TAWA YASAINI MIKATABA MITANO YA UWEKEZAJI YENYE THAMANI YA ZAIDI YA DOLA MILIONI 24 ZA MAREKANI

 

. ………

Na Beatus Maganja, Dar es Salaam

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) leo tarehe 16 Januari, 2026 imesaini mikataba mitano (5) ya uwekezaji katika sekta ya uhifadhi na utalii yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 24,996,672 sawa na takribani Shilingi Bilioni 63 za Kitanzania, na Kampuni ya GBP Trading Ltd, katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mikataba hiyo inahusisha uwekezaji wa huduma za utalii katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA yakiwemo Hifadhi ya Mpanga–Kipengere (mikataba miwili), Hifadhi ya Kijereshi (mikataba miwili) na Hifadhi ya Wami–Mbiki (mkataba mmoja), lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza mapato na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali zilizopo katika maeneo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania, hatua aliyoeleza kuwa imeongeza idadi ya watalii na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Nchi yetu imepata heshima kubwa duniani baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kufanya Royal Tour iliyopelekea ongezeko kubwa la watalii kutoka Millioni 1.5 mpaka Millioni 2.2 Kwa watalii wa nje na watalii wa ndani kufikia millioni 3.2 na Kwa takwimu za Novemba 2025 zinaonesha Idadi ya watalii wameongezeka Kwa asilimia 9” amesema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa sekta ya utalii nchini iko imara na ni wakati sahihi kwa wawekezaji kuwekeza, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mifumo rafiki na sera bora zinazoendelea kuwavutia wawekezaji, huku Wizara ikiendelea kusimamia utekelezaji wa sera hizo ili kuhakikisha uwekezaji unakuwa na tija kwa Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Rajab Semfuko, alisema mikataba hiyo ni kielelezo cha utekelezaji wa mikakati madhubuti ya kuongeza mapato ya mamlaka hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo utaongeza vitanda 190 vya malazi ya watalii na kuingiza wastani wa Shilingi Bilioni 9.2 kwa mwaka.

Aidha, naye pia alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za dhati za kuvutia wawekezaji katika sekta ya utalii, akieleza kuwa jitihada hizo zimeendelea kuleta manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi.

Vilevile, Semfuko alieleza kuwa TAWA imeandaa Mkakati wa Kuongeza Mapato wa miaka mitano (2025–2030) unaolenga kuiwezesha mamlaka hiyo kujitegemea kifedha ifikapo mwaka 2027/28 kwa kuzalisha Shilingi Bilioni 189 kwa mwaka kupitia uboreshaji wa miundombinu ya utalii, uanzishaji wa mazao mapya ya utalii na uimarishaji wa vyanzo vya mapato vilivyopo.

Naye Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Bw. Mlage Yussuf Kabange, alisema mbali na mapato yatakayopatikana na kuingia Serikalini, mikataba hiyo ina vipengele vinavyonufaisha moja kwa moja jamii zinazozunguka hifadhi husika, ikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii na kuchangamsha shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.

Kabange aliahidi kuwa TAWA itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa wawekezaji ili kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa, huku akizitaka sekta binafsi na wadau wengine kuchangamkia fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika maeneo mbalimbali yanayosimamiwa na TAWA kwa manufaa ya uhifadhi endelevu na maendeleo ya Taifa.