Polisi Mbeya Wakamata Watuhumiwa wa Mauaji ya Watoto Watatu – Video



Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Doto Lubongeja, mkazi wa Madundasi wilayani Mbarali, kwa tuhuma za mauaji ya kinyama ya watoto watatu wa familia moja kwa kuwanyonga shingo kisha kuiba mifugo yao.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Januari 15, 2026, katika Kijiji cha Madundasi. Watoto waliopoteza maisha ni Petro Amosi (8), Samu Amosi (6), na Nkamba Amosi (4). Inadaiwa kuwa mtuhumiwa aliwavizia watoto hao wakiwa peke yao wakichunga ng’ombe jirani na nyumbani kwao na kuwaua kabla ya kutokomea na mifugo.

Akizungumza na wanahabari leo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Wilbert Siwa amesema baada ya kutekeleza mauaji hayo, Lubongeja alitoroka na ng’ombe 15 na kwenda kuzificha kwa mjomba wake, Masoda Kurwa, katika Kijiji cha Madundasi “B”. Wahusika hao walifanikiwa kuwauza ng’ombe hao kwa thamani ya Shilingi milioni 5.1.

Kufuatia msako mkali uliofanywa na askari wa uchunguzi, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wote wawili (Lubongeja na Kurwa). Aidha, Polisi wamefanikiwa kuwapata ng’ombe wote 15 walioibwa na fedha taslimu Shilingi 5,100,000 zilizotokana na mauzo hayo ya haramu.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa tamaa ya mali ndiyo chanzo kikuu cha unyama huo. Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha upelelezi ili kuwafikisha watuhumiwa mahakamani haraka iwezekanavyo.