UHONDO wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena usiku wa leo kwa kupigwa mechi moja ya kiporo kati ya wanafainali wa Kombe la Mapinduzi 2026, Azam FC na Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi inazikutanisha timu zenye upinzani mkali, lakini zikiwa zinalingana pointi kila moja ikiwa na tisa, japo zinatofautiana idadi ya mechi ilizocheza.
Coastal ambao ni wageni wa mechi hiyo imecheza mechi nane, wakatyi Azam ikiwa na na mitano na kila moja imeshinda mara mbili na kutoka sare tatu, isipokuwa Wagosi wamepoteza mechi tatu ilihali Wanalambalamba haijaonja uchungu wa kufungwa hadi sasa kama ilivyo kwa Yanga.
Hii ni mechi ya kisasi kwa Wagosi kwani wanakumbukumbu ya kupoteza mechi ya mwisho kwenye uwanja huo msimu uliopita ilipolala bao 1-0 kabla ya kubanwa nyumbani kwa kutoka suluhu ziliporudiana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Februari 19 mwaka jana.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa hili litakuwa ni pambano la 25 kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu tangu 2011, kwani tayari zilishakutana mara 24, huku Azam ikishinda mara 13 dhidi ya mara nne za Wagosi na mechi nyingine saba zikiisha kwa sare ikiwamo ya mwisho ya msimu uliopita.
Katika mechi tano zilizopita baina ya timu hizo katika Ligi Kuu tangu 2023, Coastal haijashinda mbele ya Azam na ni mechi mbili tu ilijitutumua na kutoka sare, ikiruhusu kufungwa mabao matano na yenyewe kufunga moja tu katika sare ya 1-1 siku ya Machi 06, 2024.
Pia katika mechi nyingine mbili za Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho (FA), Coastal ilipoteza zote kwa vipigo vya 3-0 na 5-2 mtawalia kuonyesha jamaa walivyo wanyonge mbele ya Azam iliyo na safu kali ya ushambuliaji iliyofunga mabao sita na ukuta mgumu ulioruhusu mabao mawili kupitia mechi tano ilizocheza za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Coastal yenyewe katika mechi nane imefunga mabao matano tu na kufungwa sita, hali inayoonyesha leo mabeki wa timu hiyo wa kazi ya kuwazuia Japhte Kitambala mwenye bao moja na Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao mawili na asisti moja sambamba na Nassor Saadun mwenye bao moja na asisti mbili alizotoa wakati Azam inaizamisha Simba kwa mabao 2-0 mechi ya mwisho ya Ligi kwa timu hizo.
Hata hivyo, Coastal licha ya kuwa na wastani usioridhisha wa mabao, lakini ina washambuliaji hatari, Athuman Masumbuko ‘Makambo JR’ na Maabad Maulid wenye mabao mawili kila mmoja, lakini ni timu inayotengeneza nafasi kupitia mashambulizi makali kupitia pembeni.
Kwa aina ya soka na mbinu wanazotumia makocha wa timu hiyo, Mohammed Muya na Ibenge ni wazi mashabiki wanatarajia kupata burudani kwenye Uwanja wa Azam Complex, japo wenyeji wana nafasi kubwa ya kuendeleza ubabe kwa Wagosi ambao mara ya mwisho katika Ligi ilipoteza 1-0 kwa watetezi Yanga ikicheza ugenini siku chache baada ya suluhu na Mashujaa mjini Kigoma.
Azam ina faida kubwa ya kikosi hicho kutoka katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ikipoteza klwa penalti 5-4 baada ya kucheza mechi tano mfululizo bila kupoteza ndani ya dakika 90, huku baadhi ya nyota wake wengine kurejea kutoka michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 walipoenda na timu ya taifa, Taifa Stars iliyotolewa hatua ya 16 Bora.
Hata hivyo, kwa mujibu wa makocha wa timu hizo ni kwamba kila mmoja imejiandaa kukabiliana na upinzani wa dakika 90 na itakayotumia vyema dakika hizo ndio itakayoibuka na ushindi.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi moja itakayozikutanisha wenyeji Simba dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, huku kila moja ikiwa na kumbukumbu ya matokeo tofauti, Simba ikipoteza mbele ya Azam kwa mabao 2-0, ilihali Wakata Miwa wakitoka suluhu kwenye uwanja huo dhidi ya JKT Tanzania.