Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema uuzwaji wa vileo pamoja na vinywaji vyenye sukari nyingi kwa gharama nafuu katika baadhi ya nchi duniani, unachochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
WHO imetaja kiwango cha chini cha kodi katika bidhaa hizo kama moja ya sababu ya bidhaa hizo kuuzwa kwa gharama nafuu, jambo linalosababisha kuongezeka kwa magonjwa hayo kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, saratani na mengineyo ya aina hiyo.
WHO imeyaeleza hayo katika taarifa yake kwa umma iliyoitoa Januari 13, 2025 baada ya uzinduzi wa ripoti zake mbili za kimataifa, ikitaja makundi ya vijana na watoto kuathirika zaidi na magonjwa hayo.
Katika ripoti hizo WHO imetoa ushauri kwa nchi mbalimbali duniani kuongeza kodi na ushuru katika vinywaji hivyo pamoja na vilevi, jambo ambalo litasaidia kuongeza mapato ya serikali na kupunguza matumizi ya bidhaa hizo.
Imesema fedha iztakazopatikana zitasaidia kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za afya kwa umma.
Ripoti hizo zinaeleza soko la kimataifa la vinywaji vyenye sukari na vileo huzalisha faida ya mabilioni ya dola kwa kampuni, lakini Serikali hupata sehemu ndogo tu ya mapato hayo, huku jamii zikibeba gharama za muda mrefu za kiafya na kiuchumi.
Kwa mujibu wa WHO, angalau nchi 116 zimeweka kodi kwa vinywaji vyenye sukari, nyingi zikilenga soda pekee. Hata hivyo, bidhaa nyingine zenye sukari nyingi kama juisi za matunda asilimia 100, vinywaji vya maziwa vilivyotiwa sukari na kahawa au chai zilizo tayari kunywa mara nyingi hazitozwi kodi.
Ingawa asilimia 97 ya nchi zinatoza kodi kwa vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) na hali hiyo haijabadilika tangu ripoti ya mwaka 2023.
Ripoti nyingine inaonyesha nchi 167 zinatoza kodi kwa vinywaji vyenye kilevi huku 12 zikikataza pombe kabisa.
Pamoja na hatua hizo, pombe imeendelea kuwa nafuu au bei yake kubaki palepale katika nchi nyingi tangu 2022, kutokana na kodi kutorekebishwa kulingana na mfumuko wa bei na ukuaji wa kipato.
Mvinyo hautoziwi kodi katika angalau nchi 25, nyingi zikiwa barani Ulaya, licha ya hatari zake za kiafya kuthibitika.
Taarifa hiyo pia inabainisha kuwa sehemu ya kodi katika bei ya pombe bado ni ndogo, ikikadiriwa asilimia 14 kwa bia na asilimia 22.5 kwa vinywaji vikali.
Kodi za vinywaji vyenye sukari ni ndogo zaidi na hazilengi soko lote, zikichangia takriban asilimia 2 tu ya bei ya soda ya kawaida duniani.
“Nchi chache hurekebisha kodi kulingana na mfumuko wa bei, hivyo kuruhusu bidhaa zinazoathiri afya kuendelea kuwa nafuu, kadri muda unavyopita,” amesema.
Akitoa maoni yake kuhusu ushauri huo wa WHO kwa nchi mbalimbali duniani, Mtaalam wa Lishe, Sylvia Senkoro amesema kabla ya kupitia na kutekeleza ushauri huo ni vyema kufanyika kwa utafiti wa kina kuhusu uhusiano uliopo kati kiwango cha kodi, gharama ya bidhaa hizo pamoja na usababishaji wake ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
Senkoro amesema utafiti ni muhimu kwa sababu, si wote wanaotumia vibaya aina hizo za bidhaa hadi kiwango ambacho kinaweza kusababisha madhara makubwa.
“Utafiti huo unatakiwa kujikita katika kuangalia ni watu gani haswa wanatumia bidhaa hizo na kwa kiwango gani na sababu zipi, ili kujua ni kwa kiwango gani utadhibiti kwa kutumia njia sahihi,” amesema.
Pia ameshauri pamoja na mambo mengine amesisitiza utoaji wa elimu kwa wingi kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ili waweze kufanya maamuzi yaliyosahihi.
“Elimu hiyo itolewe kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, mtaa hadi jamii kwa ujumla kwa kuwa ndiyo njia kubwa itakayosaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema.
Kauli ya Senkoro inaungwa mkono na mtaalamu wa Lishe, Lucy John ambaye anaeleza kuwa kuongeza kwa kodi pekee katika aina hiyo ya bidhaa, hakutasaidia kupambana na magonjwa hayo kama wananchi watakuwa hawana elimu ya kutosha.
Amesema ili kukabiliana na magonjwa hayo uwekezaji zaidi unapaswa kufanyika katika kutoa elimu kwa umma.
“Kuna pombe, vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi vinauzwa kwa gharama kubwa sana, lakini bado vinanunuliwa kwa wingi, ndio maana ninasisitiza zaidi uwekezaji katika elimu,” amesema.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa na utaratibu wa kutoza kiwango kikubwa cha kodi kwa vinywaji baridi na vilevi kwa kila lita moja inayozalishwa au kuingizwa nchini.
Vilevile katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilibainisha kuanzisha vyanzo vya mapato kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa Wote na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kupitia vinjwaji hivyo.
Vyanzo hivyo vya mapato ni pamoja na Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.
“Sh20 kwa lita kwa bia zinazotambulika kwa Heading 22.03; Sh30 kwa lita kwa mvinyo unaotambulika kwa Heading 22.04, 22.05, na 22.06; Sh50 kwa lita kwa pombe kali na vinywaji vingine vinavyotambulika kwa Heading 22.08.