KAMA unakumbuka jana Mwanaspoti lilikueleza kuhusu kutibuka kwa dili la kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua kutuatika Raja Casablanca ya Morocco na kudokeza kuwa hata hivyo hatasalia klabuni hapo kutokana na kuuzwa klabu nyingine ya Uarabuni.
Sasa imebainika kwamba nyota huyo aliyemaliza akiwa kinara wa mabao Msimbazi na Ligi Kuu Bara msimu ulipita kwa kufunga 16 na asisti tisa, ameuzwa CR Belouizdad ya Algeria inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovich.
Lakini, wakati Ahoua anatoka Simba, timu hiyo imefanikiwa kumnasa beki wa kati Osmail Olivier Toure, aliyewahi kuichezea wa Stellenbosch, ili kuchukua nafasi ya Chamou Karaboue aliye mbioni kutolewa kwa mkopo, huku Nickson Kibabage akimwaga wino kuitumikia timu hiyo.
Toure aliitumikia Stellenbosch kwa misimu miwili 2023-2025 kabla ya kupelekwa FC Baniyas ya falme za Kiarabu (U.A.E).
Awali, Mwanaspoti liliripoti kuwa Ahoua anaondoka Simba kumfuata aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ambaye ndiye aliyemsajili klabuni hapo na kufanya naye kazi kwa msimu mmoja kabla ya kocha huyo Msauzi kurejea Raja na alikuwa akimpigia hesabu kumpeleka huko.
Hata hivyo, kitendo cha kocha huyo kumsajili nyota wa kimataifa wa Morocco aliyewahi kutamba na timu za Frankfurt na Schalke 04 katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), Aymen Barkok kilifanya dili hilo kukwama.
Licha ya dili hilo kukwama, lakini inaelezwa Ahoua hakuwa na furaha kusalia Msimbazi, na bahati nzuri Ramovich alikuwa akimmezea mate na alipojua haendi Raja akaharakisha kumsajili baada ya CR Belouizdad kumalizana na mabosi wa Simba.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa ofa ya Ahoua kwenda Raja Casablanca iliyeyuka kutokana na kukosekana kwa maelewano ya pande mbili, na mchezaji tayari alikuwa anataka kuondoka, hivyo baada ya ofa hiyo mpya umefanyika uamuzi wa haraka.
“Ahoua aliomba kuondoka na alikataa kuongeza mkataba mpya akisisitiza yupo tayari hata kuvunja mkataba wa miezi sita uliobaki ili aweze kuondoka. Hivyo kutokana na hayo ili klabu iweze kuambulia kitu tumefanya haraka kukamilisha dili hilo,” mmoja wa vigogo wa Simba ameliambia Mwanaspoti na kuongeza:
“Kiungo huyo ambaye alikuwa mfungaji wetu bora wa msimu anaondoka kwenda CR Belouizdad, biashara baina ya pande zote imekamilika na kwenda vizuri. Tunamtakia kila la heri na tunathamini mchango wake ndani ya timu yetu.”
Kiongozi huyo amesema kuondoka kwa kiungo huyo ilikuwa wazi na walishaanza kufanya uamuzi wa kutafuta mbadala wake ambaye tayari wapo katika hatua nzuri za kukamilisha usajili.
“Hili jambo la kuondoka kwa Ahoua sio jipya licha ya kwamba tulikuwa na uhakika wa kubaki naye kutokana na mkataba, lakini mchezaji asingefanya vizuri kutokana na kutokuwa tayari, hivyo uamuzi wa kumuachia ni bora kwa maslahi ya timu,”€ amesema na kuongeza:
“Hakuna muda wa kupoteza tayari mbadala wake mazungumzo kati ya klabu na klabu yanaenda vizuri na muda wowote kabla ya dirisha kufungwa atatangazwa kuziba nafasi ya kiungo huyo.”
Mwanaspoti lilipojaribu kudodosa juu ya jina la kiungo mpya, kiongozi huyo amesema muda bado na mambo yakienda vizuri watatoa taarifa lakini kwa sasa timu inapambana katika mazungumzo na klabu anayoitumikia.
Lakini, chanzo chetu kikizungumzia usajili wa beki wa kati kilithibitisha kumalizana na mchezaji ambaye kimemtaja kuwa ni pendekezo la benchi la ufundi huku kikisita kutaja jina lake pia.
Mwanaspoti linafahamu usajili kuwa ni nyota wa zamani wa Stellenbosch, Toure ambaye alishawahi kufanya kazi na kocha wa Simba, Steve Barker huko Sauzi. Inaelezwa ujio wa Toure unailazimisha Simba kumtafutia timu ya mkopo, Chamou Karaboue ingawa haijafahamika anaenda wapi.
Simba ina mabeki wa kati watano akiwamo Abdulrazak Hamza aliye majeruhi, Rushine de Reuck, Wilson Nangu, Vedastus Masinde na Chamou.
WAWI 04
Katika hatua nyingine Simba imekamilisha dili la kumsajili beki wa kushoto wa Singida Black Stars, Nickson Kibabage kama Mwanaspoti lilivyoripoti mapema, na alikuwa njiani kujiunga na kambi ya timu hiyo ambayo kesho itashuka uwanjani kuvaana na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Kibabage aliyewahi kuitumikia Yanga, ametua ili kusaidiana na Anthony Mligo aliyesajiliwa msimu huu kutoka Namungo kuziba nafasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyetua Yanga.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa mchakato wa kumnasa Kibabage umekamilika kwa kusaini mkataba, na kuanzia leo ataungana na timu hiyo kwa mechi zilizopo mbele zikiwa za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Eseperance ya Tunisia.
“Kibabage yupo Dar es Salaam hakusafiri na Singida Black Stars kwenda Dodoma ambapo timu yake imeenda kucheza mchezo wa Ligi Kuu (uliopigwa jana), hii ni kutokana na kutaka kukamilisha mpango wake wa kuitumikia Simba,” kilisema chanzo.
“Kibabage ni mchezaji wa Simba kuanzia sasa, na atavaa uzi mwekundu na mweupe. Tunatambua uwezo alionao ataweza kuisaidia timu kufanya vizuri kwani tayari ana uzoefu wa kutosha kutokana na kucheza mashindano mengi ndani na nje.”
Msako wa beki wa kushoto umefanyika baada ya kocha mkuu, Steve Barker kuonyesha uhitaji mkubwa wa mchezaji wa nafasi hiyo kutokana na Mligo kukosa uzoefu mkubwa, lakini Naby Camara aliyetajwa kasajiliwa kwa ajili ya nafasi hiyo anaonekana anamudu zaidi maeneo mengine ikiwamo kiungo na hivyo, Mligo kukosa wa kumpiga tafu.
Uongozi wa Simba umevutiwa na Kibabage ukiamini ndiye mtu sahihi anayeweza kuziba pengo la Tshabalala au kuimarisha eneo hilo, kutokana na uzoefu wake katika Ligi Kuu Bara.
Simba inakabiliwa na mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Esperance itakayovaana nayo mechi mbili mfululizo kuanzia Januari 24 na 30, baada ya awali kupoteza mechi mbili za Kundi D mbele ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali.
Timu hiyo pia kwa misimu minne mfululizo haijawahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho (FA), jambo ambalo limewafanya mabosi kupambana ili angalau msimu huu wafute machozi ya mashabiki kwa kurejesha mataji hayo yanayoshikiliwa na Yanga.