Vifo vya watu wakiwa ndani peke yao vyashtua

Dar es Salaam. Matukio ya watu kufariki dunia wakiwa ndani ya nyumba walizoishi peke yao na miili kugundulika baadaye yanatia hofu na kuibua maswali kuhusu usalama na mshikamano wa kijamii.

Alhamisi Januari 15, 2026, mkazi wa Igodima, jijini Mbeya, Zainabu Mwalyepelo, mwalimu na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CUoM), alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa maelezo ya familia, Mwalyepelo alikuwa na changamoto ya kiafya na kutokana na hali yake hakupenda kukaa maeneo yenye kelele, hivyo alikuwa akiishi pekee.

Tukio hilo si la kwanza na wala si la mwisho. Februari 25, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mkoa wa Kagera, wakili Seth Niyikiza, alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake mjini Bukoba, mkoani Kagera.

Kifo chake kiligundulika baada ya mmoja wa wateja wake kuona inzi wengi dirishani, huku majirani wakihisi harufu mbaya ikitoka ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi peke yake.

Vivyo hivyo, Novemba 24, 2024, John Lema (57), mkazi wa Mtaa wa Sokoni, jijini Arusha, alikutwa akiwa amekufa ndani ya nyumba yake, ikisadikiwa kifo kilitokea takribani siku nne kabla ya mwili wake kugundulika. Mwili wake ulikuwa umeanza kuharibika.

Haya ni baadhi ya matukio yaliyoripotiwa na mamlaka husika kwa umma, lakini yapo mengine ambayo husalia kuwa simulizi mitaani.

Akizungumza na Mwananchi, Januari 16, 2026, mkazi wa Goba, mkoani Dar es Salaam, Ephrahim Elias, anakumbuka msiba wa binamu wa baba yake ambaye alifariki dunia bila ndugu kujua kwa muda mrefu.

“Binamu wa baba alifariki dunia, ilichukua takribani wiki mbili kabla ya kugundulika. Alikuwa anapigiwa simu bila mafanikio, ndugu wakaanza kuulizana kuhusu alipo, lakini hakuna aliyekuwa na taarifa zake,” anasimulia.

Anasema baada ya juhudi za kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio, uamuzi ulifikiwa wa kwenda nyumbani kwake, ndipo ilipobainika alishafariki dunia muda mrefu, takribani wiki mbili tangu alipoanza kutafutwa.

“Nyumbani alikuwa akiishi peke yake,” anasema.

Matukio haya yanaonyesha changamoto zinazowakabili watu wanaoishi peke yao, ambao ugonjwa au kifo vinaweza kutokea bila msaada wa karibu kutoka kwa familia au jamii.

Hali ikiwa hivyo, baadhi ya watu wanaoishi peke yao wanasema hulazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira ya kazi, masomo au changamoto za kiafya, licha ya kutambua hatari zinazoweza kujitokeza.

“Nikiugua usiku sina mtu wa kunipeleka hospitali ninachofanya ni kupiga simu kwa ndugu au rafiki ambao nahisi watanipa msaada wa haraka. Sina namna, naishi peke yangu kutokana na mazingira, kukaa na watu inataka moyo,” anasema mkazi wa Ubungo, Jumanne Said.

Kwa upande wake, Christina Alex, mkazi wa Tabata, wilayani Ilala, anasema wakati mwingine wanaishi wenyewe kwa sababu ya masharti ya nyumba wanazopanga.

Anaeleza wapo wenye nyumba wasiotaka watu wengi kwenye nyumba zao, ambao huhitaji mpangaji anayeishi peke yake.

“Si kwamba tunapenda kuishi wenyewe, wakati mwingine tunakutana na masharti magumu kutoka kwa mwenye nyumba. Hataki ndugu, marafiki wala wenza na upatikanaji wa nyumba ulivyo mgumu inabidi kukubali masharti,” anasema.

Anasema licha ya kuishi peke yake amekuwa na utaratibu wa kuongea na ndugu zake kila siku kwa ajili ya kujenga mazoea ya mawasiliano ambayo yatamweka salama endapo atapata changamoto yoyote.

Clara Makoko, mkazi wa Kiluvya, wilayani Ubungo anasema si kwamba anapenda kuishi pekee, tatizo ni kuwa hana ndugu wa kuishi naye.

“Tumezaliwa watano, watoto wa ndugu zangu bado wanasoma, kijana wangu anafanya kazi mkoani. Kuishi na kijana wa kazi pia ni changamoto kwa kuwa hakuna shughuli za kufanya nitamlipa mshahara wa bure na kuongeza gharama za maisha,” anasema.

