Tanga. Bandari ya Tanga imesema madereva wa magari ya mizigo wana nafasi kubwa ya kunufaika na biashara ya usafirishaji wa magari yanayopitia bandarini hapo iwapo watajenga uaminifu na kufanya kazi zao kwa uadilifu na weledi.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, wakati wa uzinduzi wa Chama cha Madereva wa Magari ya Transit Mkoa wa Tanga (Chamata), chenye wanachama zaidi ya 400.
Mbega amesema kwa wastani magari kati ya 600 hadi 800 hushushwa Bandari ya Tanga kila mwezi, yakihitaji kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Mtu anakupa gari lake la thamani ulipeleke Zambia au Kongo. Kama hauna uaminifu na uzoefu wa kufanya kazi hii, haiwezekani. Nawaomba muwe waaminifu na mfanye kazi kwa weledi ili wateja wajenge imani nanyi,” alisema Mbega.
Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega akizungumza wakati wa uzinduzi wa chama Cha madereva wa Transit mkoa wa Tanga
Ameongeza kuwa endapo madereva watazingatia maadili na kujenga imani kwa wateja, malalamiko yaliyokuwepo kuwa Bandari ya Tanga hainufaishi madereva wa ndani yataondoka.
“Kilio chenu kwamba Bandari ya Tanga haiwanufaishi madereva wa Tanga kitaisha. Kwa idadi ya magari 600 hadi 800 kwa mwezi, kila mmoja ana nafasi ya kupata kazi endapo mtajenga imani,” alisisitiza Mbega.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Transit Taifa, Adam Mwenda, amesema awali biashara ya usafirishaji wa magari ilikuwa ikifanyika kiholela, hali iliyosababisha upotevu wa vimpuli na vifaa vya magari, huku lawama zikielekezwa kwa mamlaka ya bandari.
“Kupitia chama chetu, tutahakikisha dereva anayesafirisha gari amekaguliwa, ana taarifa zake kamili pamoja na wadhamini wake, kama njia ya kumhakikishia mteja usalama wa mali yake,” alisema Mwenda.
Ameongeza kuwa chama hicho kitawajengea uwezo madereva kwa kuwapatia mafunzo ya kitaaluma, ikiwemo elimu ya mipaka ya kimataifa, lugha za mawasiliano na stadi za biashara, kwa lengo la kuwafanya kuwa madereva wa kiwango cha kimataifa.
Mdau wa sekta ya usafirishaji, Shekue Pashua , amewataka madereva kuongeza bidii na kulinda mali za wateja wao, akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maadili ya kazi.
“Hatutarajii kusikia sampuli au redio ya gari imepotea. Ofisi yetu itachukua hatua kali za kinidhamu kwa atakayekiuka taratibu, ikiwemo kumvua fursa ya kazi, kwa lengo la kulinda heshima ya tasnia na kukuza Bandari ya Tanga,” alisema Shekue.
Hatua ya kuanzishwa kwa Chamata inalenga kumaliza kilio cha muda mrefu cha madereva wa Tanga, waliokuwa wakilalamikia kupoteza fursa za usafirishaji kwa madereva kutoka nje ya mkoa huo.