Dodoma. Chama cha Wafanyakazi Wakusanya Mapato Tanzania (Tarewu) kimefanya matembezi ya mshikamano kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya wakusanya mapato na walipa kodi, hatua inayolenga kukuza uelewano, amani na ushirikiano katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa matembezi hayo, leo Januari 17, 2026 Mwenyekiti wa chama hicho, Rutufya Mtafya, amesema chama hicho kinawaunganisha wafanyakazi wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwemo kodi, ada na ushuru mbalimbali.
Amesema chama kinaamini katika mshikamano na ushirikiano na jamii kama njia ya kuhakikisha uendelevu wa uchumi, uwekezaji na biashara.
“Tumeandaa matembezi haya kwa lengo la kuwaweka karibu wadau wetu ambao ni walipa kodi, tunaamini mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania atakuwa katika usalama na amani endapo ataona mlipa kodi anaendelea vizuri katika shughuli zake za kiuchumi,” amesema Mtafya.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kupata mapato ya uhakika endapo kutakuwa na ushirikiano mzuri kati ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, wafanyabiashara na wawekezaji.
Kwa upande wake, Tumaini Kichila, Mwenyekiti wa Uchaguzi wa chama hicho, amesema kabla ya matembezi yaliyofanyika leo Jumamosi chama kilifanya uchaguzi wa kuwatafuta viongozi wakuu wa taifa watakaokiongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kichila ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi nyingine kuzingatia misingi ya demokrasia, uhuru na haki wakati wa uchaguzi, akisema kukosekana kwa misingi hiyo husababisha kukosekana kwa amani miongoni mwa wananchi na viongozi wao.
Nao wafanyabiashara na walipa kodi wamesema matembezi hayo yamewasaidia kuondoa hofu na kujenga kujiamini baina yao na wakusanya mapato.
“Awali tulikuwa tunawaogopa hadi kufikia kufunga maduka yetu, lakini leo matembezi haya yametusaidia kuuliza maswali na kuona kuwa wao ni watu wa kawaida, tumeelewa kuwa kulipa kodi ni wajibu wetu,” amesema mfanyabiashara Muntazi Kilimani.