ya kubadilisha viwanja kule CAF, wakakubaliwa ila tunajua hofu yao. Wanalenga kuongezewa mashabiki wengi ingawa bado hawajajibiwa ila tunasubiri. Tutakwenda kupambana nao kwenye uwanja wowote,” amesema bosi mmoja wa juu wa Yanga.

Yanga itatanguliza watu wawili leo Jumamosi wanaokwenda kusimamia kila hatua ya maandalizi ya kuipoikea timu nchini humo ambapo mmoja atakuwa Cairo na mwingine Alexandria.