Anayedaiwa kujinyonga mahabusu kuzikwa leo akiacha maswali 10 tata

Moshi. Wakati maziko ya kijana Michael Rambau (19) ambaye polisi wanasema alijiua kwa kujinyonga akiwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi yakifanyila leo, Jumamosi, Januari 17, 2026, maswali 10 tata bado hayajapata majibu juu ya mazingira ya kifo hicho.

Kijana huyo ambaye ni fundi bomba na dereva bodaboda mkazi wa mtaa wa Karikacha, kata ya Rau, mkoani Kilimanjaro anadaiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu alikokuwa akishikiliwa Januari 13, 2026 kwa tuhuma za kumjeruhi baba yake mdogo kwa kumpiga bapa la panga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 14, 2016 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa mtuhumiwa huyo pia alikuwa anatuhumiwa kumuua baba yake mzazi Novemba 22, 2025 kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni na kisha kutoroka hadi alipokamatwa Januari 13, kwa tuhuma za kumshambulia na kumdhuru baba yake mdogo, Brian Felix.

Msemaji wa familia hiyo, Today Rambau alisema kijana huyo (marehemu) alitofautina na baba yake mdogo, alipochukua spana za gari la marehemu baba yake, aliyefariki Novemba 22, mwaka jana.

“Michael (marehemu) alikamatwa Januari 13, kwa tukio la kumshambulia baba yake mdogo kwa kumpiga na bapa na kupelekwa kituo cha polisi,” alisema msemaji huyo wa familia.

“Hili tukio ni tukio la mshituko sana kwa sababu mtu amechukuliwa leo (Januari 13) halafu unapewa taarifa eti kajiua ndani ya mahabusu, hili sio jambo la kufurahisha hata kidogo,” alisema baba mdogo wa marehemu katika maelezo yake juu ya tukio hilo.

Familia hiyo pia ilikana kufahamu tuhuma za kujana huyo kumuua baba yake na kuwa alikuwa ametoroka, suala ambalo linaongeza maswali juu ya tukio hilo.

Miongoni mwa maswali yanayoibuka ni:

1. Polisi wanasema Michael alijiua kwa kutumia mkanda, je, ilikuwaje akaingia mahabusu na mkanda wakati washukiwa huamriwa kuuvua pamoja na viatu akingali kaunta?

2. Ilikuwa mshukiwa akapokewa na kuwekwa mahabusu bila kufanyiwa upekuzi kama inavyofanyika kwa wengine?

3. Kweny mahabusu aliyowekwa alikuwa peke yake au alichanganywa na mahabusu wenzake?

4. Kama alikuwa amechanganywa na mahabusu wenzake, ilikuwaje wasimzuie mwenzao kujinyonga au hata kuwajulisha askari?

5. Kama alikuwa chumba cha peke yake, kwa nini aliwekwa peke yake wakati kosa alilokamatwa nalo lililikuwa la kujeruhi, ambalo kimsingi lina dhamana?

6. Kama mahabusu wenzake hawakusikia wala kumuona mwenzao akijinyonga, polisi waligunduaje kuna mahabusu amejinyonga na ni wakati gani waligundua

7. Kujinyonga kunaendana na purukushani, ilikuwaje kijana huyo akajinyonga bila kusikika purukushani ambazo zingewashtua polisi?

8. Mahabusu ya kituo hicho na kaunta ya polisi hauzidi umbali wa meta 10 au 20, inawezekanaje mtu ajinyonge bila polisi kusikia purukushani hizo?

9. Kwa nini mazingira ya kujinyonga mbona hayajafafanuliwa na uchunguzi umefikia wapi?

10. Polisi wanasema alichukuliwa na kuhojiwa, alihojiwa wapi, kwa muda gani na alirudishwa mahabusu muda gani?