BENCHI la ufundi la Alliance ya Mwanza limemaliza mkataba wa mwaka mmoja liliosaini msimu uliopita, huku likisubiri uongozi uamue kuanza mazungumzo ya mkataba mpya au kuliachia likatafute changamoto kwingine.
Alliance Girls inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake kwa zaidi ya misimu nane mfululizo, inaongozwa na Kocha Mkuu, Sultan Juma, msaidizi Amani Luambano na wa makipa, Masoud Bakari ambao msimu uliopita walichukua mikoba iliyoachwa wazi na Ezekiel Chobanka aliyetimkia Ceassia Queens ya Iringa.
Sultan Juma na wenzake msimu uliopita waliiongoza Alliance kumaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake, na msimu huu katika mechi nane wanashika nafasi ya nne nyuma ya vigogo Simba Queens, JKT Queens na Yanga Princess.
Timu hiyo imeshinda mechi tano, sare moja na kupoteza mbili, huku ikipachika mabao saba na kuruhusu saba, ambapo imevuna alama 16.
Hata hivyo, kumekuwa na tetesi za uongozi wa timu kufikia makubaliano ya kutoendelea na benchi la ufundi, huku ukihaha kutafuta mbadala katika dirisha dogo la usajili litakalofungwa Januari 30, 2026.
Chanzo cha kuaminika ndani ya uongozi wa Alliance Girls kililiambia Mwanaspoti kuwa taarifa za kutotaka kuongeza mkataba na benchi lao la ufundi ni za uongo na zinapaswa kupuuzwa, kwani wanafanya juhudi za kumalizana na makocha hao .
Alisema uongozi una nia ya kuendelea na makocha hao kwani wamekuwa na mwenendo mzuri wa matokeo ndani ya timu hiyo, hivyo taarifa zinazoendelea kusambaa zinapaswa kupuuzwa kwani ni jambo la kawaida wakati wa usajili.
”Ukweli ni kwamba mkataba unaisha, ila mazungumzo ya kuendelea nao bado yapo tunataka wabaki. Stori nyingine ni labda wanajiongezea thamani siku ambayo tutakaa mezeni watake ofa kubwa,” kilisema chanzo hicho.
“Labda wanajitangaza kwa timu nyingine, lakini sisi hatuwezi kuwaacha kiwepesi hivyo. Lakini ikitokea wakapata ofa kubwa ambayo itakuja kuzidi yetu inawezekana wakatoka.”
Naye Kocha Mkuu wa Alliance Girls, Sultan Juma alikiri mkataba wake kumalizika ndani ya timu hiyo na kwamba anachosubiri ni kufanya mazungumzo mapya na waajiri wake ambao mpaka sasa hawajamtafuta.