Makoko anasema anachofanya ni kuishi vizuri na jirani yake ambaye huwasiliana naye wakati wote ili kujuliana hali.

“Nikitoka nahakikisha nimemuaga jirani yangu. Tumetengeneza mazingira ambayo mtu asipomuona mwenzake kwa saa kadhaa ni lazima atampigia simu au kutembelea nyumbani kujua kulikoni,” anasema.

Kauli ya serikali ya mtaa

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Mwingamno, anasema matukio ya watu kuishi peke yao na kufariki dunia bila kugundulika mapema yanatia wasiwasi kiusalama na kijamii.

“Wapo wanaoamua kuishi peke yao kwa mtindo wao wa maisha, hawapendi kuishi na jamii wala kuwa na majirani. Mtu wa aina hii anaweza kufariki na hakuna anayejua hadi harufu inapoanza au nyumba kuonekana imefungwa muda mrefu,” anasema.

Mwingamno anasema baadhi ya watu huamua kuishi wenyewe kwa hiari, huku wengine wakilazimishwa na masharti ya wenye nyumba.

Mbali ya vifo, anasema haki hiyo huongeza hatari za uhalifu, kwani mtu anayeishi peke yake ni rahisi kuvamiwa au kufanyiwa uhalifu bila msaada wa haraka kutoka kwa majirani.

Anasema viongozi wa mitaa mara kadhaa hushughulikia matukio hayo na kutoa suluhisho la kuyaepuka.

“Tunashauri wamiliki wa nyumba kuajiri walinzi au kuhakikisha mtu wa karibu anakuwa na taarifa za wakazi, mlinzi anaweza kutuambia mzee yupo au hayupo, leo hajatoka, simu haipokei. Tukiona hali hiyo inaendelea kwa muda, tunaanza kuchukua hatua mapema,” anasema.

Anatoa mfano wa tukio la mwaka 2015 lililotokea Kigamboni, akieleza mwanafunzi wa chuo alifariki dunia akiwa peke yake ndani ya chumba na hakugundulika hadi rafiki yake alipofika baada ya simu kutopokewa.

Anasema tukio hilo limechangia juhudi za elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuishi pamoja au angalau wawili.

“Tunashauri wasipangishe mtu mmoja, hasa vijana na mabinti waishi wawili wawili ili waweze kusaidiana na kutoa taarifa mapema panapotokea changamoto. Kwa zaidi ya miaka 10 sasa, hatujashuhudia tukio kama hilo tena. Mshikamano wa kijamii ni nguzo muhimu ya usalama na ustawi wa wananchi,” anasema.

Mtaalamu wa saikolojia, Clara Mwambungu, anasema kuishi mwenyewe bila mtandao wa kijamii huongeza hatari ya msongo wa mawazo na kuchelewa kupata msaada wa kitabibu.

“Upweke wa muda mrefu humfanya mtu kujitegemea kupita kiasi, hali inayopunguza mawasiliano na ndugu, marafiki na majirani na kuamini kila kitu anakiweza bila msaada wa mtu mwingine,” anasema.

Mwambungu anasema watu wa aina hiyo huamua kukaa kimya pindi wanapokuwa na dalili za ugonjwa, jambo linalosababisha kuchelewa kufika hospitalini au kupata msaada.

Hali hiyo anasema wakati mwingine huleta madhara makubwa au kifo kisichogundulika kwa wakati.

Mwambungu anasema maisha ya aina hiyo huchangia jamii kutotambua hatari mapema ambazo dalili zake ni kama kutokujibu simu au kutoonekana kwa siku kadhaa, ambazo mara nyingi huchukuliwa kuwa kawaida, lakini tatizo linapokuwa kubwa ndipo linaibua taharuki.

Anashauri kuimarishwa uhusiano wa kijamii akieleza: “Watu wanaoishi wenyewe wanapaswa kujenga mazoea ya kuwasiliana mara kwa mara na mtu wa karibu.”

“Jamii pia irejeshe utamaduni wa kujali majirani. Hatua hizi zinaweza kupunguza matukio ya wagonjwa kuugua au kufariki dunia kimya kimya, hivyo kuokoa maisha,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Katavi, Joseph Ndunguru, anasema jamii imepoteza utamaduni wa kufuatiliana na kujali majirani, hali inayochangia matukio ya watu kuugua au kufa bila msaada.

“Leo kila mtu ana shughuli zake, ukimya wa mtu hauchukuliwi kama tatizo mpaka harufu au tukio kubwa litokee, huu siyo utamaduni wetu,” anasema.