Wadau wampa Rais Samia nondo tano ahadi ya kuliponya taifa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutamka azma ya kulikarabati, kulijenga upya na kulihuisha Taifa baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, wachambuzi wa masuala ya siasa wameibua mambo matano wanayosema ni muhimu kufanikisha dhamira hiyo, yakibebwa na utashi wa kisiasa.

Kauli hiyo ya Rais Samia alitoa juzi Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, wakati wa hafla ya kufungua mwaka pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alirejea nyakati ngumu ambazo Tanzania imepitia tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Oktoba 29, huku akitoa wito kwa mabalozi kushirikiana na Serikali kwa kuheshimu uhuru na mamlaka ya Taifa.

Siku ya uchaguzi mkuu, kulizuka maandamano yaliyotawaliwa na vurugu na kupelekea uharibifu wa mali na watu kadhaa kuuawa kwa risasi na wengine wakijeruhiwa.

Wakizungumzia ahadi hiyo ya Rais Samia, wachambuzi hao wamesema Serikali inapaswa kushirikisha makundi mbali, kukomesha matukio ya utekaji na kulichukulia suala kama ajenda ya kitaifa inayohitaji uamuzi wa pamoja. 

Said Miraji, mmoja wa wachambuzi wa siasa na masuala ya jamii, amesema kauli ya Rais Samia ni ahadi na ipo siku anaweza kuulizwa na Watanzania kuhusu utekelezaji wa ahadi hiyo. 

“Lakini siamini kama Rais Samia anaweza kusimama mbele ya mabalozi na kutoa ahadi isiyotekelezeka, bila shaka ana dhamira ya kutaka kuitekeleza,” amesema.

“Ili kutimiza hayo, yafuatayo yafanyike: Kwanza utashi wa Rais Samia uwepo, Serikali na chama anachotoka (CCM) waichukulie kama ajenda inayohitaji uamuzi. Isichukulie jambo hili, kama la mtu binafsi, bali liwe la Serikali na CCM ili kulitekeleza,” amesema Miraji.

Miraji amesema kuna haja ya Serikali kukaa na kufanya majadiliano na jamii kupitia makundi mbali mbalimbali, kwa sababu hivi sasa jambo kubwa lililo mbeleni ni mustakabali wa Taifa.

  “Kuna suala la kuzungumza na vyama vya siasa ili kupata maelewano, kuna jamii ya wasomi na watu dini. Ukichunguza migogoro yetu ya kisiasa imehusisha makundi mengi ya vijana, wanasiasa, wafanyabiashara, wasomi na watalaamu,” ameeleza.

Hata hivyo, Miraji amedokeza kuwa mchakato si mwepesi bali unahitaji ushirikino na mchango wa kila Mtanzania ili kupata mustakabali wa Taifa.

  “Wasiotaka kushiriki katika hili, basi watampa sababu Rais Samia na ipo siku atasema mimi nilijitahidi, nilitaka kulifanya hili, lakini wenzangu hawakutaka kuniunga mkono na kunisaidia,” amesema Miraji.

Wakati Miraj akishauri hayo, Profesa George Kahangwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) amesema kwa nyakati tofauti Rais Samia amekuwa akitao ahadi kama hizo, basi Watanzania wanasubiria kwa hamu utekelezaji wake.

“Si jana (Alhamisi), suala la maridhiano ameliongea mara kadhaa, ingawa kila anapozungumza kuna kuwa na maswali. Wapo Watanzania wanaouliza anataka kuridhiana na nani?

“Pengine anavyoendelea kulizungumza hili, itafika mahali atasema hayo maridhiano ni kati ya nani na nani? Ni bora amesema mapema ili wale wanaotaka kuridhia wajiandae kutoa maoni yao mapema,” amesema Profesa Kahangwa.

Hata hivyo, Profesa Kahangwa amesema, “pengine Rais anaendeleza ufafanuzi kwa kile ambacho Watanzania tulishangaa na jumuiya za kimataifa ilishangaa. Hatukuwahi kupita katika hali ile ya Oktoba 29.”

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Rainery Songea amesema ili Rais Samia atimize ahadi hiyo, anapaswa kuanza na wanasiasa kupitia vyama vyao.

“Ili kupata maridhiano sahihi lazima ukae na vyama vya siasa kikiwemo Chadema, ukiondoa CCM kwa sasa chama chenye watu wengi ni Chadema,” amesema Songea.

 Songea amedai kuna mvutano wa baadhi ya viongozi wa dini, ukienda Katoliki kuna sintofahamu kuhusu maoni yao kutofanyiwa kazi, vivyo hivyo kwa Waislamu kuna watu wamegawanyika kuna Bakwata na zile taasisi zingine za zilizopo chini yake.

 “Huu mgawanyiko lazima Serikali ikae kwa pamoja, tukubalianetukae na vyama vya siasa, taasisi zote za dini na wananchi. Twende mbele na kurudi nyuma, kwa yale yalitokea, vyama vya siasa huwezi kuvitoa kwenye mazungumza ya mwafaka,” amesema.

 “Jambo jingine linalowaumiza Watanzania ni kutopata majibu kuhusu utekaji, lazima ifike mahali kama Taifa tupate suluhisho la kukomesha matukio ya aina hii,” ameeleza Songea.

Akitoa maoni yake kupitia andiko lake lililosambazwa katika mitandao ya kijamii, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, amesema hotuba ya Rais Samia imepiga hatua moja mbele.

Hata hivyo, Dk Bagonza amemshauri Rais Samia kuzingatia masuala mbalimbali ikiwemo kukubali Oktoba 29 kuna kitu hakikwenda sawa na kuna watu hawakuonekana.

 “Ni jukumu lake kutoa hesabu, namsihi akubali kuna kitu hakikwenda sawa. Awajue, awape pole, nao awaahidi kuwa haitatokea tena, familia zionyeshwe walipo Taifa litapona na Rais atapona,” ameandika Askofu Bagonza.

Ameongeza: “Rais ametoa pole kwa kukata intaneti na ameomba radhi. Akaahidi kuwa jambo hilo halitarudiwa tena. Vema. Lakini kukatika kwa intaneti kuliruhusu mambo mengine kufanyika. Kuna vifo, kuna vilema, kuna hasara za kiuchumi. Mwandishi wa hotuba awakumbuke hawa safari ijayo. Uhai ni bora kuliko intaneti.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza la Kuu la Kiislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka ameshauri Watanzania wajenge moyo wa kuaminiana na kupeana nafasi ili yaliyoelezwa na Rais Samia yatekelezwe.

“Ili kutekelezwa hayo, kunahitaji mtu apewe nafasi, pia apewe moyo kwa kile atakachokifanya. Kwa hiyo Taifa linahitaji kujenga moyo wa kuaminiana, kusaidiana, kushirikiana na kuweka mbele masilahi ya taifa,” amesema.

“Tumefarijika kwa Rais Samia kuonesha nia njema ya kile anachotaka kukifanya na kilichotokea kimetusikitisha, kimetuhuzunisha na kutufedhesha sote, kwa sababu hatukuyatarajia,” amesema Sheikh Mataka.

Sheikh Mataka amesema siku zote dhamira njema ni kujifunza kwa yale yaliyotokea, hivyo yameshatokea, Watanzania wakae chini ili kuridhiana na kujengeana imani na kuaminiana.

“Tukiishi maisha ya kuwekeana shaka na kutuhumiana, hatuwezi kulijenga Taifa, lazima tuaminiane na tusaidiane,” amesema.